Kardinali Pengo: Muungano si bahati nasibu
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka waamini na
wananchi kwa ujumla kutambua kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si jambo
la bahati nasibu.
Kardinali Pengo ameyasema hayo ofisini kwake hivi karibuni alipoitisha
vyombo vya habari vya Kanisa Katoliki kuzungumzia pamoja na mambo mengine
ongezeko la Parokia mpya jimboni kwake pamoja na mabadiliko kwa Maparoko na
Maparoko Wasaidizi katika baadhi ya Parokia jimboni humo.
Asemema suala la Muungano linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa pekee kwa
kila Mtanzania hasa waamini Wakatoliki na kwamba kila mwamini anapaswa kutambua
kuwa amepewa jukumu na Mwenyezi Mungu kulinda na kuombea Muungano huo.
Kardinali Pengo anasema ni jambo la kushangaza jinsi Mungu anavyotenda
mambo yake kwa wanadamu kwani alileta Imani Katoliki kupitia Zanzibar na kwamba
baada ya Uhuru Mungu aliwapatia neema watu wake wa pande mbili za Zanzibar na
Tanganyika kuungana na kuwa kitu kimoja.
Anasema wakati Kanisa likijiandaa kwa adhimisho la Jubilei ya miaka 150
ya uwepo wa Kanisa Katoliki katika eneo la Afrika Mashariki ifikapo 2018
Zanzibar haiwezi kuwekwa pembeni.
Kuhusu utendaji wa serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Kardinali Pengo anasema hali inaonesha viongozi wa taifa hili
wameanza vizuri na kasi yao inaleta matumaini makubwa.
Kardinali Pengo anawaomba wananchi wa Imani zote kumuombea Rais Dakta
John Pombe Magufuli kwa Mwenyezi Mungu ili alinde uongozi wake na auimarishe
uweze kubaki katika malengo yake ya kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.
Anaongeza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuomba kwa Mungu ili ibilisi
asije akawabadilisha mioyo wale ambao wanaonekana ni watetezi wa wanyonge
wakaanza kutenda kinyume na matarajio ya wananchi walio wengi.
“Ibilisi ana namna yake ya kufanya vitu mnaweza kushutukia tu mambo
yamebadilika wale ambao mnatarajia wawe watetezi wa Watanzania wa chini
wanageuka kuwa ndiyo wakandamizaji wakubwa kwa Watanzania wanyonge.” Amesema
Kardinali Pengo
Ujenzi wa
Nyumba ya Askofu Bagamoyo
Kwa namna ya pekee anawashukuru waamini Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
kwa majitoleo yao ya fedha katika kuhakikisha ujenzi wa nyumba ya Askofu katika
jimbo Katoliki tarajiwa unafanyika kwa mafanikio makubwa.
Kardinali Pengo anasema mpaka sasa amefanikiwa kupata michango kutoka
kwa waamini mbalimbali kiasi cha shilingi milioni miatatu na kidogo ambazo
zimesaidia kuanza kwa ujenzi huo kwa kasi kubwa.
“Naomba kuwashukuru wale wote walioniwezesha kuzipata fedha hizo kwa
ajili ya huo mradi” amesema Kardinali Pengo
Amesema katika kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa Jimbo Kuu Dar es
Salaam kutoka katika akiba yake limetoa shilingi milioni miambili hamsini na
hivyo kufanya idadi ya pesa zilitolewa kwa ajili ya mradi huo kuwa shilingi
milioni miatano na hamsini.
Amesema pesa hizo ni nyingi na zimefanya kazi kubwa lakini hazitoshi
kukamilisha mradi huo kutokana na gharama za ujenzi kuwa kubwa kwa nyakati hizi
hivyo kiasi hicho bado hakitoshelezi kukamilisha mradi huo.
Kutokana na hali hiyo Kardinali Pengo anasema kiasi cha fedha ambacho si
pungufu ya milioni mianne bado kinahitajika na hivyo anaendela kuwasihi waamini
kujitokeza kwa wingi kutoa michango yao ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Anasema matarajio yaliyopo ni kwamba mpaka kufika mwanzoni mwa mwaka
2018 ujenzi huo uwe umekamilika ilikusudi ikimpendeza Baba Mtakatifu aweze
kulipatia jimbo tarajiwa la Bagamoyo Askofu Mpya katika mwaka huohuo
unaotarajiwa kufanyika sherehe za miaka 150 ya Ukatoliki Afrika Mashariki na
kwamna ya pekee nchini Tanzania.
Amesema lengo lake la kuzungumzia juu ya mradi huo ni kuomba ukarimu wa
waamini kwani Maaskofu wa Baraza Katoliki Tanzania waliamua wazo la kupata
Askofu wa Bagamoyo na wazo kumuomba Baba Mtakatifu atengeneze jimbo Katoliki
Bagamoyo kwa mwaka 2018 na uhakikishaji wa kuwa na mahali pa kukaa kwa Askofu
Mpya ni jukumu la Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam.
Amesema kwakuweka nguvu pamoja mradi huo utafanikiwa na kwamba
anawaombea kwa Mungu ili azidishe ukarimu wao na afanikishe maendeleo ya kila
Parokia na pia afanikishe maandalizi ya Jubilei ya miaka miamoja na hamsini ya
Kanisa Katoliki Mashariki mwa bara la Afrika ifikapo mwaka 2018.
