Kwa nini wakatoliki huingia kanisani na viatu, na kukaa kwenye viti?
SWALI.
Kwa nini sisi Wakatoliki tunaingia kanisani na viatu? Amri ya Mungu ilitoka
katika Kut 3:5 mahali tusomavyo ifuatavyo, “Mwenyezi Mungu akamwambia,
‘Usije karibu! Vua viatu vyako kwa
sababu mahali hapa unaposimama ni mahali patakatifu’”. Swali hili nimeulizwa
kwa ujumbe wa simu.
Jibu: Musa alipewa amri ya
kinidhamu tu. Musa aliagizwa kufanya vile kimwili kuashiria jambo la kiroho.
Baada ya kusoma vyema Biblia, Wakristo tumegundua kwamba Mungu ni roho na
anapaswa kuabudiwa rohoni.
Imeandikwa katika Yn 4:21-24
hivi, “Yesu akamwambia, ‘Niamini wakati
unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi
Wasamaria mnawambudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu
kwa maana wokuvu unatoka kwa Wayahudi.
Lakini wakati waja, tena
umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na
ukweli. Maana Baba awataka watu wanaomwabudu namna hiyo. Mungu ni roho na watu
wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.’”
Kwa neno hili la Mungu (Yesu
Kristo), Wakristo tumeelewa vyema kwamba makubasi anayokataa Mungu na
tunayopaswa kuyavua kabla ya kumjongea Mungu ni dhambi na siyo viatu na
makubasi haya yanayoonekana. Siyo buti hizi au ndala na yeboyebo hizi za miguuni. Kinyume chake ni
dhambi zilizo rohoni mwetu ambamo tunakutana na
Mungu Mtakatifu.
Tunamwabudu Mungu rohoni, basi
humo ndimo mnamopaswa kuwa safi kabla ya kumjongea Mungu mtakatifu. Namna ya
kuvua viatu na makubasi ya kiroho ni kujongea kwa muungamishi na kuungama
dhambi. Ni kukikabili kiti cha Kitubio.
Ndipo tunahimizana kufanya toba
(kuungama) kabla ya kujongea sakramenti, kama vile, Kipaimara, Ekaristi
Takatifu, Ndoa na Daraja. Kwa jumla tunahimizana kuacha dhambi, ndiyo kuvua
makubasi, kabla ya kumkaribia Mungu. Kifupi, ni suala la kuachana na makubasi
ya rohoni, yaani dhambi na siyo viatu au makubasi haya ya miguuni.
Swali 2. Kwa nini tunakaa
kwenye viti na siyo kwenye majamvi kama kipindi cha Yesu walivyokuwa wakikaa
hekaluni? Swali hili nimeulizwa vile vile kwa ujumbe wa simu.
Jibu: Awali ya yote si kweli
kwamba wakati wa Yesu watu walikuwa wakikaa kwenye majamvi. Huku ni kulazimisha
mambo ya siku hizi yasomeke kwenye Biblia. Yesu aliishi katika karne ya kwanza
B.K.na wakati ule hekaluni na hata kwenye masinagogi hakukuwa kunatumika
majamvi kwa ajili ya kukaa waamini. Aidha, hamkuwa na benchi za kukaa. Watu
walikuwa wanasali wangali wamesimama.
Lakini hata kama majamvi
yangelikuwepo wakati ule, Wakristo hawapo kusudi waige kila kitu cha Wayahudi
ijapokuwa Kristo alikuwa Myahudi na alianzia kule kuhubiri. Ukristo ni dini
mpya na tofauti na dini ya Kiyahudi. Kama dini mpya ina haki ya kuwa na desturi
zake wala si lazima “kukopi” mambo na desturi zote za Wayahudi.
Majamvi ya leo tusiyapeleke
kwenye karne ya kwanza B.K. sembuse kabla yake. Wakati ule haya mambo
tuliyoyazoea sasa hayakuwapo kama
yalivyo leo. Natoa mifano. Mfano, hakukuwa na karatasi walitumia ngozi za mbuzi
au kondoo. Walitumia pia magombo ya
matete yaliyopondwa na kugandishwa kwa aina ya gundi.
