Wanachuo msitumie dawa za kulevya-Ask. Mkude


ASKOFU wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude ametoa wito kwa vijana hususani waliopo vyuoni kutojihusisha na dawa za kulevya, kwani kufanya hivyo ni kusitisha ndoto na mafanikio waliyojiwekea maishani.
Askofu Mkude ametoa wito huo alipokuwa akihubiri katika ibada ya Misa Takatifu iliyoambatana na uzinduzi na kubariki eneo la kufanyia ibada kwa wanafunzi  wa Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine (SUA) Jumuiya ya Mtakatifu Don Bosco New Hostel iliyopo nje kidogo ya Chuo hicho katika  Parokia ya Maria Konsolata SUA.
Katika mahubiri yake Askofu Mkude amekazia umuhimu wa wanachuo kuzitafakari kwa kina athari zitokanazo na dawa za kulevya kwa afya zao, hivyo watambue kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wakiwa wema ili kumtumikia siku zote za maisha yao.
“Mwenyezi Mungu amewaumba vizuri ili mumtumikie yeye siku zote za maisha yenu ya hapa duniani hivyo ili kuliepuka hili janga la dawa za kulevya mnatakiwa mtafakari kwa kina athari zitokanazo na matumizi na uuzaji wake,” amesema Askofu Mkude.
Hata hivyo amesema kuwa wapo baadhi ya watu wameshawishika kujiingiza kwenye biashara hiyo haramu ili wapate utajiri wa haraka bila kujali na kuangalia kuwa watumiaji ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu.
“Baadhi ya watu wameshawishika na kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya kwa kutamani utajiri wa haraka na kusahau katika mzunguko  alioutengeza wa uuzaji inawezamfikia ndugu yake au motto nae akawa ni mmoja wa wanunuzi na mtumiaji, hapo ndipo utakagundua nguvu kazi ya Taifa inavyoteketea hasa vijana.”

Askofu Mkude amewaasa pia waamini kujiepusha na misingi ya vishawishi vinavyoweza kuwasabisha kuingia upotevuni bali wanapaswa kutambua thamani yao mbele ya Mwenyezi Mungu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI