JUBILEI YA MASHEMASI
Mashemasi ni watumishi na mitume wa Kristo wanaotumwa kumtangaza na kumshuhudia Yesu kwa njia ya huduma ya mapendo. Yesu Kristo amejifunua kama Neno wa Baba ambaye amekuja kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, akawa ni chemchemi ya furaha na huduma kwa wote, yaani akawa Shemasi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa kwa watangazaji na wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu kuhakikisha kwamba, wanafuata kikamilifu maagizo ya Kristo Yesu.
Ikumbukwe kwamba, dhamana ya Uinjilishaji ni kwa Wakristo wote na huduma ya upendo ni njia muafaka ya kumwilisha utume wa kumfuasa Yesu, kielelezo cha ushuhuda wa maisha yanayojikita katika huduma. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu, Jumapili tarehe 29 Mei 2016. Ili kuwa kweli ni watumishi wema na waamifu, kuna haja ya kujikita katika dhana ya uwepo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya zawadi ya huduma kutoka kwa Mungu inayotolewa kama sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anawataka Mashemasi kuwa wazi na tayari daima kutoa huduma inayobubujika kutoka katika fadhila ya unyenyekevu wa moyo, huku wakiendelea kushangazwa na Mungu katika maisha ya kila siku. Mtumishi mwema na mwaminifu anafahamu na kutambua dhamana, wajibu na nafasi yake, tayari kuhudumia hata wale wanaokuja kuomba msaada nje kabisa ya muda uliokubalika, kielelezo cha sadaka katika maisha. Kwa njia ya maisha ya kuwajibika, huduma ya Mashemasi itaweza kuzaa matunda ya Kiinjili.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili ya Jumapili ya Tisa ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa inakazia kwa namna ya pekee kabisa huduma ambayo ilitolewa na Yesu kwa kuwaponya wale waliokimbilia huruma na upendo wake. Yesu anashangazwa na maneno yaliyotolewa na Akida kwa kujiona kuwa hastahili kamwe Yesu kuingia katika nyumba yake, lakini aseme neno tu na mtumishi wake atapona. Unyenyekevu huu wa Akida unamgusa Yesu, kielelezo cha mfumo wa maisha ya Mungu ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mungu ni upendo unaojidhihirisha kwa namna ya pekee katika kumhudumia mwanadamu kwa uvumilivu na wema, daima akiwa tayari kuteseka kutokana na dhambi za binadamu. Mungu anatafuta njia itakayomwezesha mwamini kuwa mtu mwema zaidi katika maisha, changamoto kwa Wakristo kumuiga Mwenyezi Mungu ili kuwahudumia wengine; kwa kuwapokea kwa ukarimu, huruma na mapendo; kwa kuendelea kujitahidi kuwafahamu bila kuchoka; kwa kuwasikiliza kwa makini na kuwahudumia kikamilifu.
Mashemasi wakiwa na moyo wa unyenyekevu hapo wito wao kama wahudumu wa upendo, utaweza kukua na kukomaa. Waamini wanakumbushwa kwamba, kila mmoja wao anapendwa na amechaguliwa kwa namna ya pekee na Mwenyezi Mungu; anaitwa na kutumwa kuhudumia, baada ya kuponywa kutoka katika undani wa maisha. Ili kuwa wahudumu wema na waaminifu kuna haja kwanza kabisa kuwa na afya ya kiroho; kwani moyo ulioponywa na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, hauwezi kuwa mgumu na kujifungia katika ubinafsi wake.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mashemasi kumwomba Kristo Yesu, ili aweze kuwaponya, ili kufanana naye kama marafiki na wala si kama watumwa. Mashemasi wawe ni watu wa sala inayowasilisha furaha na matumaini; magumu na changamoto za maisha wanazokabiliana nazo kila siku. Hii iwe ni sala ya kweli inayopeleka maisha kwa Kristo. Pale Mashemasi watakapokuwa wanahudumia katika Ibada ya Misa Takatifu, hapo wataweza kuona uwepo wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili yao, ili wao pia waweze kuwa ni sadaka kwa wengine.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu kwa kukazia utayari katika maisha; unyenyekevu wa moyo na majadiliano endelevu na Yesu katika sala na kwa njia hii, kamwe hawatakuwa na woga wala makunyanzi ya kuwa ni watumishi wa Kristo, tayari kukua na kutoa faraja kwa mwili wa Kristo unaojionesha kati ya maskini wa nyakati hizi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment