‘Kanisa siyo mshindani, ni mtumishi’ Ask. Ngalalekumtwa
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu
Tarcisius Ngalalekumtwa amesema kuwa Kanisa halina wazo lolote la ushindani
katika utoaji wa huduma zake, bali linafanya hayo yote kwa kuwa huo ni utume na
wito wake.
Ameeleza hayo katika
maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii
nchini (CSSC), yaliyofanyika jijini Dar es salaam, na kubainisha kuwa Kanisa
linatumia rasilimali zake kwa ajili ya ustawi wa taifa na watu wake.
“Kanisa siyo mfanya
biashara, na siyo mshindani ila ni mtumishi. Kanisa linaendelea kutoa huduma
bora ikiwemo elimu bora na siyo bora elimu, afya na kuwatunza wenye dhiki.
Hatuna nia ya kuingia ushindani, tunatumia rasilimali zetu kwa ajili ya taifa
letu ili liwe lenye heshima, utu na ustawi” ameeleza Askofu Ngalalekumtwa
ambaye pia ni Makamu wa Rais wa CSSC.
Kauli hiyo imeungwa
mkono na Rais wa CSSC Askofu Alex Malasusa aliyeweka wazi kwamba makanisa
hayatoi huduma za afya na elimu kwa ajili ya kupata faida kiuchumi.
Amesema kuwa makanisa
yanajikita katika utoaji wa huduma hizo ikiwa ni sehemu ya wito wake na kwamba
hakuna dhamira yoyote ya kujitafutia utajiri kupitia huduma hizo.
Kwa upande wake Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Frederick Shoo
amesema kuwa CSSC itaendelea kutoa
huduma za jamii na kamwe hawaruhusiwi kuacha wito huo kwani ni sehemu ya utume
wao.
Aidha ameongeza kuwa
wanahitaji roho ya ushirikiano, roho ya kujitoa kama waliyokuwa nayo waasisi w
tume hiyo katika kuwahudumia wanadamu.
“Tunajivunia miaka 25 ya
utoaji huduma za jamii, licha ya kukutana na changamoto kadhaa, tunajua
changamoto hizo ni fursa kwetu. Tutaendelea kuweka utambulisho katika utoaji wa
huduma kama wafuasi wa kristo: yaani upendo, huruma na uadilifu” ameeleza.
Comments
Post a Comment