Ujumbe wa Papa Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima 2017

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini wanaolala mlangoni pa matajiri si kero inayopaswa kushughulikiwa kama “chuma chakavu” bali ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kubadili mfumo wa maisha tayari kuwakumbatia na kuwasaidia wengine katika shida na mahangaiko yao. Changamoto kubwa wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni kujitahidi kumwilisha sehemu ya Injili la Lazaro maskini na tajiri asiyejali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zake. “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2017, muda wa kusali, kutafakari, kujikita katika maisha ya Kisakramenti, lakini zaidi kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu anasema, Kipindi cha Kwaresima ni mwanzo mpya na njia inayowaelekeza waamini katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, kielelezo cha ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti, muda wa toba na wongofu wa ndani, ili kujenga na kuimarisha urafiki na Mwenyezi na Kristo Yesu ambaye daima anaendelea kuwa ni rafiki mwaminifu! Hata pale ambapo mwamini anatenda dhambi na kukengeuka, lakini Kristo Yesu anaendelea kubaki kuwa ni mwaminifu, anawasubiri waja wake ili waweze kutubu na kumrudia tena, ili kuwaonjesha huruma yake isiyokuwa na kifani!
Kwaresima ni kipindi kilichokubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili kuweza kuboresha maisha ya kiroho kwa kutumia nyenzo takatifu zilizowekwa na Mama Kanisa yaani: Kufunga, Kusali na Kutoa sadaka, lakini zaidi ni kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini katika Kipindi cha Kwaresima kutafakari kuhusu mfano wa Mtu tajiri na Lazaro maskini, (Rej. Lk. 16: 19-31). Huu ni ufunguo wa kufikiri na kutenda ili hatimaye, kuweza kupata furaha ya kweli sanjari na maisha ya uzima wa milele kwa kujikita katika toba na wongofu wa kweli!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwinjili Luka anamchambua kwa kina na mapana Lazaro maskini, aliyekuwa anawekwa mlangono, akiwa na vidonda vingi naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyokuwa yanaanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakavilamba vidonda vyake. Hii ni picha ya tajiri na maskini aliyedharauliwa na kunyenyekeshwa kwa nguvu! Maskini huyu alikuwa anaitwa Lazaro, maana yake “Mungu anatusaidia”.
Kumbe, hapa kuna mtu mwenye historia, utu na heshima yake! Maskini mbele ya yule tajiri alionekana kuwa si mali kitu! Lakini kwa waamini ni mtu anayepaswa kufahamika, kwani ana sura, ni zawadi na utajiri mkubwa unaopaswa kukumbatiwa; kupendwa kwa kukumbuka kwamba, hata Mwenyezi Mungu katika ukamilifu wake, daima amekuwa akiwekwa pembezoni mwa maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Lazaro maskini anawakumbusha waamini kwamba, jirani yako ni zawadi, changamoto ya kujenga uhusiano mwema kwa kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya binadamu. Lazaro maskini mlangoni pa tajiri si kero inayopaswa kushughulikiwa kama ”chuma chakavu” bali ni mwaliko wa kutubu na kubadili mtindo wa maisha sanjari na kufungua mlango wa moyo kwa ajili ya jirani kwani kila mtu ni zawadi, anaweza kuwa ni jirani wa karibu au mtu wasiyemfahamu.
Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka uliokubalika kwa waamini kufungua malango ya nyoyo zao kwa maskini ili kutambua Uso wa Kristo Yesu, tayari kukutana naye katika hija ya maisha ya kiroho. Kila mtu wanayekutana naye ni zawadi inayopaswa kupokelewa, kuheshimiwa, kupendwa. Neno la Mungu liwasaidie waamini kupokea na kupenda zawadi ya maisha, hususan pale mtu anapokuwa dhaifu na maskini. Ili kumwilisha changamoto hii, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha ya yule mtu tajiri. Kimsingi dhambi inawafumba macho waamini kiasi cha kutoweza kuona mahitaji msingi ya jirani zao.
