Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria kwa njia ya mahubiri na kifo chake


Mwinjili Mathayo katika maadhimisho ya Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa anaendelea kutoa muhtasari wa Heri za Mlimani, ambamo Kristo Yesu anataka kuwasaidia wasikilizaji wake, ili kuweza kufahamu kwa undani Sheria ya Musa, iliyofungwa kwa Agano la Kale na kupata utimilifu wake kwenye Agano Jipya, kwa njia ya Kristo Yesu. Hapa alifanikiwa kuifafanua Sheria katika mzizi, umuhimu na lengo lake kwa watu wa Mungu.

Yesu alifanya ufafanuzi huu kwa njia ya mahubiri yake, lakini zaidi, kwa kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani, ili kutimiza mapenzi ya Mungu na kutenda haki iliyokuwa inazidi ile haki ya Mafarisayo. Hii ni haki inayofumbatwa katika upendo na huruma kiasi hata cha kupenya katika undani wa Amri za Mungu na hivyo kuepuka uwezekano wa kuitekeleza Sheria kwa kufuata mkumbo au kuchagua yale mambo yanayompendeza mtu! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Februari 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa namna ya pekee anasema, Baba Mtakatifu, Yesu aliamua kufafanua Amri tatu: yaani Usiue, Usizini na wala Usiape kwa jina la Mungu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu anapozungumzia kuhusu Amri ya “kutoua” kimwili kwa kumwondolea mtu uhai wake anaendelea zaidi kugusa hata mauaji yanayoweza kupelekea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa njia ya maneno na mawazo. Haya ni matendo ambayo yanaweza kumpelekea mtu kufanya mauaji. Yesu anawaalika wafuasi wake kutokuweka ngazi ya dhambi,bali kutambua kwamba, dhambi zote hizi zina madhara katika maisha ya mwanadamu. Yesu anapowataka wafuasi wake kutokushutumu, kwa wengi jambo hili linaweza kuonekana kama salam ya asubuhi, kwani shutuma na matusi ni mambo yanayopelekea kwenye kifo, yanagusa undani wa mtu, kumbe kuna haja ya kuondokana na tabia hii inayohatarisha maisha ya watu!
Kristo Yesu alitumia fursa ile kufafanua na hatimaye, kuipatia Amri ya kutozini utimilifu wake, kwani inagusa undani na heshima ya watu wa ndoa. Mtu anaweza kufikia hatua hii kwa njia ya mawazo machafu, matusi na hata kuzini nafsini mwake, kwa kutamani mwanamke asiyekuwa mke wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuzini ni sawa na wizi, rushwa na dhambi nyingine zote ambazo kimsingi zinatendwa katika mawazo na moyoni mwa mtu kwa kuwa na maamuzi potofu na baadaye, mawazo haya yanamwilishwa katika matendo. Yesu anaonya kwamba, mtu anayemwangalia mwanamke kwa tamaa, tayari amekwisha kuzini naye moyoni mwake, tayari ameanza kusafisha njia ya kuzini naye kimwili.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu mawazo yanayojitokeza katika mwelekeo huu! Yesu anawataka wanafunzi wake kuwa waaminifu kwa viapo vyao na kamwe wasiape kwa Jina la Mungu, kwani hizi ni dalili za kutokuwa na usalama na kielelezo cha maisha ya ndumilakuwili katika mahusiano ya binadamu. Watu wanapenda kutumia mamlaka ya Mungu ili kuwa na uhakika wa mambo ya kibinadamu. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kujenga na kudumisha mazingira ya kifamilia na katika jamii hali ya ukweli na kuaminiana, ili kushuhudia ukweli pasi ya kukimbilia mamlaka ya Mungu ili kuweza kuaminiwa. Hali ya kutoaminiana na kudhaniana vibaya ni mambo yanayohatarisha daima amani na utulivu kati ya watu!
Mwishoni, mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria, Mwanamke msikivu, mpole, mwaminifu na mtii mwenye furaha, ili aweze kuwasaidia kukaribia zaidi na zaidi Injili ili kuwa Wakristo wa kweli na wala si “Wakristo wa kuchongwa”. Jambo hili linawezekana kwa njia ya neema ya Roho Mtakatifu, anayewawezesha waamini kutenda yote kwa upendo, ili kutimiza mapenzi ya Mungu! Msiue, msizini wala msiape kwa uwongo! Ni mambo makuu matatu ambayo Yesu ameyakazia katika Injili ya Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI