Maaskofu Katoliki wataka hukumu ya kifo itazamwe upya
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki nchini wameiasa serikali
kubadili sheria inayoruhusu adhabu ya kifo kwa wahalifu badala yake watoe hukumu
ya kifungo cha maisha.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya ameeleza hayo kwa niaba ya Maaskofu Katoliki
Tanzania hivi karibuni huko jimboni TUNDURU-Masasi kwenye ibada ya mazishi ya
Askofu wa Jimbo hilo marehemu Castory Msemwa.
“Leo tunapomzika Askofu Msemwa tunakumbuka kuwa mwanadamu
anazaliwa na anakufa kupitia vifo mbalimbali ukiwemo uzee na magonjwa. Huo ni
mpango wa Mungu kwamba mwanadamu afe ili afike kwenye makao aliyomuandalia.
Lakini kuna vifo ambavyo ni kinyume na mpango wa Mungu
ikiwemo sheria inayoruhusu mahakimu kutoa hukumu ya kifo. Aliye na mamlaka ya
kuchukua uhai wa mwanadamu ni Mungu peke yake kwani uhai ni zawadi kutoka kwa
Mungu.
Sababu ya vifo vinavyotokea duniani ni sisi wanadamu
wenyewe. Maandiko matakatifu yanatuambia Mungu peke yake ndiye ana uwezo na
mamlaka ya kuchukua uhai. Uhai ni kitu kitakatifu lakini baadhi yetu tunapuuza.
Tunafahamu kwamba sheria za nchi nyingi duniani zinaruhusu
mahakimu kutoa adhabu ya kifo ikiwemo Tanzania. Tunaiomba serikali yetu ione namna
ya kubadili sheria hiyo na badala ya kifo, wahalifu wapewe adhabu ya kifungo
cha maisha. Kama taifa tusikubali kuridhia mikataba ambayo haiheshimu uhai,”
amesisitiza Askofu Mkuu Kinyaiya.
Aidha maaskofu pia
wameisisitiza jamii kuacha kutoa mimba kwani ni namna nyingine ya kutoa uhai wa
mwanadamu suala ambalo wamesema ni kosa na ni dhambi kwa anayetoa na yeyote
anayeshiriki. Hivyo jamii nzima ina wajibu wa kuheshimu na kutunza uhai ambao
ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Wamewaonya vijana ambao ni nguvu ya taifa la Tanzania kuacha
kuhatarisha maisha yao kwa kukumbatia utamaduni wa kifo.
“Vijana wanakufa kabla ya wakati wao kwa kudhoofisha miili
yao kwa kutumia sumu mbalimbali kama vile mahusiano ya hovyo hovyo, dawa za
kulevya nk. Wakidhani ndiyo namna ya kupata starehe kumbe wanajiangamiza.
Tatizo la vijana kujiua wenyewe nalo linaongezeka Tanzania.
Kufuatana na ripoti ya Shirika la Afya duniani Tanzania ni kati ya nchi 10
duniani, zinazoongoza kwa watu hasa vijana kujiua.
Wapendwa vijana sisi wazee wenu tunawaasa muachane na huo utamaduni
wa kifo, ishini maadili, maadili mliyofundishwa na Askofu Castory MSEMWA,
mnayofundishwa na viongozi wenu wa dini mkijua kuwa miili yenu ni hekalu la
Roho Mtakatifu,” amesema.
Katika mazishi hayo Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya amesema
kuwa, Maaskofu Katoliki Tanzania pia wametaka jamii itafakari pia kifo cha
mazingira katika dunia wanayoishi.
Katika barua yake ya pili inayojulikana kama ' Laudato Si'
yaani ‘sifa iwe kwako’ Baba Mtakatifu
Fransisko pamoja na mambo mengine anazungumzia jinsi wanadamu wanavyoiua dunia kwa vitendo
mbalimbali. Wanatumia dunia kwa uroho bila mpango kiasi kwamba wanaiua dunia
ambayo ni mama yao.
