SHEREHE YA EKARISTI TAKATIFU-MAANA HALISI NI MAANDAMANO
Tunaadhimisha Sherehe ya Mwili na
Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo kila mwaka siku ya Alhamisi inayofuata
baada ya kuadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kwa kuwa Sherehe hiyo ni Sikukuu ya amri, Kanisa imeruhusu kuiadhimisha siku ya Dominika inayofuata ili Wakristo wote waweze kutimiza wajibu wao wa
kusali .
Kuanza na Kuenea
Kihistoria Sherehe hiyo ilianza huko Ufaransa
kutokana na maono ya mtawa Juliana aliyoanza kuyapata mnamo mwaka 1209. Baada
ya juhudi kubwa ya kumwomba Askofu wake kuanzisha Sherehe hiyo, hatimaye ombi la sista Juliana lilipokelwa. Mwaka 1246
iliadhimishwa kwa mara ya kwanza huko Lie’ge
nchini Ufaransa.
Mwaka 1264 Papa Urban IV (wa nne) aliitangaza
Sherehe hiyo iadhimishwe popote katika Kanisa. Kumbe kabla ya kuteuliwa kuwa
Papa, Urban alikuwa shemasi na baadaye
padri wa jimbo hilo la Liege, alishaifahamu historia ya sikukuu hiyo. Papa Urban IV alimwomba Mt.Thomaso wa Akwino(1224-1274)
ambaye alikuwa mtaalamu sana katika elimu ya Mungu kuandika sala na tenzi zote
za Sherehe hiyo. Tunaona utaalamu wake hasa katika Sekwensia ndefu ya Sherehe
hiyo.
Kwa bahati mbaya Papa Urban IV alifariki mwaka huohuo na
kufanya agizo lake kutotekelezwa kwa miaka kadhaa. Alikuwa Papa Klementi V (1264-1314,
ambaye alikuwa Papa kuanzia 1305 katika Mtaguso wa Vienna(1311-1312) aliagiza
kwa mkazo kwamba Sherehe hiyo iadhimishwe potepote katika Kanisa Katoliki.
Pamoja naye, baadaye Papa Yohane XXII (ishirini na mbili) naye alisisitiza
jambo hilo. Sherehe hiyo mpaka miaka ya karibuni ilikuwa ikiitwa: Sherehe
ya Mwili wa Kristo (Corpus Christi). Ni dhahiri kuwa mwelekeo wa Sherehe ulikuwa hasa
kumwabudu Kristu katika Mwili wake kama jina la Sherehe lilivyosimama. Basi
mnamo mwaka 1849 Papa Pius wa tisa aliweka Sikukuu ya Damu Takatifu ya Yesu
ambayo iliadhimishwa Julai 1. Kwa hiyo kulikuwa na sikukuu mbili: Sherehe ya Mwili wa Bwana na Sikukuu ya Damu Takatifu
ya Bwana.
Marekebisho
ya Mtaguso
Katika marekebisho yaliyofanywa na
Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano ni pamoja na kurekebisha Sherehe hiyo. Katika
Katekisimu ndogo tunasoma: Ekaristi Takatifu
ni Sakramenti ya Mwili na Damu takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu - mtu,
katika maumbo ya mkate na divai. Mkate na divai ni alama za Sakramenti.
Kwa vile Sikukuu hizo mbili zilikuwa
na mwelekeo wa kuzitenga alama wazi za Sakramenti hiyo moja Mwili peke yake na Damu takatifu kuadhimishwa katika nafasi tofauti basi marekebisho
ya Mtaguso mkuu yameziunganisha kuwa Sherehe moja. Sasa Sherehe hii inaitwa: Sherehe
ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni dhahiri kuelewa
kwamba mwili ulio hai ni pamoja na damu yake hai pia. Jina hilo ndefu
hufupishwa kwa kusema: Sherehe ya Ekaristi Takatifu.
Maandamano ya Kuabudu
Tangu Sherehe hiyo ilipoanza imekuwa
na utaratibu wa kufanya maandamano pamoja na Sakramenti ya Ekaristi
ikichukuliwa katika chombo maalum kiitwacho monstransi ili kumwabudu Bwana
wetu Yesu Kristo hadharani. Maandamano hayo yamekuwa yakipambwa na bendera
nyeupe na hata rangi nyingine zenye kuvutia pamoja na maandishi ya kumtukuza
Yesu katika Ekaristi. Bendera na vipeperushi hivyo vinapamba sehemu mbalimbali
ya maandamano hayo; yaani sehemu ya watoto, vijana, akinababa na hata
akinamama. Wasichana au pengine akinamama wachache walioandaliwa huwa mbele ya
Ekaristi na kumwaga maua kama ishara ya heshima kubwa kwa Bwana wetu Yesu
Kristo.
