Papa Francisko aomba msamaha kutokana na nyanyaso za kijinsia!
Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imelichafua Kanisa, kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho; ukweli unaopaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma ya Mungu, ili kuanza upya! Nina Msamehe, Baba! Ni kitabu kilichoandikwa na Daniel Pittet na utangulizi wake kuandikwa na Baba Mtkatifu Francisko anayempongeza Daniel Pittet kwa ushuhuda wake makini, licha ya kunyanyaswa kijinsia wakati alipokuwa mtoto mdogo, lakini amekuwa na ujasiri wa ajabu wa kuweza kusimulia nyanyaso hizi.
Baba Mtakatifu anasema, alibahatika kukutana na kuzungumza na Daniel Pittet kunako mwaka 2015 mjini Vatican wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Akamshirikisha kuhusu nia yake ya kuandika kitabu kuhusu upendo; kitabu ambacho kingekuwa ni mkusanyiko wa shuhuda za watawa na wakleri walionyanyaswa kijinsia katika maisha yao. Baba Mtakatifu anasema, aliguswa kwa namna ya pekee na ushuhuda uliotolewa na Daniel Pittet, kwani hata baada ya miaka mingi ya mateso na mahangaiko ya ndani, ameendelea kuonesha moyo wa subira, ili kuona haki inayofumbatwa katika huruma inatendeka.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, watu wengi wataweza kukisoma kitabu hiki na kuona jinsi ambavyo dhambi na ubaya vinaweza kujipenyeza kwa mtumishi wa Mungu ndani ya Kanisa! Inasikitisha kuona Padre au mtawa akitenda mambo haya ambayo kinyume kabisa cha dhamana na utume wake, ambao kimsingi, ungekuwa ni daraja ya kuwapeleka watoto kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya anakuwa ni kikwazo, kiasi cha kuwapelekea baadhi ya watu kukatisha maisha yao baada ya kuzidiwa na uchungu!
Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Kanisa, anapenda kuomba msamaha kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na kashfa hii ndani ya Kanisa; anatumia fursa hii ili kuwaombea upendo, kwani dhambi hii ni kubwa sana inayokwenda kinyume kabisa cha Mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. “Bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yafaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari” Mt. 18:6. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linapaswa kuwa ni Mama mpendelevu anayewahudumia na kuwatunza watoto wadogo, maskini na wasioweza kujilinda wenyewe. Kanisa halitakuwa na huruma kwa Wakleri wanaosaliti maisha na utume wao; kwa Maaskofu mahalia au Makardinali wanaotaka kuwalinda na kuwatetea kama ilivyowahi kutokea katika historia na maisha ya Kanisa.
Katika mateso na mahangaiko ya ndani, Daniel Pittet amebarikiwa kukutana na Uso mwingine wa Kanisa, uliomwezesha kuwa na imani tena kwa watumishi wa Mungu na Kanisa. Anasimulia nguvu ya sala iliyomsindikiza na kumfariji katika kipindi hiki cha giza nene la maisha ya kiroho. Akaamua kukutana na mtesi wake miaka 44 baadaye, ili kuweza kumwangalia usoni, kwani alikuwa ametenda mabaya yaliyogusa undani wa maisha yake! Yule mtoto aliyenyanyaswa kijinsia, leo hii ni mtu mzima, dhaifu, lakini walau anaweza kupiga moyo konde na kusonga mbele. Ni watu wengi ambao wanashindwa kutambua kwamba, hakumchukia, bali alimsamehe na huu ukawa ni msingi wa njia ya msamaha wa kweli.
Huyu ni kijana ambaye ameonesha ujasiri kwa kuvunjilia mbali kuta za ukimya zilizokuwa zinafisha kashfa na mahangaiko ya watu ndani ya Kanisa, ili kuonesha mwanga katika giza la maisha ya Kanisa. Huu ni ukurasa mpya unaopania kulisafisha Kanisa pamoja wahusika kusutwa na dhamiri nyofu ili kuwajibika kwa vitendo vyao dhidi ya watoto wadogo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anasali kwa ajili ya kumwombea Daniel pamoja na wale wote walionyanyaswa katika utoto wao, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwainua tena, kuwagusa na kuwaponya; pamoja na kuwakirimia waamini wote huruma na msamaha wake usiokuwa na kifani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment