Wazazi wana wajibu wa kuchochea miito
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Tanga Mhashamu Anthony Banzi amewahimiza
wazazi na wana jumuiya kuichochea miito ya vijana wao ya kuwa watawa na mapadri
ili isiishie njiani na kutimiza kusudi ambalo Mungu ameweka ndani yao.
Amesema hayo katika
ibada ya kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa shemasi Gitaga Okindo wa shirika
la Mapendo ambayo imefanyika jimboni Tanga na kuhudhuriwa na watu
mbalimbali akiwemo mkuu wa shirika.
Askofu Banzi amesema
kuwa, wazazi wana jukumu la kuhakikisha vijana hawaishii njiani katika kutimiza
wito wao wa kumtumikia Mungu, wawasaidie ili kusudi la Mungu litimie kwa kuwa
tayari ameweka kitu ndani yao.
“Wazazi mpo karibu
na vijana wetu hivyo mkiona mwelekeo wa
mtoto ni kuifanya kazi ya Mungu usimwache akaishia njiani, mtieni moyo na
kumsisitiza kufanya yanayompendeza Mungu ikiwemo kumpeleka seminari ndogo ili
atimize kusudi la kumtumikia Mungu,” amesema Askofu Banzi.
Amesisitiza kuwa,
kuwatoa vijana siyo kuwapoteza, ikiwa kijana ana hiyo karama basi apewe ushirikiano
na miongozo kwani hapotezwi ila anawekewa hazina Mbinguni kwa kuwa Mungu anamuhitaji
ili aifanye kazi yake.
“Mtoto ni zawadi
toka kwa Mungu, hivyo anapoihitaji zawadi aliyokupa ifanye kazi yake usiizuie
kwa kutoa sababu ambazo hazina mashiko machoni pa Mungu, mpe Mungu cha kwake
haupotezi ila unajiwekea hazina mbinguni na matunda yake utayaona,” amesema
Askofu Banzi.
Amesema umeshuhudiwa
upungufu wa mapadri katika Kanisa lakini wazazi na jamii wakishirikiana kumtia
moyo kijana kutimiza wito ambao Mungu ameweka ndani yake, kutakuwa na mapadri
wa kutosha.
“Uzalishaji wa
mapadri hauridhishi, siyo kama hawapo wenye huo wito, wapo ila baadhi ya wazazi
wanawakwamisha vijana wao hivyo wazazi na jumuiya kwa msisitizo mkubwa,
tusiwakatishe tamaa badala yake tuwe nao bega bega ikiwemo kuwapeleka seminari
ndogo ili watimize wito wao, kwa kufanya hivyo hatupotezi ila tunawekeza kwa
Mungu,” amesema Akofu Banzi.
Comments
Post a Comment