HOTUBA YA PAPA JUU YA WANAWAKE MASHEMASHI:VATICAN YATAHADHARISHA
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya habari ya Vatican na Jimbo Takatifu kwa Ujumla, Padre Federico Lombardi, ametoa ufafanuzi juu ya hotuba ya Papa Francisko wakati akikutana na Wakuu wa Mashirika ya Kike , akisema , Papa Francisko hajasema kama analenga kuanzisha utaratibu wa kutoa daraja la ushemasi au ukuhani kwa wanawake bali alikubaliana na Masista kuunda Tume ya kuchunguza zaidi majukumu yaliyofanywa na Mashemasi wanawake katika kanisa la mwanzo.
Padre Lombardi ametoa maelezo haya kufuatia taarifa nyingi za vyombo vya habari, baada ya Papa kukutana na Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Watawa wa Kike, wakati wa kipindi cha maswali na majibu , Alhamisi iliyopita, katika ukumbi wa mjini Vatican, ambamo kati ya mengine pia , alijibu swali lililouliza juu ya uwezekano wa Kanisa kuwa na mashemasi wa kike. Masista Mama Wakuu wapatao 900, walikutana na Papa, kama sehemu ya Mkutano wao Mkuu wa Umoja wao wa Kimataifa, uliokuwa ukiendelea hapa Roma.
Mkutano wa Baba Mtakatifu Francisko na Masista ulidumu kwa muda wa saa moja na nusu, ambamo walizungumzia maswala mbalim mbali juu ya utume na majukumu ya wanawake katika maisha yao kidini. Na Papa alijibu maswali kadhaa nyeti , ikiwemo nini kinachozuia hasa Kanisa kuwapa wanawake hata daraja la Ushemasi wa kudumu , kama ilivyokuwa katika maisha ya Kanisa la mwanzo. Katika jibu lake, Papa alisema, uelewa juu ya jukumu la mashemasi wa kike katika Kanisa la Mwanzo si bayana na hivyo walikubaliana na Masista kwamba , itafaa kuunda Tume ya kuchunguza zaidi juu ya suala hili.
Padre Federico Lombardi ametaja Mkutano huu wa Papa na Masista toka duniani kote, kwamba yalikuwa ni mazungumzo mazuri yenye kutia moyo kuhusu uwepo wa wanawake katika utume wa Kanisa na hasa maisha ya wanawake waliotolea maisha yao huduma ya Kanisa ikiwa ni pamoja na wajibu wao katika nafasi muhimu ndani ya Idara mbalimbali za Kanisa ambako wakfu wa kikuhani hauhitajiki.
Akizungumzia juu ya maoni mengi yaliyotolewa juu ya maelezo ya Papa kuhusu kuunda Tume ya kuchunguza suala la mashemasi wa kike, Padre Lombardi amesema , suala hili limekuwa likiongelewa ndani ya Kanisa hata katika siku za nyuma, kutokana na ukweli kwamba wakati wa Kanisa la mwanzo, kulikuwa na wanawake wanaotajwa kama Mashemasi ambao walifanya kazi fulani ndani ya jamii ya kikristo, lakini majukumu hayo hayakutajwa bayana.
Padre Lombardi anasema kuna haja ya kuwa waaminifu katika jambo hili, wakati tunatoa maoni juu ya maneno ya Papa Francisko, ambamo alitaja juu ya kuanzisha Tume ya kutazama tena suala hili kwa uwazi zaidi, majukumu yaliyofanywa na Mashemasi wanawake wakati wa kanisa la mwanzo . Papa hakusema yeye anakusudia kuanzisha utaratibu wa kuweka mashemasi wa kike na wala hakuzungumzia juu ya Daraja la Ukuhani kwa wanawake. Na kwamba, Papa katika mahubiri yake ya wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Ekaristi , aliweka wazi kwamba suala hili liko nje ya fikra zake.
Padre Lombardi pia amesema ni makosa kupuuzia mengine yote muhimu yaliyozungumzwa na Papa Francisko wakati akikutana na Masista , na kung’ang’ania hoja moja tu ya uwezekani wa Ukuhani kwa wanawake kama vile hapakuwa na mengine hayakuzungumzwa.
Comments
Post a Comment