Mikeka, mazulia na majamvi
yalikuwa nadra mno labda kwa matajiri wakubwa sana. Shida hii ilitokana na
viwango vya chini vya sanaa za kufuma na kusuka. Hakukuwa na viwanda. Nguo
zilikuwa za kufuma kwa kutumia sufu na manyoya ya mbuzi. Tena ilikuwaa kazi ya
mama kufuma kwa mikono. Mama mvivu alimaanisha watu wa familia yake kutokuwa na
nguo (rej. Mit 31:10-31).
Majamvi hayakuwako. Magodoro
hayakuwako. Vitanda vya mbao na kadhalika havikuwako. Ukisikia godoro au
kitanda cha mtu, ilikuwa na joho lake. Majoho ndiyo yaliyotumika kwa wakati
mmoja kama mkeka na blanketi. Majoho yalikuwa makubwa. Mtu alipolala alitumia
sehemu fulani kutandika chini na upande mwingine kujikunjia kama blanketi.
Ndiyo maana hata Yesu alipokuwa
anaingia Yerusalemu walifaulu kumtandikia nguo zao tu na wala siyo mikeka na
mazulia (rej. Mk 11:8). Hivi hekaluni sawa na kwenye masinagogi hakukuwa na
mikeka yoyote.
Pili, hekaluni na kwenye
masinagogi waamini hawakuwa wanakaa. Hekaluni na kwenye masinagogi waamini
walikuwa wanasimama. Hivi, kwa ujumla, kusema kulikuwa na majamvi na kwamba
watu walikuwa wakikaa ni kuongopa.
Walikokuwa wanakaa walikuwa
viongozi wawili (mkuu wa ibada au kwenye sinagogi – mkuu wa sinagogi na
msaidizi wake hazzan). Wengine wote walikuwa wanasimama. Ndiyo maana kwenda
kusali kulikuwa kunajulikana pia kama “kwenda kusimama mbele ya Bwana (rejea
Zab 24:3, 130:3, 134:1 na 135:2). Hivi hakukuwa hata na haja ya kuwa na mikeka.
Nina mashaka. Swali linaonekana
kutokea kwenye mazingira ya Waislamu wanaotaka kuonesha kwamba mikeka
wanayotumia misikitini inaendana na mambo yaliyokuwa yanatumiwa hekaluni au
kwenye sinagoni enzi za Yesu.
“Ulazimishaji” huu wa mambo si sawa.
Kukaa kama kukaa kulikuwa nje
ya nyumba za ibada, hususan majumbani mwa watu. Hata kwenye karamu kubwa kubwa
watu hawakukaa isipokuwa waliegemeana (kama
kulaliana vile). Mfano wake ni namna walivyoegemeana kwenye karamu ya
mwisho.
Kumbe, tangu Ukristo ulipoanza,
namna ya kukaa kwenye mikutano ilikuwa huru kwa Wakristo. Ilitegemea tu mila na
desturi za watu waliofikiwa na Ukristo. Wapo waliokuwa wakikaa kama Wayahudi
kwenye “fomu” na kuegemeana. Wapo waliokuwa wakisimama tu na kadhalika.
Matumizi ya benchi yametokea Ulaya. Ulaya walipopokea Ukristo na kujenga makanisa,
waamini waliingiza namna zao na desturi zao za kukaa kanisani, kwani ilikuwa
huru.
Upigaji magoti uliingizwa
baadaye na Mtakatifu Francis wa Assisi baada ya kupata wazo la kupiga magoti
kutoka katika safari yake ya Misri. Kule aliwaona watu wakipiga magoti, ndipo
akapenda Wakristo wafanye hivyo hivyo mbele ya Ekaristi Takatifu. Hivi ni
Wakristo Wazungu walioingiza viti vya kuhamishika (katika basilica) na
visivyohamishika ndiyo benchi za kukalia na kupigia magoti.
Lakini, pamoja na hayo yote, Wakristo
wanajua bado kwamba mkao wa kanisani ni huru. Haikatazwi, wenye mikeka na
mazulia wanaweza kutumia. Wenye vigoda wanaweza kutumia na kadhalika.
Katika yote, tukumbuke bado
kwamba Wakristo hawapo kusudi waige kila kitu cha Wayahudi ijapokuwa Kristo alikuwa
Myahudi na alianzia kule kuhubiri. Ukristo ni dini tofauti na dini ya Kiyahudi.
Wakristo tunatakiwa kumwabudu Mungu na kusali, kwa namna zipi na tungali
tumekaa vipi, bado ni huru. Tunaagizwa
tutumie akili tu (rej. Mt 22:34-40).
Comments
Post a Comment