Siku ya Wagonjwa Duniani: Huduma ya tiba ni haki msingi kwa kila mtu!
Maadhimisho ya Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Mshangao kwa makuu aliyotenda Mungu: “Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu”. Lk. 1:49. Maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa kuanzia tarehe 10 - 13 Februari 2017. Haya yamesemwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ambaye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, Katibu mkuu mwakilishi aliyekuwa ameambatana na Professa Antonio Gioacchino Spagnolo kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha “Sacro Cuore” kilichoko mjini Roma, walioshiriki kikamilifu katika kuandaa “Mwongozo Mpya wa Wafanyakazi katika Sekta ya Afya”. Mwongozo huu umezinduliwa rasmi, Jumanne, tarehe 6 Februari 2016 mbele ya jopo la waandishi wa habari mjini Vatican.
Kardinali Turkson anasema, huduma ya afya ni haki msingi kwa wote pasi na ubaguzi. Mwongozo unabainisha mambo msingi ya huduma kwa afya ya binadamu na changamoto za kimaadili zinazojitokeza katika sekta ya afya, ili ziweze kuvaliwa njuga mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo na Mafundisho ya Kanisa. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye kilele cha Jubilei ya miaka 25 ya Siku ya Wagonjwa Duniani huko Lourdes, Ufaransa; mahali ambapo Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kwa mara ya kwanza alimtokea Mtakatifu Bernadetha Soubirous.
Hii ni mara ya tatu kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani inaadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1993 na mara ya pili mwaka 2004 wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jubilei ya miaka 150 tangu Kanisa lilipotangaza kwamba Bikira Maria kukingiwa Dhambi ya asili ni sehemu ya mafundisho tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani anapenda kutoa changamoto kwa familia ya Mungu kutafakari kwa kina na mapana juu ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuzama zaidi katika afya ya binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hapa kuna haja ya kuwa mwelekeo makini kuhusu masuala ya kimaadili katika sekta ya afya kwa kuzingatia kanuni maadili katika masuala ya kibaiolojia; kwa kuwaenzi wanyonge na kudumisha mazingira bora zaidi.
Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi ambayo yamevaliwa njuga na Mama Kanisa katika kipindi cha Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Wagonjwa Duniani. Utekelezaji huu ulifuatiwa kwa kuchapishwa kwa Kitabu cha Mwongozo wa taalimungu maadili, uliotafsiriwa katika lugha 19; mwongozo ambao umetumiwa na wafanyakazi katika sekta ya afya kwa miaka 25. “Mwongozo Mpya wa Wafanyakazi katika Sekta ya Afya” na matunda ya juhudi, maarifa na weledi ulioneshwa na kushuhudiwa na Hayati Askofu mkuu Zymunt Zimowski aliyesimamamia na kuratibu kazi hii kwa unyenyekevu mkubwa. Huu ni urithi ambao Hayati Askofu mkuu Zimowski ameliacha Kanisa katika sekta ya afya kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na mwongozo huu, hivi punde utaweza kutafsiriwa katika lugha mbali mbali
Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu anasema,“Mwongozo Mpya wa Wafanyakazi katika Sekta ya Afya” unajaribu kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tema mbali mbali ambazo zimekuwa zikijadiliwa katika sekta ya afya kwa kukazia tena kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu, kwani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wafanyakazi katika sekta ya afya ni wahudumu wa Injili ya uhai, changamoto ni kupenda kuyakumbatia na kuyaenzi maisha hadi pale mwanadamu anapoitupa mkono dunia.
Professa Antonio Gioacchino Spagnolo katika hotuba yake amefafanua mambo mapya yaliyoibuliwa na Mwongozo huu kama sehemu ya mwendelezo wa wito na huduma ya Kanisa kwa wagonjwa. Anakumbusha kwamba, Kanisa ni mhudumu wa faraja na kielelezo cha Uso wa huruma ya Mungu, changamoto kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, faraja na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Ili kuwawezesha wafanyakazi katika sekta ya afya kuwa kweli ni wahudumu wa maisha ya mwanadamu wanapaswa kunolewa mara kwa mara, ili kweli waweze kutekeleza dhamana yao katika tiba pamoja na kuendelea kuwa ni wahudumu wa zawadi ya maisha; kwa kukuzana kudumisha mahusiano kati yao na wagonjwa pamoja na kuwajengea wagonjwa imani katika huduma wanaywapatia.
Mwongozo huu unahimiza pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kusimamia kanuni maadili na utu wema katika ujumla wake; wakati wa maisha na pale mgonjwa anapopambana na mauti. Kuna tafakari za kimaadili na kichungaji zinazotolewa kwa wafanyakazi katika sekta ya afya! Katika sehemu ya maisha; mwongozo huu unakazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki ya maisha; umuhimu wa chanjo na tiba kwa wagonjwa. Kila mtu ana haki ya kupata huduma ya dawa na kufaidika na maendeleo ya teknolojia ya vifaa tiba, ingawa hadi sasa kuna baadhi ya wagonjwa wanashindwa kupata tiba kutokana na dhana “dawa yatima” ambazo hazina mvuto kwa wawekezaji, lengo ni kuwa na haki katika sekta ya afya kwa kuendeleza utafiti na tiba kwa magonjwa! Hapa kuna haja ya kuzingatia maadili ya huduma ya tiba kwa wagonjwa.
Mwongozo unawataka wahudumu wa afya kuonesha weledi, uwajibikaji, maadili na utu wema, kwa wagonjwa walioko kufani. Utashi halali wa wagonjwa unapaswa kuzingatiwa kwa kuheshimu itifaki na dhamiri hao ya mhudumu wa afya. Kanisa linapinga dhana ya kifolaini au ‘Eutanasia”. Kwa namna ya pekee, Kanisa linawaalika wafanyakazi katika sekta ya afya kuheshimu dakika za mwisho za mgonjwa anayekaribia kuaga dunia, ili kweli aweze kupewa haki yake kwa kuaga dunia katika hali ya amani na utulivu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment