KILI MARATHON ITUNZE NA KULINDA UUMBAJI-DOKTA AIDAN MSAFIRI
Moja kati ya maeneo yaliyoathirika na mabadiliko ya tabia
nchi ni mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro.Ni wazi kuwa nyuzi joto kufikia 35,mvua
za kusuasua na maralia za milimani yote haya yamesababishwa na ukataji na
uchomaji miti pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.
Na hata katika barua yake,Baba Mtakatifu Papa Francis
ameendelea kuikumbusha dunia juu ya wajibu wa wanadamu kutunza na kwa kiwango
kikubwa kuuheshimu uumbaji. Katika sura ya tano ya barua ya Papa
Francis,ameeleza wazi hatua mbalimbali za kuchukua.Bila kuuheshimu uumbaji
hakuna maisha tena.
Mashindano ya Kili Marathoni yenye historia hapa nchini na
nje,mwaka huu yameshirikisha wakimbiaji 8,000 wenye sifa kadhaa lakini zaidi
wenye imani,wanaoamini uumbaji na wanaomuamini Mwenyezi Mungu.
Naamini kuwa mashindano haya yenye heshima kubwa yanaweza kuwa
kielelezo kizuri katika njia hizi,kuwa
chachu ya mshikamano baina ya wanadamu na kuleta amani,kuleta mshikamano na
uumbaji katika kulinda na kuheshimu mazingira,mshikamano wa matajiri na
masikini katika matumizi sahihi ya rasilimali za dunia hii,mshikamano baina ya
imani mbalimbali.
Kielelezo cha Kili Marathoni kina sura hizi,sura ya mlima
mrefu ambao katika biblia Takatifu umeelezwa katika Mika 4:2,Isaya 52:7,kumbe
wakimbiaji ni vizuri wakazingatia na kutafakari kwa kina juu ya kuuhifadhi
mlima Kilimanjaro na mambo ya biblia kiimani.Pia sura ya kukimbia imeashiriwa
katika Isaya 40:31,Wakorintho wa kwanza 9:24 na Waebrania 12:1.
Ili kuweza kutunza na kulinda mlima Kilimanjaro na uumbaji
wa Mungu kwa ujumla,lazima wanakanisa,serikali na wadau wote waweke dhamira ya kufufua na kuendeleza,kuziishi tunu kadhaa
zikiwemo,kiasi,kujali,kuheshimu,hekima,uwajibikaji,maendeleo endelevu yenye
sura ya kibinadamu,mapendo ya kweli kwa Mwenyezi Mungu,wenzetu na uumbaji
Mathayo 22:37-39,huruma kwa masikini,rasilimali,ardhi,maji,misitu na rasilimali
na vizazi vijavyo.
Kwa ufupi baba Mtakatifu Francis katika barua yake ya
kulinda ulimwengu anamwita kila mwanadamu pale alipo kuwa balozi mzuri wa
utetezi wa haki za uumbaji na wanadamu kwa ujumla.Elimu kwa watoto na vijana ni
kipaumbele ili kufikia lengo la Papa Francis.
Ni vizuri mashindano ya Kili Marathoni ya mwaka ujao 2017
yawe na sura za kiimani na kimaadili pamoja na kuwa na sura za utalii wa
kibishara zaidi.Suala la upandaji wa miti 8,000 liwe endelevu pia.
Mwandishi wa makala hii ni balozi wa mabadiliko ya tabia nchi
Tanzania.Anapatikana kwa anuani hii S.L.P 3041 Moshi Tanzania.
Comments
Post a Comment