Jimbo Kuu Tabora lafungua jubilei miaka 100 ya upadri
ASKOFU
Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora amezindua Jubilei ya Miaka 100
ya Upadri ngazi ya Jimbo na kuwasihi waamini kuwaombea mapadri ili watekeleze majukumu yao
kwa hekima na unyenyekevu.
Ufunguzi wa Jubilei hiyo umefanyika hivi
karibuni katika Kanisa Kuu la jimbo hilo huku Askofu Mkuu Ruzoka akisisitiza
kuwa, upadri si kazi nyepesi na ni maisha yanayohitaji sala na imani thabiti
kwa Mungu. Hivyo ni vyema mapadri wakazidi kuomba kuongezewa imani ili wadumu
katika maisha hayo ya kumtumikia Mungu na kuinjilisha kama walivyofanya
wamisionari wa Kwanza.
“Maisha ya Upadri si lelemama! zipo changamoto
mbalimbali ambazo mapadri wanakutana nazo. Changamoto hizo mtaendelea kukutana
nazo lakini jambo la msingi ni kuzikabidhi kwa Kristo aliye asili ya wito wenu
ili apambane nazo. Hizo ndizo dhoruba walizokutana nazo wafuasi wa Kristo
wakiwa safarini na Kristo mwenyewe akazituliza .
Hivyo ninawasihi mapadri kumuomba Mungu daima awajalie fadhila ya
Hekima kama ile ya Sulemani. Hekima iliyomsaidia kuliongoza Taifa Teule la
Israel. Mkumbuke kuwa pale Taifa la Israeli lilipomsahau Mungu na kufanya yao,
lilisambaratika, kadhalika padri naye asipomtegemea Mungu katika utume wake
hawezi kufanikiwa hata mara moja,” amesema Askofu Mkuu Ruzoka.
Aidha amewakumbusha wazazi wajibu wao wa
kuwalea vema watoto wao na kuwaandaa ili wapende maisha ya upadri na utawa. Kamwe
wazazi wasiwazuie watoto wao kuingia maisha ya miito mitakatifu kwa ajili ya
kumtumikia Mungu na Taifa lake.
Wito pia ulitolewa kwa waamini wote
kutunza Imani iliyokwisha pandwa katika mioyo yao na Kristo mwenyewe kwa njia
ya Sakramenti za Kanisa kupitia mapadri.
Amesisitiza; “Kumpata padri mmoja ni
zaidi ya kuongoa watu elfu Kumi, hii yote ni kusema kuwa, padri kwa nafasi yake ndiye
muadhimishaji wa matakatifu ya Mungu kwa ajili
ya kuwapeleka watu wengi kwa Kristo kwa njia ya Masakrameni na
mafundisho yake.
Hivyo mapadri wanapaswa kutunza zawadi
hiyo waliyopewa na Mungu, kwani palipo na padri kuna Ekalisti Takatifu, na penye
Ekaristi Takatifu pana padri.”
Katika Adhimisho hilo pia waamini wote
wamealikwa kuwaombea Mapadri wa Kwanza katika Jimbo hilo Kuu la Tabora ambao
sasa ni marehemu, yaani Pd. Raphael Kavula, Pd. Simon Makulumo, na Pd. Philipo
Luziga wote waliopadirishwa Agosti mwaka 1928 na Mjumbe wa Baba Mtakatifu Arthur
Hinsley.
Jubilei hizi pacha yaani ya miaka 150 ya
Uinjilishaji na miaka 100 ya Upadri Tanzania Bara zilizinduliwa kitaifa Oktoba
Mosi mwaka 2016 katika Jimbo Katoliki Bukoba na Majimbo yanaendelea kuzindua Jibilei
hizo katika ngazi ya majimbo.
Comments
Post a Comment