PAROKIA MPYA YAZINDULIWA DODOMA
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Theresia
wa Mtoto Yesu Nzinje jimboni humo huku akiwataka wakristo kulitumia ipasavyo Kanisa
la parokia hiyo kwa kuwatumia mapadri kubariki ndoa, kubatiza na kupata huduma
nyingine za Kanisa.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika
homilia yake kwenye adhimisho la kutabaruku Kanisa na kutangaza parokia mpya ya
Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Nzinje.
Amesema kuwa wakristo hao wana kila
sababu ya kumshukuru Mungu kupata parokia, kumbe wanalo jukumu la kuhakikisha
wanapata huduma za kiroho kanisani hapo pamoja na masakramenti mbalimbali.
Askofu Mkuu Kinyaiya amefafanua
kwamba waamini hao hawana budi kuwa wamisionari wa kulitangaza neno la Mungu na
kuwavuta wakatoliki wengine kufika kanisani hapo kusali.
“Ndugu zangu leo tunapotabaruku
Kanisa hili, lazima tujue ni nyumba ya Mungu, hivyo basi litumike kwa kazi yake
Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Askofu Mkuu Kinyaiya.
Askofu Mkuu Kinyaiya amewashukuru na
kuwapongeza waamini wote wa parokia hiyo kwa majitoleo yao ambayo walitumia
nguvu kwa ajili ya kusomba kokoto, mchanga na rasilimali fedha kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.
“Nina kila sababu ya kuwashukuru kwa
yote mliyoyafanya hasa kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili, na pia nashuhudia
sasa mnajenga nyumba ya mapadri hongereni nyote,” amesema Askofu Mkuu Kinyaiya.
Ibada ya misa takatifu kwa ajili ya
uzinduzi wa parokia hiyo imehudhuriwa na idadi kubwa ya waamini pamoja na watu
wenye mapenzi mema akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na mke wake mama
Tunu Pinda na viongozi wa dini mbalimbali.
Wakati huohuo Askofu Mkuu Kinyaiya
amefungisha jumla ya ndoa takatifu nne kwa waamini wa Kanisa hilo.
Amewasisitiza wanandoa hao kutunza
viapo vyao vya ndoa na kuzilea familia zao watakazopewa na Mungu kwa upendo na
maadili ya dini ya kikristo.
Comments
Post a Comment