Kardinali atahadharisha chuki za kidini
θ Asema Kanisa Katoliki halistawi kwa ruzuku za serikali
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo ameonya dhidi ya uzushi wa baadhi ya watu kuwa ruzuku
toka serikalini ndizo kichocheo cha maendeleo ya Kanisa hilo.
Akizungumza na gazeti
Kiongozi Kardinali Pengo amesema kuwa,
hizo ni chokochoko za wasiolitakia mema Kanisa na kwamba zisipokemewa kwa dhati
zinaweza kusababisha chuki za kidini jambo ambalo ni hatari katika jamii.
“Mimi sina kubwa la kusema ila ninawaambia
watu hawa kuwa, wachunguze kwanza kabla ya kusema, hakuna ukweli wowote juu ya
Kanisa Katoliki eti linasaidiwa na Serikali na haya ndiyo yanayoleta chokochoko
na chuki za kidini baadaye,” amesema Kardinali Pengo.
Ameongeza kuwa, kuna
vitu vingi ambavyo vinazungumzwa mtaani juu ya Kanisa Katoliki na kuanza
kuamsha chuki, baina ya wale wenye uelewa mdogo kuwa Kanisa Katoliki linapewa
fedha na Serikali kitu ambacho si kweli.
Kardinali Pengo
ameendelea kusema kuwa Kanisa Katoliki lina vyanzo vyake vingi vya kupata fedha
ikiwemo sadaka za waamini, ambazo ndizo zimekuwa chachu ya kuendelea kwake na
kuwa kila nchi hapa duniani Kanisa limekuwa likijiendesha lenyewe pasipo
kutegemeana.
“Kanisa lina miradi
chungu nzima zikiwemo shule na hospitali, ambazo zimekuwa
zikiingiza fedha na kulisaidia Kanisa kukua na kujitegemea pasipo kutegemea
chochote, wanaodai kuwa tunapewa ruzuku na Serikali si wakweli wachunguze, sio
kukaa na kuzungumza vitu vya uongo”amesema Kardinali Pengo.
Ameendelea kusema kuwa
Kanisa Katoliki halijawahi kupata fedha wala kwenda kuomba msaada serikalini
ili kuendesha shughuli zake za uinjilishaji ila watu wasiokuwa na mapenzi mema
na Kanisa hilo wamezusha taarifa hizo hewa ndiyo chanzo cha kusambaa kwa chuki
ambapo baadhi ya watu wa madhehebu mengine wataamini kitu ambacho si cha kweli.
Aidha Kardinali Pengo
amewataka waamini wa kanisa hilo kuendelea kusali na kuwaombea kwa Mungu watu
wanaozusha taarifa za uongo ili wawe na
ufahamu wa mambo wajue na kulitambua kanisa katoliki na kuwa wajinze jinsi
kanisa hilo linavyojiendesha ili nao wapeleke neema hiyo katika madhehebu yao
waweze kuendelea kama kanisa katoliki lilivyoendelea.
Mbali na hilo Kardinali
Pengo ametumia fursa hiyo kuendelea kuwatia moyo watu kuvumilia hali ngumu ya
maisha yaliyopo sasa kwa kuwa ugumu huo wa maisha ndiyo njia ya kufikia
mafanikio.
Amewataka kuacha
kulalamikia kitendo cha rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli
kununua ndege na kuanza kwa mchakato wake wa kujenga uwanja wa ndege wa
kimataifa huko Chato Mkoani Geita kwa kuwa nalo ni jambo jema.
Amesema ili kufikia
mafanikio ni lazima kupitia magumu kwa kuwa kila safari ina changamoto zake na
kwa changamoto hizo ni lazima wananchi wafunge mikanda ili kuimaliza amewataka
kumuombea rais Magufuli ili kumaliza changamoto hizo na si kumlaumu.
Comments
Post a Comment