YUBILEI YA MIAKA 100 YA UPADRI - MIKONO YAKE MUHIMU KATIKA KUTAKASA WAAMINI

Hapana shaka kwamba mikono ya mwanadamu ni viungo muhimu sana katika utendaji wa kazi za kila siku. Kadhalika katika kuadhimisha Liturujia, Padri hutumia sana mikono yake. Tunapoadhimisha Yubilei ya miaka 100 ya Upadri Tanzania tutumie  nafasi hii kutafakari utumishi wake wa kikuhani katika kutakasa Wakristo.
Mikono hupakwa mafuta  
Katika Liturujia ya Sakramenti ya Upadri, Askofu akishamwekea Shemasi mikono na kusali  Sala rasmi ya kumweka wakfu,  mteule huwa  Padri mpya. Tendo la kumwekea mikono likienda sambamba na Sala ya kumweka wakfu linafanya kiini cha kupata Daraja ya Upadri. Padri mpya huvishwa stola ya Kipadri na kasula ndiyo mavazi yanayodhihirisha hadhi yake ya kuwa Padri na ni mavazi rasmi ya kuadhimisha Ekaristi Takatifu.
Baada ya kuvishwa mavazi hayo  Padri mpya huja mbele ya Askofu na kupiga magoti. Askofu humpaka mafuta matakatifu ya Krisma katika viganja vya mikono yote miwili na wakati huo husema sala ifuatayo:
 “Bwana Yesu Kristo, ambaye Baba alimpaka mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu, akulinde kwa ajili ya kuwatakasa Wakristo na kumtolea Mungu sadaka”.
Lengo la kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma kwenye viganja vya mikono yake linatamkwa waziwazi katika sala hiyo. Mikono ya Padri inatakaswa ili: mosi, Padri anatakiwa kuitumia mikono yake kuwatakasa Wakristo; na pili ni kwamba inampasa aitumie mikono hiyo kwa ajili ya kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka. Katika maisha ya Padri mikono yake ni viungo vitakatifu ambavyo huvitumia hasa kwa mambo makubwa  yaliyotajwa.  Tuone  nafasi muhimu ambazo Padri anatakiwa kutumia mikono katika kuwatakasa Wakristo.
Sakramenti ya Ubatizo
Padri kama kuhani hufanya utumishi kwa kutumia mikono yake  kuwatakasa Wakristo kwa nafasi mbalimbali. Tuzione nafasi hizo katika mfululizo wa mtu tangu anapokuwa Mkristo.
Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi huitwa Sakramenti za Kuwaingiza watu katika Ukristo. Katika Sakramenti ya Ubatizo  Mkristo hutakaswa na kuondolewa dhambi zote na kupata Neema ya utakaso kwa mara ya kwanza. Kwa Sakramenti hiyo pia hutiwa muhuri au alama isiyofutika rohoni mwake na kuwa mwana wa Mungu na mwana- Kanisa.
Ingawa Sakramenti hiyo huweza pia kuadhimishwa na Shemasi, na katika hatari ya kufa mtu yeyote anayejua kubatiza, lakini Padri ambaye mikono yake imetakaswa, huitumia katika kutakasa watu. Anatumia mikono kuwapaka Wakatekumeni Mafuta ya Wakatekumeni, kumwaga maji kichwani wakati wa Ubatizo na iwapo ni watoto wanaobatizwa huwapaka pia Krisma takatifu. Kwa kufanya vile Padri huwatakasa watu.
Sakramenti ya Kipaimara
Katika Sakramenti ya Kipaimara Askofu au Padri akitumwa na Askofu hutumia mikono yake katika kutoa Sakaramenti. Hunyosha mikono yake ili kumwomba Roho Mtakatifu awashukie wale wanaopata Kipaimara.  Tendo la kunyosha mikono juu ya Wakristo limekuwa likitumika tangu enzi za Mitume kama ishara ya kumwomba Roho Mtakatifu:
“Walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao” (Mdo 6:6).  Wakristo wapya wa Samaria walipelekewa Petro na Yohane nao waliwaombea Roho Mtakatifu. “Ndipo wakaweka mikono yao juu yao nao wakampokea Roho Mtakatifu”(Mdo 8:17). Tendo la kunyosha mikono wakati wa kutoa Sakramenti ya Kipaimara ni ishara muhimu sana. Tazama pia sehemu zifuatazo: (Mdo 9:17; 13:3; 19:6 28:8).Katika Sakramenti hiyo Kuhani hutumia mikono yake kuwapaka Krisma wale anaowapa Kipaimara.
