AMUCTA KUONGEZA UFAULU WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU
CHUO Kikuu kishiriki cha Askofu Mihayo Tabora AMUCTA na
shirika toka nchini Uholanzi la KENTALIS wameendesha semina kwa walimu 25 wa
shule za Sekondari ndani ya Manispaa ya Tabora kwa ajili ya watoto wenye
matatizo ya kusikia na kuongea hivi karibuni Tabora.
Akiongea na Blogi hii juma hili, Mkurugenzi wa Kitivo cha
Elimu Dr. Sr. Sophia Mbilije amesema chuo na shirika la Kentalis wameamua kutoa
semina hiyo kwa walimu wa sekondari ili kusaidia kuinua ufaulu wa watoto
wenye tatizo la kusikia na kuongea.
Aidha katika semina hiyo wameandaa mtaala ambao watauweka
katika kanzi data ili walimu na wanafunzi wote katika shule 19 za Tanzania
zenye watoto wenye mahitaji maalumu waweze kupata ujuzi utakaowasaidia
kujipatia elimu.
Katika Kanzi data hiyo walimu wamefundishwa kuweka, kuchukua
na kutumia picha, michoro, na vielelezo vingine lengo likiwa kuwasaidia watoto
hao wenye matatizo ya kusikia na kuongea waweze kuelewa mada zinazofundishwa
madarasani na hatimaye ufaulu wao uweze kupanda.
Aidha Dr. Sr. Mbilije amesema wao na shirika hilo la Uholanzi
wamelenga wanafunzi wa kidato cha kwanza na nne katika masomo ya sayansi, hii
ikienda sambamba na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano yaani Tanzania ya
viwanda.
Walimu waliopata bahati ya kupata semina hiyo ni kutoka
shule za sekondari ndani ya Manispaa ya Tabora na chuo cha ualimu Tabora (T.T.C).
Semina hiyo ilihudhuriwa na wahadhiri na wahadhiri
wasaidizi wa chuo kikuu cha AMUCTA-Tabora ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa
na wawezeshaji toka ndani na nje ya Tanzania.
Zoezi hilo
litakuwa endelevu katika Mkoa wa Tabora na hasa lengo kuu likiwa kuandaa wataalamu
wa masomo ya sayansi hususani watoto wenye mahitaji maalumu.
Comments
Post a Comment