AMANI HAIJI KWA BUNDUKI
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa pia ni fursa kwa wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia kukutana na kuadhimisha tukio hili huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amewataka wanajeshi na askari hawa kuwa ni wasmaria wema katika ujenzi wa amani, usalama na upatanisho wa kijamii kwani ulimwengu mamboleo unaonekana kuwa na maadui wengi kuliko hata marafiki!
Maadhimisho ya Jubilei ya vikosi vya ulinzi na usalama imekuwa ni fursa ya kufanya kumbu kumbu ya miaka thelathini tangu Waraka “Huduma ya Maisha ya Kiroho kwa Wanajeshi”, “Spirituali Militum Curae” ulipochapishwa. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya ambalo limepewa dhamana ya kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kuanzia tarehe 29 hadi Mei Mosi, 2016 limefanya Kongamano la kimataifa lililozikutanisha familia za wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Viongozi wakuu kutoka Vatican walishirikisha: tafakari, mawazo, fursa na changamoto zilizopo katika ulimwengu mamboleo, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kujikita katika haki msingi za binadamu! Katika tafakari yake, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican amegusia huduma za maisha ya kiroho zinazotolewa kwa wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kama hija ya “Fumbo la Pasaka” linalowawezesha waamini kutembea katika giza la utupu na mahangaiko ya ndani kama ilivyokuwa Siku ile ya Ijumaa kuu!
Upendo wa Kristo Mfufuka unaendelea kumwilishwa kila siku ya maisha katika mateso na mahangaiko ya wanajeshi na askari ambao wakati mwingine hawana hata mahali pa kulaza vichwa vyao! Huduma hii ya kichungaji ni sehemu ya mchakato unaopania kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika maisha ya watu kuyapatia mwelekeo mpya unaojikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Wahudumu wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama hawana budi kufanya hija na wanajeshi pamoja na askari hawa, daima wakibeba Msalaba wa maisha, utume na dhamana yao, tayari kumfuasa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia na Mlango wa huruma ya Mungu.
Hki ni kielelezo cha Agano Jipya na milele, utimilifu wa Sheria na Amri za Mungu, changamoto ya kutekeleza dhamana hii kwa unyofu mkubwa ili kuwaendea kondoo waliopotea na kutawanyika kama umande wa asubuhi ili kuwaonjesha wote hawa wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Monsinyo Viganò anakaza kusema, imani ya kweli inamfanya mtu kuwa huru kwani katika undani wa mwanadamu kuna kiu kubwa ya maisha ya kiroho yanayopaswa kumwambata Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Lakini haya ni mapambano ya kufa mtu! Kwani Ibilisi daima yuko kazini akitaka kuwatega na kuwaangusha watu ili wamezwe na malimwengu na huko watakiona kile kilichomnyoa Kanga manyoya!
Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia amezungumzia kwa kina na mapana utume anaoutekeleza katika maisha ya wanajeshi na askari pamoja na familia zao; umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, umefika wakati kwa Bara la Ulaya kujikita katika msingi wa amani kwa kuondokana na dhana ya vita ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha mateso na mahangaiko ya wengi.
Kanisa linatambua kwamba, amani ya kweli haiwezi kujengwa kwa mtutu wa bunduki au mkong’oto unaotolewa na askari, lakini amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopokelewa na kufanyiwa kazi kila siku ya maisha kwa msaada wa Mungu! Kumbe, mchakato wa Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo na huruma ya Mungu, mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko.
Wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma, msamaha, haki, amani na upatanisho wa kijamii. Wawe ni watu wa huduma kwa binadamu, hususan kwa maskini, watu wasiokuwa na ulinzi na usalama katika maisha yao; watu wasiokuwa na hatia, wanaotengwa na kunyanyaswa kutokana na sababu mbali mbali!
Askofu mkuu Santo Marcianò anasema, kuna uwezekano mkubwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa karibu zaidi na Jimbo la Kijeshi kwa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji wa ukarimu; kwa kutoa huduma makini inayojikita katika huruma na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji ambao kwa wakati huu wanaonekana kuwa ni kero kubwa Barani Ulaya! Viongozi wa Kanisa wanaweza pia kusaidia mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene ili kutoa kisogo kwa utamaduni wa vita na kinzani zisizokuwa na mashiko wala mvuto! Mambo yote haya yanahitaji majiundo makini na ushirikiano kati ya Kanisa na Vikosi vya ulinzi na usalama, sanjari na kudumisha sala, imani na matumaini.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment