Mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupambana na mifumo mipya ya utumwa mamboleo inayoendelea kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake.Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kuanzia Jumanne tarehe 7 hadi tarehe 8 Februari 2017 inaendesha mkutano maalum kuhusu mifumo mipya ya utumwa mamboleo.

Mabingwa, wafanyakazi, viongozi wa serikali, majaji, watafiti pamoja na waandishi wa habari wanashiriki katika mkutano huu, ili kupembua kwa kina na mapana changamoto hii inayoendelea kuenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia. Kwa muda wa miaka thelathini, Shirika la Afya Duniani limekuwa likipambana na biashara haramu ya binadamu, lakini bila mafanikio yanayokusudiwa kwani kila kukicha biashara hii inazidi kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu unafanyika kulingana na makundi ya mahali wanapotoka wajumbe, yaani kutoka Amerika, Afrika na Bara la Ulaya, kwani kila sehemu ina changamoto zake.
Taasisi ya Kisayansi ya Kipapa inakaza kusema, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake inakwenda kinyume cha kanuni msingi za haki za binadamu, usawa, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii ni mifumo mipya ya utumwa mamboleo inayowatumbukiza wafanyakazi katika baa la umaskini; kwa kuwanyanyasa na kuwadhulumu wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu ambao wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo kana kwamba, si watu wenye heshima na utu wao. Takwimu zinaonesha kwamba, upandikizaji wa viungo vya binadamu kwa mwaka 2014 ulikuwa ni kiasi cha milioni moja, sawa na asilimia 10% ya mahitaji halisi ya viungo vya binadamu. Hitaji kubwa ni figo ambazo ni sawa na asilimia 75% ya biashara haramu ya viungo vya binadamu! Mahitaji haya yanafuatiwa na: ini, moyo, mapafu na bandama.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI