SHIRIKA LA MABINTI WA MARIA LAPONGEZWA
PADRI Alfred Lwamba wa
Jimbo Kuu Katoliki Mwanza amelipongeza shirika la Masista la Mabinti wa Maria
kwa kazi nzuri wanayofanya ndani ya Kanisa na kwa jamii yote kwani licha ya
mambo ya kiroho pia wamekuwa wakitoa huduma nzuri kwenye
sekta ya elimu na afya pamoja na kuwapatia malezi bora watoto
wanaosoma katika shule zao.
Pongezi hizo amezitoa baada ya
misa takatifu kwenye sherehe ya ufunguzi wa jengo la utawala la ghorofa
mbili la shule ya Sekondari ya Lumala iliyopo Jimbo Kuu Katoliki Mwanza
inayoendeshwa na shirika la Mabinti wa Maria ambako wamekuwa wakitoa malezi na
elimu bora kwa watoto wanaosoma hapo.
Padri Lwamba amesema uwekezaji
uliofanywa na shirika hilo katika huduma za jamii hasa elimu na afya ni
kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla na wamekuwa wakitimiza
wajibu huo katika kuwalea watoto kimaadili mema na maarifa yatakayowasaidia
baadaye katika kulitumikia Taifa.
Amesema elimu inayotolewa katika shule
ya Lumala kuanzia chekechea, msingi hadi Sekondari kidato cha nne ni elimu bora
na malezi mema ya kiroho kwa watoto wote bila ubaguzi
wa kidini.
Padri Lwamba amewahimiza wazazi
na walezi kuwekeza zaidi katika kuwasomesha watoto kwa sababu wakitaka wawe
madaktari, marubani, walimu na wataalamu mbalimbali ni lazima watumie fursa
kuhakikisha wanawasomesha watoto.
“Hata maadiko matakatifu katika
Biblia yametwambia kuwa “ mshike sana elimu usije ukamwacha akaenda zake” kwa
hiyo ndugu zangu wazazi na walezi tunawajibu wa kuwasomesha watoto
waweze kupata elimu bora,” amesema padri Lwamba.
Nayo jamii ya Jimbo Kuu Katoliki Mwanza
wamelipongeza shirika la Masista la Mabinti wa Maria lenye makao yake makuu
Jimbo Kuu Tabora kwa kazi nzuri wananazofanya katika suala la elimu na malezi
bora kwa watoto wanaosoma katika shule hiyo inayoendesha shirika hilo.
Mzazi Erick Odhiambo ambaye pia
ni Mwenyekiti wa ujenzi akiongea kwa niaba ya wazazi wenye watoto wanaosoma katika
shule hiyo iliyopo parokia ya Ilemela katika Jimbo Kuu Mwanza ametoa pongezi
kwa shirika hilo kwa kujenga shule hiyo na kutoa huduma za kiroho ikiwemo suala
la elimu na malezi bora kwa watoto wao wanaosoma hapo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo
Benjamin Perman amewashukuru wazazi na walezi kwa ushirikiano wao mzuri na
kuahidi kuendelea kutoa elimu bora, malezi mazuri ya kiroho na kimwili
kwa watoto wote bila kujali tofauti za kiimani.
Makamu Mama Mkuu wa Shirika la
Mabinti wa Maria lenye makao makuu Kipalapala Jimbo Kuu Katoliki Tabora Sista Maria
Evodia Lupagaro aliyemuwakilisha Mama Mkuu Theresia Sungi, amesema karama yao
ni upendo, huruma na huduma na ameipongeza jamii na Serikali kwa ushirikiano
wao kwa shirika wanapoihudumia jamii.
Sista Lupagaro amesema wanaishukuru
Serikali kwa kuwapatia kibali cha kuanzisha na kuendesha shule hiyo na imekuwa
ikiwakagua na kuwapa miongozo mbalimbali kielimu katika kuendesha shule lengo
likiwa kuwasaidia watoto wa Taifa la kesho.
Comments
Post a Comment