JUBILEI YA WAKLERI YAANZA KUTIMUA VUMBI MJINI VATICAN
Wakleri na majandokasisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuanzia tarehe 1- 3 Juni 2016 wanaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuungana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi na wito wa Daraja Takatifu, mwendelezo wa utume wa Kristo Yesu katika: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kilele cha Jubilei ya Wakleri na Majandokasisi ni hapo tarehe 3 Juni 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Wakleri Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 25 machi 1995.
Katika barua hii, Mtakatifu Yohane Paulo II kwa namna ya pekee, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa utakatifu wa maisha ya wakleri kama chachu muhimu sana kwenye mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha. Ulimwengu mamboleo unahitaji wainjilishaji wapya, wenye ari na moyo mkuu, wanaofumbata zawadi ya wito na maisha ya kipadre kama hija inayowaelekeza kwenye utakatifu wa maisha. Wakleri watambue kwamba wanayo dhamana ya kuwatakatifuza watu wa Mungu katika huduma yao ya kichungaji.
Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, kutokana na changamoto ya utakatifu wa maisha, kila Jimbo katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, litaadhimisha Siku ya Kuombea Utakatifu wa Wakleri. Tangu wakati huo, Kanisa limeanza kuwa na Mapokeo ya kuwaombea Wakleri katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: chemchemi ya Sakramenti za Kanisa, Hekalu Takatifu la Mungu; Kiini cha upendo na huruma ya Mungu; Utakatifu, hekima na elimu yote. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha amani na upatanisho kati ya Mungu na binadamu na ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utii kwa Baba wa milele!
Haya ndiyo mazingira ambamo Wakleri wanaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tukio ambalo linajikita katika: toba na wongofu wa ndani kwa kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawakumbusha Wakleri kwamba, wanaweza kuwa kweli vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, ikiwa kama wao watakuwa pia watu wa kwanza kufanya toba na kuomba msamaha. Watambue kwamba, kama Wakleri wanashiriki utume wa Kristo Yesu na hivyo wanakuwa ishara halisi wa mwendelezo ya upendo wa Kimungu unaosamehe na kuokoa.
Tarehe 1 Juni 2016, Ratiba ya maadhimisho ya Jubilei ya Wakleri inaonesha kwamba, kutakuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Sakramenti ya Upatanisho ili kuweza kupokea rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu. Kutakuwa na Katekesi na Ibada ya Misa Takatifu kadiri ya makundi ya lugha.
Tarehe 2 Juni 2016 itakuwa ni siku ya mafungo ya kiroho; siku ya ukimya, kusali, kutafakari na kuabudu. Ni wakati wa kujichimbia jangwani ili kukutana na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutoa tafakari tatu kwa Wakleri na baadaye kutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu. Tarehe 3 Juni 2016, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Hii ni Siku ya kuombea utakatifu wa Wakleri. Baba Mtakatifu Francisko, majira ya saa 3:30 asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, iko nawe bega kwa bega kukujuza yale yanayoendelea kujiri katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment