Askofu Chengula: Wafarijini wagonjwa
WAAMINI Wakatoliki wametakiwa
kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wote, kuwafariji na kutambua uwepo wa Kristo
ndani ya wagonjwa hao wanaowahudumia.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya, Mhashamu Evarist
Chengula wakati akitoa Homilia katika Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya
Wagonjwa iliyofanyika katika Kanisa la Roho Mtakatifu, Parokia ya Ruanda, Jimbo
Katoliki Mbeya.
Katika ibada hiyo, Askofu Chengula amesema watu wote wanatakiwa
kuwatunza wagonjwa huku wakiamini wanambeba Kristo, maana kutofanya hivyo
kunasababisha wagonjwa kujiona wamekataliwa na ulimwengu huku wakikata tamaa na
kuhusisha magonjwa na imani za kishirikina, jambo linalosababisha chuki na
uongo kwa binadamu.
Amesema wagonjwa ni kielelezo cha
upendo wa Kristo kushirikishwa katika mateso ya Yesu, hivyo
wanapaswa wajiweke mikononi mwa Mama Bikira Maria maana kwa mateso wayapatayo ni ukombozi kwao kwakuwa Yesu Kristo ni Mganga.
“Kutembelea Wagonjwa ni njia mojawapo ya kuwarejesha kutoka katika
mawazo ya kuwekwa pembezoni mwa jamii, na baadhi ya wagonjwa wengine wanapona
kabisa kutokana na imani zao, huku wakijiona sawa sawa na wasio wagonjwa
kutokana na faraja kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki.” Amesema Askofu
Chengula.
Ikumbukwe kuwa kila mwaka tarehe 11 Februari Kanisa Katoliki huadhimisha
kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa
Lurdi, ambapo siku hiyo pia iliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili
(ii) kuwa mahususi kwa ajili ya kuwaombea wagonjwa, kwani wagonjwa wengi
wanaoenda Hija Lurdi wanapata uponyaji.
Comments
Post a Comment