“Msiogope gharama kuwapa watoto elimu bora” Askofu Amani
Askofu wa jimbo Katoliki
Moshi Mhashamu Isaac Amani ametoa wito
kwa waamini na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawapeleka watoto shule na wasiogope
gharama katika kwa sababu elimu bora ina
gharama.
Askofu
Amani ambaye pia ni msimamizi wa kiti cha Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu ametoa
wito huo alipokuwa akizindua rasmi shule ya sekondari ya wasichana ya
Michaud ambayo ni ya
bweni iliyopo Karatu Jimboni Mbulu na kuitaka jamii isiogope gharama
katika kuwasomesha watoto kwa faida ya taifa.
Akihubiri
katika misa ya uzinduzi wa sekondari hiyo inayomilikiwa na Masista wa Shirika
la Mabinti wa Maria amesema elimu bora
ina gharama na kuwataka waumini na jamii kwa ujumla kuwekeza kwenye elimu kwa
kuwasomesha watoto wao.
Askofu
Amani amesema ili dunia na taifa liende mbele lazima uwekezaji ufanyike kwenye elimu ambayo ni ufunguo wa dunia na
mwanga wa ulimwengu na kuitaka jamii na waumini kuhakikisha wanawasomesha
watoto ili wawe wataalamu na viongozi wazuri wa
taifa hapo baadaye.
“Elimu
hutenda miujiza kwa mtu aliyesoma lazima tusomeshe watoto wetu na
kuwaandaa kuja kuwa wataalamu mbalimbali na viongozi wa kesho katika kulitumikia kanisa na taifa letu hapo
baadaye,” amesema
Askofu
Amani amesema elimu humwandaa mtoto kuwa mzalendo kwa taifa hivyo lazima
uwekezaji kwenye suala hilo lenye tija
kubwa ambalo pia huwaandaa wahudumu
wazuri wa kiroho, mapadri, watawa na walei ndani ya Kanisa.
Amesema
mtu akiwa msomi humfanya kutambua thamani ya watu na utu wa
wengine kwa kuishi nao kwa furaha,
upatano, msamaha na wenye kumtumainia Mungu na kuwataka waumini wasiogope
kuwapeleka shule watoto kwa faida ya maisha yao ya baadaye katika dunia hii ya
sayansi na teknolojia.
Amewaasa
pia wanafunzi wajitahidi kusoma sana
masomo ya sayansi na waachane na hofu na woga
kuhusu kulisoma somo hilo kwa faida ya taifa ili liweze kupata wataalamu katika kada
mbalimbali za kuwatumikia watu kiroho na kimwili.
Akisoma
risala Sista Catherine Kabula amesema shule hiyo yenye usajili namba S .4970
imeanza rasmi mwaka 2016 na inafundisha masomo ya sayansi, sanaa, TEHAMA na
kuitaka jamii kuchangamkia fursa hiyo
kwa kuwapeleka watoto hapo ili wapate elimu bora.
Naye
Mama mkuu wa shirika la Mabinti wa Maria, Sista Theresia Sungi amesema kwa
kufahamu umuhimu wa elimu katika dunia hii
wameamua kuweka kipaumbele kwenye suala hilo lengo likiwa kuisaidia
jamii na kutoa wito kwa wazazi na walezi
kuwapeleka watoto wao katika shule za Kanisa ambazo zimekuwa zikitoa
elimu bora na malezi mema ya kiroho na kimwili.
Mkuu wa
wilaya ya Karatu, Bi.Theresia Mhongo amelipongeza Kanisa Katoliki kuwa limekuwa likifanya kazi nzuri kwenye huduma za jamii katika sekta za afya, elimu, maji na
kuwashukuru Shirika la Masista wa Mabinti wa Maria kwa kuwekeza kwenye jambo la elimu kwa sababu wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ya uhaba wa
shule za sekondari miongoni mwa jamii.
Comments
Post a Comment