“Matokeo ya madhara yanaturudia kwa njia ya ukame, ongezeko
la hewa ya ukaa ambalo ni mbaya kwa afya zetu nk. Tutakimbilia wapi tukiiharibu
dunia?
Tunamuasa kila mmoja wenu asiiumize dunia kwa vitendo
visivyofaa, kama vile kukata miti hovyohovyo, kuchoma uoto asilia, kuua wanyama
nk.” amesisitiza Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma.
Ameiasa jamii kuacha kulilia kifo kwani jinsi wanavyomuona
Marehemu Askofu Castory Msemwa ndivyo kila mmoja atakuwa hivyo kwani kuzaliwa
ni bahati na matokeo yake ni kifo ili mwanadamu aende kuishi na Mungu kwenye
makao aliyomuandalia.
“Kuna watu wengi hawajapata bahati ya kuzaliwa duniani kwa sababu
hawakutungwa mimba kabisa na hawakuja duniani kabisa na kwakuwa hawakuja
duniani kabisa hawatakufa kwa sababu hawapo.
Sisi tuliobahatika kuzaliwa duniani hatma yetu ni kufa ili
turudi kwa Baba, hivyo tusilalamikie kifo kwani ni sehemu ya hiyo bahati ya
kuishi hapa duniani.
Tumeambiwa kuwa Askofu MSEMWA amefariki kwa ugonjwa ambapo
Mwenyezi Mungu ameamua kumchukua. Sisi kama wanadamu jukumu letu ni kupokea
mapenzi ya Mungu ijapokuwa ni magumu kama wanadamu. Tuendelee kumuombea.
Ni wakati wetu wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu
Msemwa hapa duniani kwani aliyoyafanya hakuna mtu mwingine ambaye anaweza
kufanya kwani duniani hakuna watu wawili wanaweza kufanana na kufanya jambo
lilelile. Kila mtu ana namna yake ya kutenda, naye alikuwa maalumu.
Tunamshukuru Askofu Msemwa kwa kutumia vipaji vyake
kulitumikia Kanisa na jamii kwa ujumla bila kulalamika. Tunaamini kuwa kwakuwa
alijitahidi kuishi wito wake kama Padri na Askofu Mwenyezi Mungu atampokea
kwake mbinguni.
Suala la msingi ni kuishi ukristo wetu, tuishi maisha ya Sakramenti
ili tujitakatifuze, tuwe watu wa toba tujiandae ili siku moja turudi kwa baba
yetu Mbinguni,” ameeleza.
Amesema kuwa Maaskofu wanashukuru wote waliojitolea kumuuguza
na kujaribu kuokoa maisha ya Askofu Msemwa kuanzia madaktari katika hospitali
ya Taifa Muhimbili, India nk.
Pia anashukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Oman pamoja na
serikali nzima ya Tanzania kwa ushirikiano wa kusafirisha mwili wa marehemu
kutoka Oman hadi Tunduru kwenye maziko.
Amesema Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki wanaungana na wana
Tunduru kufarijiana na kutiana moyo katika kipindi hicho kigumu.
Amewataka mapadri wa Jimbo Katoliki TUNDURU-Masasi kuwa na
ushirikiano wakati huo ambapo wanasubiria wapewe msimamizi wa muda.
“Ni wazi kiti cha Askofu hapa Tunduru Masasi kipo wazi, sasa
ni wajibu wetu kusali na kuomba ili Roho wa Mungu atuchagulie mchungaji
mwingine wa Tunduru Masasi.
Tunawaomba mtunge sala maalumu mtakayoisali kila jumapili
baada ya Misa kwa lengo hilo.
Na wakati tukisubiri Askofu mwingine, sisi Maaskofu
tunawasihi sana mkae kwa amani, upendo na mshikamano,” amesisitiza Askofu Mkuu
Kinyaiya.
Comments
Post a Comment