Atagaza
parokia mpya
Aidha Kardinali Pengo ametangaza ongezeko la Parokia sita mpya na hivyo
kunalifanya jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam hilo kuwa na jumla ya Parokia
tisini na tano kutoka themenini na tisa za awali.
Parokia hizo mpya ni miongoni mwa vigango kumi na moja ambavyo awali
vilitangazwa kuwa Parokia teule Januari sita mwaka huu wakati wa utoaji wa
daraja takatifu ya Ushemasi kwa Mashemasi wawili wanaotarajiwa kupata
sakramenti ya Upadrisho mapema Julai mwaka huu.
Mwadhama anasema anayomategemeo ikimpendeza Mungu ifikapo Julai mwaka
huu baada ya Upadrisho wa Mapadri wapya wa Jimbo upo uwezekano wa kupata
Parokia nyingine.
Parokia mpya zilizotangazwa na Mwadhama kuwa Mpya ni pamoja na Parokia
ya Kijitonyama ambapo Padri Arnold Babu Tarimo wa Shirika la Kazi za Roho
Mtakatifu (OSS) ameteuliwa kuwa Paroko wa Parokia hiyo, Parokia ya Mshikamano
ambayo itakuwa chini ya uongozi wa Paroko Bartholomew Mrosso Padri wa Shirika
la Wamisionari wa Afrika na Parokia ya Mbande ambayo Paroko wake ni Padri
Pushpa Raj, Padri wa Shirika la Bikira Maria Imakulata (MMI).
Nyingine ni Parokia ya Msakuzi Mbezi Mwisho ambapo Padri Fulgence Oisso
wa Shirika la Rosminiani ameteuliwa kuwa Paroko wa parokia hiyo, huku Padri
Wolfgang Michael Tengia wa Shirika la la Wamisionari wa Clareti akiteuliwa kuwa
Paroko wa Parokia Mpya ya Michungwani Kimara na Parokia ya sita ni Parokia ya
Mtakatifu Rita iliyopo Kimara Temboni ambayo Paroko wake ameteuliwa Padri
Constantine Mlelwa ambaye ni Padri wa Shirika la Mt. Agustino.
Mabadiliko ya
Maparoko
Katika hatua nyingi Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amefanya
mabadiliko ya Maparoko na Maparoko Wasaidizi kwa baadhi ya Parokia za Jimbo Kuu
Dar es Salaam amabapo utekelezaji wa mabadiliko hayo unaanza mara moja Mei Mosi
mwaka huu.
Katika mabadiliko hayo Paroko wa sasa wa Parokia ya Kanisa Kuu la
Mtakatifu Yosefu Padri Theophile Hostie Bolampeti ameamishiwa katika Parokia ya
Manzese kuwa Paroko wa parokia hiyo ambayo awali ilikuwa chini ya uongozi wa
Mapadri wa Shirika la Wasionari wa Afrika (White Fathers)
Pamoja na kwamba Parokia ya Manzese sasa inahudumiwa na Mapadri
wazalendo, kwa namna ya pekee Kardinali Pengo amewaomba Mapadri wa Shirika la
Wamisionari wa Afrika kuendelea kutoa Mapadri Wasaidizi katika Parokia hiyo
hadi mwezi Julai mwaka huu.
Padri Joseph Matumaini ambaye alikuwa Paroko wa Parokia ya Magomeni
ameteuliwa kuwa Paroko Mpya wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu na anaendelea
kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uchungaji Jimbo Kuu Dar es Salaam.
Mwadhama anasema kwakuwa Padri Matumaini ndiye Mkurugenzi wa Uchungaji
jimboni ameona si vyema akae mbali na Mchungaji Mkuu wa Jimbo ambaye ni Askofu.
Hii ni mara ya pili kwa Padri Matumani kushika nafasi ya Uparoko katika
Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kwani aliwahi kuwa Paroko wa Parokia hiyo ya
Kanisa Kuu kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2004 na kabla ya hapo aliwahi kuwa
Paroko Msaidizi kanisani hapo kati ya mwaka 1998 hadi mwaka 1999.
Aidha Padri Christian Likoko ameamishwa kutoka Parokia ya Kizinga na
ameteuliwa kuwa Paroko Mpya wa Parokia ya Magomeni huku Parokia ya Kizinga
ikibaki chini ya uongozi na uangalizi wa Paroko Msaidizi.
“…kule parokiani Kizinga bado hatujapata Paroko lakini yule ambaye
amekuwa Msaidizi katika parokia hiyo anashika majukumu siyo tu ya Usaidizi
lakini pia ya Paroko hadi hapo itakapoonekana ni lazima ama kuweka mwingine au
kumfanya yeye mwenyewe kuwa Paroko” amesema Kardinali Pengo.
Wengine waliamishwa katika vituo vyao vya kazi ni pamoja na aliyekuwa
Paroko Msaidizi Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Padri Asisi Mendonca ambaye sasa
ni Paroko Msaidizi Parokia ya Mtakatifu Petro Oysterbay na Padri Edward Sabbas
aliyekuwa akihudumu kama Paroko Msaidizi Parokia ya Mtakatifu Petro Oysterbay
ameteuliwa kuwa Paroko Msaidizi Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
Comments
Post a Comment