Kitubio na Upatanisho
 Padri hutumia pia mikono yake kwa kutakasa wakati wa kuadhimisha Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Mkristo anapokuja kwenye chumba cha kuadhimisha Sakramenti hiyo, Kuhani hutumia mikono kumbariki. Tendo la kumbariki ni tendo la kumwombea neema za Mungu na kumwombea aweze kuungama vema akiongozwa na Roho Mtakatifu.
Akishaungama dhambi zake, Kuhani humpa ushauri na malipizi kisha humpa maondoleo ya dhambi zake. Tendo la kuondoa dhambi hulifanya kwa kumwekea mikono kichwani na kusali sala maalum ya kumwombea  Roho Mtakatifu amtakase, yaani amwondolee dhambi zake. Mara nyingi Makuhani hutumia mkono mmoja wa kuume  kumnyoshea Mkristo anayeungama na kusali sala ya maondoleo. Kwa asili lakini anatakiwa kunyosha mikono yote miwili mazingira yanaporuhusu.
Sakramenti ya Mpako Mtakatifu
Katika Sakramenti ya Mpako Mtakatifu au Mpako wa Wagonjwa Padri hutumia tena mikono yake kutakasa na kuwaombea wagonjwa. Tendo la kunyosha mikono na kuwaombea wagonjwa   lina msingi pia kutoka Maandiko Matakatifu.
“Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani, akamwekea mikono akisema: ‘Ndugu Sauli, Bwana Yesu, amenituma, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu’. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa” (Mdo 9:17-18). Nafasi nyingine ya kuwaombea wagonjwa kwa tendo la kunyosha mikono  ni ile Mtume Paulo alipomponya baba ya mkuu wa kisiwa cha Melita. “Ikawa  babake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza. Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa” (Mdo 28:8-9).
Tendo la Padri kunyosha mikono kwa mgonjwa ni muhimu. Hiyo ni ishara ya kumwomba Roho Mtakatifu ili amponye mgonjwa. Kabla ya Mtaguso wa pili wa Vatikano Sakramenti  ya Mpako wa Wagonjwa  iliitwa Mpako wa mwisho, na ilikuwa ikitolewa kwa wagonjwa mahututi, waliopoteza fahamu, na wasiokuwa na tumaini la kuishi tena. Jina hilo bado linakumbukwa na waamini wengi, na baadhi ya wagonjwa huogopa kupokea Sakramenti hiyo kwa kudhani kuwa wakipokea watakufa.
Kumbe kwa sasa siyo vile. Kila mwenye ugonjwa mzito anatakiwa kupokea Sakramenti hiyo ya Mpako wa Wagonjwa. Tena wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wanatakiwa pia kupokea Sakramenti hiyo kabla ya kufanyiwa upasuaji ili kuwaombea tendo la upasuaji lifanyike vizuri na wagonjwa  waweze kupona. Mafuta ya Wagonjwa yanapobarikiwa, Askofu huwaombea wagonjwa wanapopakwa mafuta hayo wapate kupona; yaani Sala ya kubariki mafuta  inaomba afya njema kwa wale wote watakaopakwa mafuta hayo.
Padri anapotoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa  husali sala ifuatayo: “Kwa mpako huu mtakatifu na kwa upendo na huruma yake kuu, Bwana akusaidie kwa neema ya Roho Mtakatifu, na yeye mwenyewe anayekuokoa katika dhambi, na kwa wema wake akupe nafuu na akujalie afya”. Katika sala hiyo ya kutoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa hakuna wazo lolote la kumwombea mgonjwa afe. Mawazo makubwa  ni  mawili: kumwombea mgonjwa asamehewe dhambi zake na wazo la pili mgonjwa aweze kupata nafuu katika maumivu yake, na  kadiri ya mapenzi ya Mungu aweze kuwa na afya. Marekebisho ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatikano kuhusu Sakramenti hiyo yanapaswa kuelezwa kwa Wakristo, ili wasiogope kupokea Sakramenti hiyo.
Wakristo waitikie - Amina
Kuhani anapotoa Sakramenti hizo mbalimbali ambazo zinamtakasa Mkristo, Mkristo mwenyewe na wale wanaoshiriki Liturujia hiyo inawapasa kuitikia viitikio vinavyotakiwa. Mara nyingi Wakristo huwa wavivu kuitikia hata kiitikio kidogo lakini ni  muhimu: Amina.  Amina ni kiitikio cha kukubalia kwa dhati kwamba alichosali Kuhani ni ukweli kabisa, nakubali kwa dhati.  Kwa kuitikia Amina, Mkristo huifanya ile sala kuwa yake. Mkristo asiyeitikia Amina, je, hakubaliani na ile Sala?  Je, hapendi kuo

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI