KANISA LASAIDIA WALEMAVU ARUSHA
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha
Mhashamu Josaphat Lebulu ameongoza Harambee kwa ajili ya kuwasaidia watoto
wenye ulemavu wa viungo mbalimbali vya mwili katika kituo cha Mtakatifu Yohane
Paulo II kilichopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha ambapo zaidi ya shilingi
milioni kumi na saba zimekusanywa.
Harambee hiyo imefanyika hivi
karibuni katika kituo hicho ambacho kipo chini ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha na
kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo mapadri,
wachungaji kutoka madhehebu mengine pamoja na Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa
Arusha Amina Mollel kupitia walemavu .
Akizungumza katika harambee hiyo,
Askofu Mkuu Lebulu amesema kuwa kila mtu ana wajibu wa kuwasaidia walemavu na
wasiojiweza kwa kutowabagua, bali wanapaswa kuonyeshwa upendo na mshikamano
kwani nao ni binadamu kama wengine.
"Jimbo Kuu Katoliki Arusha
tuliamua kuanzisha kituo hiki mwaka 1990 kuweza kusaidia jamii kwa wenye
ulemavu na kushughulikia afya za watu mara baada ya kubaini kwamba wapo walemavu
ambao hawapewi haki zao za msingi na badala yake wanafungiwa ndani wakidhani
kwamba hawana umuhimu katika jamii, hivyo jambo hilo lilitugusa ndipo tukajidhatiti
kuanzisha kituo hiki ambacho kimekuwa mkombozi wa wengi," amesema Askofu
Lebulu.
Amesema kuwa Serikali, Asasi
za kidini, vyama vya kisiasa na jamii wanapaswa kuwaunga mkono huku wakiwa na
moyo wa kusaidia wenye ulemavu kwa kujali afya zao bila kuonyesha dharau juu
yao jambo ambalo litasaidia kuwafanya kuwa na amani ndani ya nafsi zao kwani
wanapotengwa wanajisikia vibaya.
Naye Mbunge wa viti maalumu (CCM)
Mkoa wa Arusha kupitia walemavu Amina Mollel ambaye ametoa milioni mbili na magunia
tano ya mahindi, akielezea historia ya maisha yake kwa simanzi kubwa
amesema kuwa naye ni mlemavu wa mguu tangu akiwa mtoto mdogo wa miaka
miwili na kwamba kufikia hatua hiyo amekutana na changamoto nyingi ambazo
zilimfanya aweze kutimiza ndoto zake.
"Mimi ni mlemavu, kabila langu
ni mmasai na mama yangu ni kabila la mrangi, kipindi nikiwa mdogo mama yangu
alitaka kutengwa kutokana na mila potofu, jamii iliniona siyo mtu halali lakini
familia yangu iliniombea na kunisaidia mpaka hivi sasa kuwa Mbunge vitu maalumu
kwakweli namshukuru sana Mungu amenitoa mbali, ni historia ndefu kwa hiyo
niwatie moyo walemavu wenzangu msikate tama." Amesema Amina Mollel huku
akijifuta machozi.
Aidha amesema kuwa jamii nyingi
zimekuwa na mawazo potofu kwamba mlemavu si lolote na ni mkosi na wengine
wamekuwa wakiwaua bila hatia kwa madai kuwa siyo riziki jambo ambalo ni dhambi
kubwa mbele za Mungu kwani mlemavu ana haki sawa na binadamu mwingine, bali ni
tatizo tu ambalo ni mpango wa Mungu.
Hata hivyo ametoa wito kwa uongozi
wa kituo hicho kuunda kikundi cha walemavu ili waweze kupewa asilimia ya pesa
inayotolewa na mfuko wa walemavu Halmashauri huku pia akiitaka jamii kuunda
mtandao wa marafiki wa kituo hicho ambao watakuwa wakiwasaidia walemavu kwani
taasisi nyingi tayari zinafanya hivyo.
Akisoma Risala, Mratibu wa kituo hicho
cha walemavu, Mireile Kapilima amesema kuwa kwa sasa kituo kinahudumia walemavu
zaidi ya 20,000 wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro, Simanjiro, Arumeru na
Karatu huku lengo likiwa ni kutoa huduma za elimu kwa walemavu ili waweze
kujikimu kimaisha wanapotoka hapo, kutoa elimu kwa jamii kutambua haki za
mlemavu na kumjali.
“Kupitia kituo hiki kumekuwa na
matokeo chanya kwa jamii kwani kwa kiasi fulani kumesaidia kupungua kwa
unyanyapaa, kujitokeza wazazi kuwaleta kupata huduma za matibabu na wengine kuchangia
gharama kidogo.”
Hata hivyo amesema bado kuna
changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho ikiwa ni uendelezaji wake kwani kwa
asilimia kubwa wanategemea wafadhili wa nje ambao wamekuwa wakipunguza bajeti
siku hadi siku, hivyo kuiomba jamii kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja
kuwasaidia watoto hao kwani huduma ya chakula, malazi na matibabu inakuwa
tatizo.
Comments
Post a Comment