Tajiri hatambulikani kwa jina, bali kwa mavazi yake, kwani alipenda kuvaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi na kula siku zote kwa anasa! Mavazi ya rangi ya dhambarau yalikuwa yametengwa kwa ajili ya miungu na yalikuwa na thamani kubwa sana kuliko hata dhahabu na fedha na kwamba, kitani kilikuwa ni alama ya utakatifu na alipenda mno anasa kiasi hata cha kujisahau. Kumbe, huyu kwa hakika alikuwa ni tajiri wa kupindukia kama inavyojionesha hata katika simulizi la Injili! Ni tajiri aliyepekechuliwa kwa dhambi, hali inayojionesha katika mambo makuu matatu: uchu wa fedha na mali; anasa; kiburi na majivuno.
Paulo Mtume anakaza kwa kusema shina la ubaya ni kupenda mno fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi (Rej. I Tim 6: 10). Fedha inaweza kufikia hatua ya kumtawala mwanadamu badala ya kuwa ni chombo cha huduma ili kutenda mema na kujenga mshikamano na wengine; fedha ikitumika barabara inaweza kuwa ni kuwasaidia waamini na walimwengu katika ujumla wao, jambo la msingi ni kuondokana na ubinafsi kwa kutoa nafasi kwa upendo na amani kung’ara. Mfano wa mtu tajiri na Lazaro maskini unaonesha jinsi ambavyo kiburi kilimgeuza kuwa ni mtu anayependa mno anasa na kwa kujionesha, hali inayodhihirisha utupu wa maisha ya ndani. Maisha yake ni gereza la mambo ya nje. Kiburi ni ngazi ya chini kabisa ya maisha ya kimaadili, anajionesha kama Mfalme, mungu mdogo na kusahau kuwa, ni kiumbe dhaifu anayesubiriwa na kaburi. Ni mtu ambaye fadhila ya upendo imechakachuliwa kwa kiasi kikubwa kiasi hatacha kushindwa kuwaangalia wengine kwani amezama katika ubinafsi wake. Tabia ya kumezwa mno na mali pamoja na fedha ni upofu na kushindwa kumwona Lazaro maskini aliyekuwa na njaa, akalazwa mbele ya mlango wake na kunyanyaswa. Injili ina laani kwa nguvu zote uchu wa fedha na mali kwani kamwe mwanadamu hawezi kumtumikia Mungu na mali.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 anakazia sana umuhimu wa Neno la Mungu na hasa mfano wa tajiri na Lazaro maskini, uwasaidie waamini kujiandaa barabara kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Liturujia ya Kupakwa majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, waamini watapakwa majibu na kukumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena. Maskini na matajiri wote watakufa tu na wala hawatachukua jambo lolote kutoka hapa duniani.
Majadiliano ya kina kati ya tajiri na Mzee Abramu, Baba wa imani yanaonesha kwamba, hata tajiri alikuwa ni sehemu ya watu wa Mungu, lakini hata siku moja hakuonesha uhusiano wake na Mungu, bali alijiona kuwa ni mungu mdogo. Katika shida na mahangaiko makubwa anamtambua Lazaro maskini na kuomba msaada kutoka kwake, lakini akasahau kwamba, hata yeye aliwajibika kumhudumia Lazaro maskini, lakini hakufanya vile, ndiyo maana kwa sasa anakiona cha mtema kuni! Hapa mwaliko kwa waamini ni kutenda mema; kusikiliza ushauri unaotolewa na Neno la Mungu. Kwa bahati mbaya, tajiri hakusikiliza hata kidogo Neno la Mungu, kiasi hata cha kushindwa kumpenda Mungu na jirani yake. Neno la Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu, lina nguvu kiasi cha kuweza kuamsha tena toba na wongofu wa ndani; kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake wa Kipindi cha Kwaresima kwa kuwakumbusha waamini kupyaisha maisha yao ya kiroho ili kuweza kukutana na Kristo Yesu aliye hai katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa na kwa njia ya jirani. Yesu ambaye alikaa Jangwani kwa muda wa siku 40, aliweza kumshinda Shetani, anawaonesha waamini njia ya kufuata. Roho Mtakatifu awaongoze waamini waweze kufanya kweli toba na wongofu wa ndani; watakaswe na dhambi zinazowafanya kuwa vipofu wa kumhudumia Kristo na maskini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa upyaisho wa maisha yao ya kiroho kwa kushiriki kikamilifu katika Kampeni za Kipindi cha Kwaresima sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama familia moja ya binadamu. Ushindi wa Kristo Mfufuka uwasaidie kufungua malango kwa wanyonge na maskini, ili kuishi na kushuhudia utimilifu wa furaha ya Pasaka!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI