SIKU YA MTOTO DUNIANI JUNI MOSI,PAPA ATOA WITO


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuhitimisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu, Jumapili tarehe 29 Mei 2016, amewashukuru na kuwapongeza Mashemasi wote waliohudhuria kutoka ndani na nje ya Italia kwa uwepo wao ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu pia ametumia nafasi hii kuwasalimia mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliohudhuria tukio hili la kihistoria, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu amewashukuru kwa namna ya pekee washiriki wa kongamano na hija ya msamaha lililoandaliwa na Chama cha kitume cha Celestino; Chama cha Kitaifa cha utunzaji wa nishati rafiki, kinachoendelea kutoa elimu juu ya utunzaji bora wa mazingira bila kuwasahamu mahujaji kutoka Poland ambao, siku ya Jumapili, wamefanya hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Piekary. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Mama wa huruma kuzitegemeza familia pamoja na vijana wote wanaojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Nchini Italia, Siku ya Jumapili, tarehe 29 Mei 2016 wameadhimisha Siku ya Kitaifa ya Faraja inayopania kuwasaidia watu kuishi vyema wakati mshumaa wa maisha unapokaribia kuzimika, tayari kuingia katika maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, tarehe 1 Juni 2016, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mtoto. Hii itakuwa ni fursa kwa Jumuiya za Kikristo nchini Syria kukaa na kusali pamoja ili kuombea amani na wadau wakuu katika tukio hili watakuwa ni watoto wenyewe. Watoto kutoka Syria wanawaalika watoto wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuungana nao kwa ajili ya kuombea amani duniani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ameweka nia zote hizi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na kwa namna ya pekee, alinde maisha na utume wa Mashemasi duniani kote.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI