Upungufu wa chakula waathiri watumiaji wa ARV Bunda
IMEELEZWA kuwa hali ya upungufu wa chakula katika baadhi ya
maeneo nchini imeathiri upatikanaji wa chakula cha uhakika katika kaya, huku
wilayani Bunda hali hiyo ikipelekea watumiaji wa dawa za kupunguza makali ya
Virusi vya Ukimwi (ARV) kushindwa kutumia dawa hizo ipasavyo kutokana na
kutokuwa na uhakika wa chakula.
Hayo yamebainishwa hivi
karibuni na watumiaji hao walipotembelewa na timu inayoratibu vikundi vya
ujasiriamali vinavyosimamiwa na Ushirikiano wa Dini mbalimbali nchini (TIP),
kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo asilimia kubwa ya
vikundi hivyo vinaundwa na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Akielezea baadhi ya
changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza mradi huo, mmoja wa wajumbe wa
kikundi cha Tupendane kilichopo katika kijiji cha Kabasa wilayani Bunda, Bi
Esta Maduka amesema kuwa hali ya ukosefu wa mvua kwa muda mrefu katika eneo
hilo imepelekea upungufu wa chakula na hivyo kuathiri matumizi sahihi ya dawa
hizo za ARV.
“Kuna upungufu mkubwa wa
chakula katika kijiji chetu, bei ya mahindi inapanda kila siku na kwa sasa
tunanunua mahindi kwa bei ya Shilingi 4500 kwa sado moja. Hali hii inatuathiri
sisi tunaoishi na VVU kwani inaathiri ufuasi mzuri wa dawa” ameeleza.
Aidha wajumbe hao
wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kusaidiwa chakula hasa kwa wanaotumia
ARV ili waendelee kufuata dozi na kustawisha afya zao.
Katika hatua nyingine
wajumbe hao wameupongeza mradi wa TIP kupitia TEC ambao umewawezesha kumudu mahitaji
ya maisha yao ya kila siku, huku wengine wakiendesha biashara kutokana na
mikopo na akiba wanazojiwekea katika vikundi vyao.
Moja ya faida
zinazotajwa na wanakikundi hao kutokana na uwepo wa mradi huo ni pamoja na
kupata elimu sahihi inayowawezesha kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na
matumizi sahihi ya ARV, huku uwepo wao ukitwajwa kusaidia kupunguza unyanyapaa
kwa kiasi kikubwa.
“Kikundi kimetusaidia
kuwaibua wagonjwa wapya majumbani na kuwaandikia rufaa, kutoa elimu ya lishe
bora, kutoa ushauri na kuwatembelea wagonjwa majumbani pamoja na yatima. Pia
kikundi kimekuwa chachu ya kuendesha maisha yetu kwani kinatusaidia kupata
fedha za kukidhi mahitaji yetu ya kila siku” amesema Julius Manyama.
Naye mjumbe mwingine
Musa Mgetu ameweka wazi kuwa mradi huo umemuwezesha kuanzisha biashara ya kuuza
bidhaa mbalimbali mgodini, kuendesha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, na
kumpatia faida lukuki ikiwa ni pamoja na kumuwezesha kununua ng’ombe wawili.
Kwa upande wake Mratibu
wa mradi huo kutoka TEC, Norasco Tereba ameeleza kuwa nia ya mradi huo ni
kuwajengea wananchi uwezo na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali za
maisha, kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya ARV na umuhimu wa
kuzingatia lishe kwa watu wanaoishi na VVU.
“Lengo la mradi ni kuwawezesha
watu waliojiunga katika vikundi wapewe mbinu na mafunzo yatakayowasaidia
kuendesha maisha yao. Tunalenga kuwajengea uwezo kwa kuwapa ujuzi na elimu
ambayo watabaki nayo hata pale wafadhili watakapoondoka” amesema.
Comments
Post a Comment