Kwa kawaida katika maandamano hayo
huandaliwa kituo kimoja au viwili na hata zaidi kutegemea urefu wa njia ya
maandamano. Katika vituo hivyo Ekaristi itawekwa juu ya meza iliyopambwa vizuri
na waamini husimama au hupiga magoti ili kusali kwa kitambo. Hata iwapo maandamano siyo marefu
inashauriwa sana kuwa na kituo angalau kimoja
kusudi tendo hilo la kuandamana hadharani liimarishwe na sala zinazotolewa na Wakristo
wote kama jumuiya moja inayoabudu. Katika vituo hivyo kuhani huongoza sala kuombea
parokia, Jimbo, taifa na serikali au shida
za jamii kwa jumla.
Sote Tumwabudu
Maandamano hayo na
Ekaristi yasiwe tu kama tendo la haraka kwani ni tendo la kuabudu. Tuandamane
kwa heshima mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo. Inasisitizwa sana kuwepo na kituo
angalau kimoja ambapo waamini wote kwa pamoja watatulia wakiabudu.
Tunawapongeza sana waamini wote
wanaoshiriki maandamano hayo kwa moyo wa ibada na uchaji, wakishiriki kuimba
nyimbo za Ekaristi na nyingine zinazofaa.
Wanaonyesha mfano mzuri wa kudhihirisha imani hadharani. Iwapo kuna Misa mbili
baadhi ya Wakristo walioshiriki Misa ya kwanza huja mwishoni mwa misa ya pili ili wapate
kushiriki maandamano hayo muhimu ya kumwabudu Yesu. Hongera sana kwa kuonyesha
uhai wa imani namna hiyo.
Kwa upande mwingine lakini tumeshuhudia
baadhi ya waamini waliokuwa wakisimama pembeni mwa njia ya maandano na kuongea
bila kushiriki maandamano. Huwaangalia wenzao wanapoandamana na wengine
huendelea na biashara zao. Hilo si jambo zuri kamwe! Ni mara moja tu kwa mwaka
mzima Liturujia imeweka utaratibu wa kumwabudu Yesu kwa namna hiyo. Wakristo wanapaswa
kuvumilia adha ya kuandamana na kujitoa muda wao kwa ajili ya Liturujia hiyo maalum
ya kumwabudu Yesu na kukiri imani
hadharani.
Tendo hilo la kuandamana ni tendo la
kumwabudu Yesu Kristo na kukiri kwa dhati kwamba yeye Mungu - mtu yumo katika Sakramenti
hiyo ya Mwili na Damu yake takatifu. Pamoja na hilo, ni tendo la kumshukuru kwa kudumu na waamini katika Sakramenti hiyo.
Anakaa katika Sakramenti hiyo usiku na
mchana pamoja nasi. Wakristo wangapi
huenda pale kanisani kumwabudu?
Kumpokea Yesu
kwa uchaji
Yesu tunayemwabudu ni pia chakula
chetu cha uzima wa milele. Kwa nafasi
hii inafaa kukumbuka utaratibu wa kupokea Komunyo kwa heshima stahiki. Wakristo
wajiandae vizuri kiroho na hata kuwa safi kimwili kwa kupokea Ekaristi
takatifu. Mahali wanapopokea Ekaristi wakiwa wamesimama mstari wakumbuke
kuonyesha tendo la heshima kama vile kuinama kabla ya kupokea Ekaristi.
Wanaopokea Ekaristi mkononi wakumbuke
kuwa mikono yote miwili iwe
tayari kwa tendo hilo kuu la kumpokea Bwana . Isiwe, kwa mfano, mkono moja unashika leso au simu. Inawapasa kusafisha
kwa ulimi kwenye kiganja pale ilipowekwa Ekaristi takatifu kwa sababu mara
nyingi hubaki chembechembe ambazo
zisiposafishwa kwa ulimi huanguka sakafuni na kukanyagwa. Kumbe chembechembe hizo ni sehemu ya Mwili wa Bwana.
Mkristo akishampokea Yesu katika Sakramenti haitakiwi
kuinama tena bali hurejea mahali pake kwa uchaji na kuabudu kimya kwa kitambo. Halafu
aungane na wenzake katika kuimba. Tendo hili hutendeka mara nyingi basi lifanyike kwa heshima na uchaji.
Asanteni sna kwa maelezo mazuri na yenye ufafanuzi wa kina yananisaidia hata mimi katika kuelezea katika vipindi redioni Mungu awabariki sana.
ReplyDelete