Kanisa kujenga mwelekeo mpya wa vijana duniani
Kanisa
Katoliki linatarajia kufanya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, ambayo
itatoa mwelekeo mpya wa vijana wa kizazi kipya, kutafakari na kufanyia kazi
changamoto zinazowakabili vijana ulimwenguni.
Akiongea na Kiongozi ofisini
kwake, Mratibu wa Vijana Taifa katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC), Padri Liberatus Kadio ameeleza kuwa sinodi hiyo itakuwa ni fursa kwa
maaskofu kujadili hali ya vijana ulimwenguni kwa kuangazia maisha yao kimaadili
na kiroho.
Aidha Padri Kadio ametaja
baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana kuwa ni pamoja na hali ya
kutojaliana, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, ubaguzi, ukosefu wa
ajira, ukimbizi na uhamiaji na uharibifu wa mazingira.
“Kwa kutambua kuwa dunia
inabadilika kwa kasi mno, Maaskofu watakutana kuweka mikakati na sera za
kichungaji ili kujenga kizazi kipya chenye mwelekeo mpya. Hivyo watatathmini
mambo yanayoathiri ujenzi wa kizazi kipya, kwa kutambua kuwa vijana ni wadau
wakuu katika mchakato wa mageuzi ya kijamii hivyo hawatakiwi kukosa dira
sahihi” amebainisha Padri Kadio.
Ameongeza kuwa sinodi hiyo
inalenga kuwasaidia vijana ili wapate utimilifu wa maisha wakitambua kuwa
maisha na imani ni zawadi ya Mungu. Amegusia mambo makuu yatakayopewa
kipaumbele katika mjadala huo ambayo pia yamebeba kaulimbiu kuwa ni imani na
mang’amuzi ya wito, na kuwataka vijana kutambua, kutafsiri na kuchagua kile
ambacho Mungu anakitaka katika maisha ya kijana.
“Imani iwasaidie vijana kujenga
na kudumisha umoja katika kuishi maisha ya kiroho na kiutu. Lazima vijana wawe
na maamuzi sahihi na wasome alama za nyakati na kutambua uwepo wa Roho
Mtakatifu katika historia. Aidha katika mang’amuzi ya wito vijana wawe tayari
kupokea utume kwa uchaji, ari na moyo mkuu. Wawe tayari kuchukua msalaba na
kuubeba vema wakimfuata Kristo” ameeleza.
Sinodi ya Maaskofu kwa vijana
itafanyika Oktoba 2018 na kuongozwa na mada isemayo “Vijana, imani na
mang’amuzi ya wito”.
Comments
Post a Comment