“Simamieni ukweli” Askofu Kimaryo awaasa mapadri
MAPADRI wametakiwa kuwa wakweli katika kila jambo watendalo
ili kuwakomboa wanyonge na wahitaji kutoka katika hali mbaya kimaisha na
kiroho.
Askofu wa Jimbo Katoliki
Same Mhashamu Rogarth Kimaryo ametoa rai hiyo katika Misa Takatifu ya uzinduzi
wa Jubilei ya miaka 100 ya upadri Tanzania Bara katika Jimbo hilo.
“Mapadri lazima muuige
mfano wa Nabii Yeremia aliyeitwa na Mwenyezi Mungu na kupewa majukumu
yaliyomfanya akabiliane na wafalme, wakuu, makuhani na watu wa mamlaka akitetea
ukweli hata kutaka kukatwa kichwa, lakini alisimamia alichotumwa na Mwenyezi
Mungu na kukitimiza,” amesema Askofu Kimaryo
Amesema mapadri
wametumwa na Mungu ili kuutumikia wito kwa kuwatetea wanyonge na kujitenga na
faida na tamaa za kidunia ambazo zitawaingiza katika matatizo makubwa, hivyo
wanatakiwa kuyaishi mafunzo ya Kanisa tu.
“Hapa duniani mmeteuliwa
kuwasaidia wahitaji tu kiroho, siyo kuzitumia elimu zenu kubwa na talanta
kujitajirisha, hayo mngeyapata kirahisi nje ya wito wa kipadri, mkiyazingatia
haya mtaungana nami pamoja na viongozi wa Kanisa Katoliki kujihakikishia faida
pekee tutakayoikuta mbinguni,”
Akiirejea hati ya Baba
Mtakatifu Fransisko juu ya mazingira “LAUDATO SI”, amewataka mapadri kukaa
pamoja na jamii na kusaidia kuyalinda mazingira kwa kupanda miti mingi na kuhifadhi
uoto wa asili kwani mazingira ni uhai.
“Serikali inafanya
jitihada kubwa kuhamasisha uhifadhi mazingira, tunatakiwa kuiunga mkono
kuhifadhi mazingira kwa kuotesha miti mingi, kuhifadhi vizuri mazingira
yanayotuzunguka, kukaa pamoja na kujadili mbinu mbadala ya kuzuia uchomaji
mikaa, ukataji miti na kutoishia kutoa matamko tu kwa wanaoharibu mazingira”.
Pia Askofu Kimaryo
ameitaka jamii kuisoma na kuizingatia hati ya Baba Mtakatifu juu ya Ndoa
“AMORIS LAETITIA” kwani ina mchango mkubwa katika kuzilinda familia.
“Ndoa imara na tamu
inapimwa katika maeneo mbalimbali ya kimsingi ambayo ni upendo wa kweli,
msamaha na uvumilivu, endapo mtazingatia haya kama yalivyoainishwa katika hati
ya Baba Mtakatifu ndoa zenu zitadumu milele,” amesisitiza
Akiongelea miaka 100 ya
upadri katika Jimbo la Same ambapo padri wa kwanza mzalendo alipata daraja hilo
mwaka 1937, Askofu Kimaryo amesema kazi haikuwa rahisi mtu mweusi kupewa daraja
hilo kutokana na sababu nyingi za kipindi hicho hasa ikizngatiwa kuwa nchi
ilikuwa haijapata uhuru.
Amewapongeza Maaskofu
watangulizi katika Jimbo hilo, mapadri, watawa walio hai na waliotangulia mbele
ya haki kutokana na jitihada zao ambazo zimesababisha Jimbo kukua.
Hata hivyo ameitaka
jamii kuwaombea Maaskofu, mapadri, watawa na viongozi wengine wa kidini kwani
wao si wakamilifu ili waeneze injili kwa watu wengi zaidi.
Mapadri wazalendo wanne
wa kwanza jimboni Same ni pamoja na Padri Andrea Kivaria, Padri Leonard
Kiure(1951), Padri Phocas Abedi(1961) na Padri Sabbas Msuya(1961)
Comments
Post a Comment