Papa Francisko: Iweni watakatifu, wenye huruma na wakamilifu!
Iweni watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo Mtakatifu! Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya VII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia safari inayowapeleka kwenye ukamilifu kwa kusamehe na kusahau pasi na kulipiza kisasi kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, jicho kwa jicho; jino kwa jino! Tabia ya kulipiza kisasi inamwondoa mwamini katika njia ya utakatifu wa maisha. Kwa wale wanaowatendea ubaya na jeuri, wanapaswa kuwaombea, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kujikita katika msamaha, ili kusahau yale ambayo mtu ametendewa kwa ubaya. Ubaya unashindwa kwa wema na dhambi inashindwa kwa nguvu ya ukarimu, changamoto endelevu katika maisha ya Wakristo!
Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 19 Februari 2017 alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Maria Josefa wa Moyo Mtakatifu wa Yosefu, Jimbo kuu la Roma. Vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia chanzo chake kikuu ni chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipizana kisasi, hali ambayo inajitokeza katika viwango tofauti tofauti vya maisha ya binadamu. Wakristo wanaalikwa kuwa ni watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu na mkamilifu; kwani wema wa Mungu hauna ubaguzi, anawanyeeshea mvua wema na wabaya na kwamba, huruma yake haina mipaka!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha, unaowawezesha waamini kuwa mbali na kishawishi cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, inayohatarisha mafungamano ya kijamii, kifamilia na kimataifa. Vita daima inapata chimbuko lake katika moyo wa mtu, changamoto hapa na kujenga na kukuza utamaduni wa kusamehe na kuwaombea adui na watesi wao kama anavyokaza Yesu mwenyewe katika Injili ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kushirikishwa huruma, msamaha na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa wote. Huu ni mwaliko pia kwa waamini kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma; watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu na wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu!
Waamini wanaojitahidi kuwa watakatifu, wenyehuruma na wakamilifu, wanastahili kutangazwa kuwa ni watakatifu, mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajenge utamaduni wa kuwaombea wale wasiowatakia mema katika maisha pamoja na maadui zao; waamini wajitahidi kuwa wema kwa watu wote, jambo ambalo si rahisi sana, kwani linahitaji neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani ni muhimu sana ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika familia, jamii na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Sala anasema Baba Mtakatifu ina nguvu ya kushinda ubaya, ni chombo cha amani na chachu ya utakatifu na ukamilifu wa maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia neema ya kusamehe na kusahau; neema ya kuwaombea watesi na adui zao ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu; neema ya kudumu katika amani na maridhiano na wote, tayari kuambata njia inayokwenda kwenye ukamilifu na utakatifu wa maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment