Maagizo ya Hati ya Liturujia kwa wanakwaya na watunzi
TUNAENDELEA
kuangazia changamoto mbalimbali zinazoshambulia Muziki Mtakatifu na hata kuleta
ukakasi kwa waamini na watu wenye mapenzi mema. Mfululizo huu wa makala ya
muziki mtakatifu unalenga kutoa mwanga kwa watunzi, wanakwaya, waamini na
wakleri, ili kwa pamoja tuelewe mipaka ya utume wa uimbaji na hivyo kutunza
hadhi ya muziki huo ulio tunu bora.
Na moja ya miongozo inayotoa
mwelekeo sahihi wa utume huu wa uimbaji ni ile Hati ya Liturujia (Sacrosanctum
Concilium), ambayo ni maelekezo yaliyotolewa na mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili
wa Vatikani. Basi tuendelee kujishibisha kwa maagizo hayo, yatujenge na
yatukomaze katika utume wetu.
Baada ya kupitia vipengele
kadhaa vya hati ya liturujia, yafuatayo ni maagizo yanayotolewa na hati hiyo
kwa wanakwaya na watunzi, ambayo iwapo tutayazingatia tutaepuka ukakasi na
malalamiko yanayotolewa na waamini kwetu watunzi na wanakwaya.
Uwepo wa
Kristo katika Liturujia
Tunaambiwa kuwa katika adhimisho la
Misa Takatifu, Yesu mwenyewe yupo na anajumuika na kundi la waamini. Hivyo kwa
kutambua kwamba katika adhimisho hilo tunaungana na Kristo mwenyewe, ni wazi
kuwa tunapaswa kufanya yote kwa uchaji mkubwa, unyenyekevu na unyamavu mtakatifu.
Kwa hivyo hata namna ya kuimba, au
aina ya nyimbo tunazoziimba katika misa ni lazima zidhihirishe heshima, uchaji,
unyamavu na kilele cha sala kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hati ya liturujia
inasema:
“7.
Kusudi kutimiza tendo kubwa namna hii, Kristo yupo daima katika Kanisa lake,
kwa jinsi ya pekee katika maadhimisho ya kiliturujia. Yupo kwenye Sadaka ya
Misa katika nafsi ya kasisi, ‘Yeye ambaye, akijitoa mara moja msalabani,
anajitoa tena mwenyewe kwa huduma ya mapadre’
Kwa
hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na
la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo
jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kilekile na kwa daraja
ileile”.
Tujitathmini sasa, tunaimba kwa
uchaji au tunapiga kelele na kufanya fujo? Je kwa kuimba kwetu, kweli
tunaungana na Kristo katika liturujia?
Muziki
mtakatifu ni shirikishi: lazima waamini washiriki kikamilifu
Kama nilivyowahi
kueleza hapo awali, kazi ya wanakwaya siyo kuimba. Kazi ya waimbaji wa muziki
mtakatifu ni kuwasaidia waamini wasali vizuri ili Mungu atukuzwe na mwanadamu
atakatifuzwe. Ili hayo yatimie, ni lazima waamini washiriki kikamilifu katika
matendo yote ya liturujia ikiwa ni pamoja na kuimba na kuitikia zaburi na
viitikizano.
Lakini hali iko tofauti katika
makanisa mengi hapa nchini. Waamini wamefanywa mabubu na watazamaji tu, kwa
kuwa nyimbo zinazoimbwa katika misa hazifahamiki. Yaani kila dominika ni nyimbo
mpya, tena ngumu ambazo hazishikiki kirahisi. Hali hii haiwasaidii waamini
kusali vizuri na kufikia lengo la kuwepo kwa muziki mtakatifu. Katika hili,
hati ya liturujia inaagiza hivi:
“30.
Ili kuwawezesha waamini washiriki kimatendo, mashangilio ya waamini, maitikio,
kuimba zaburi, antifona, nyimbo, vitendo, ishara na mkao wa mwili vitiliwe
maanani. Unyamavu mtakatifu utumike pia, wakati unapodaiwa.
113.
Tendo la Liturujia hupata kuwa na heshima zaidi wakati linapoadhimishwa katika
sherehe kwa kuimba, wakiwepo makasisi na kwa ushirikiano hai wa waamini.
118.
Nyimbo za kidini za (wakristo) wenyeji zihimizwe kwa bidii, ili katika ibada
mbalimbali za watu na pia katika matendo ya Liturujia sauti za waamini ziweze
kusikika vizuri, kadiri ya utaratibu na madai ya miongozo”.
Muziki
ni sala: Tunga na imba huku ukisali
Moja ya mambo ambayo watunzi wa
mwanzo hapa nchini walifaulu basi ni kutunga wakiwa katika hali ya sala. Nyimbo
zao zilikuwa tafakari tosha inayomuingiza muumini katika hali ya sala. Ndiyo
maana hata ukisikia nyimbo kama Roho yangu (E. Nyundo), Bwana Yesu waniita
(Padri Mutajwaha), Nimtume nani (Padri Ntapambata) nk, unaonja yale yanayoimbwa
humo kuwa ni sehemu ya maisha yako ya ukristo.
Tungo za leo ni kizunguzungu.
Chaguzi za maneno hufanywa kwa hisia tu na siyo sala. Melodia zinazotumika
humpeleka mtu katika tamasha, sehemu za burudani au mitaani badala ya
kumfikisha mbele ya Ekaristi Takatifu.
Zaidi ya hapo, hapaswi kuishia
katika kuimba tu. Bali uimbaji umsaidie katika kumfikisha katika kilele cha
sala. Tunaagizwa na hati ya liturujia kufanya yafuatayo:
“121.
Watunga muziki, wakisukumwa na roho ya kikristo, wajione kuwa wameitwa
kuustawisha muziki mtakatifu na kukuza hazina yake.
Pia
watunge melodia zinazolingana na sifa za muziki mtakatifu na ambao unaweza
kuimbwa si tu na kwaya kubwa, bali pia na kwaya ndogo. Tena ziwasaidie waamini
wote kushiriki kikamilifu.
Maneno
yaliyomo katika nyimbo yalingane na mafundisho ya Kanisa katoliki, zaidi
yachukuliwe hasa katika Maandiko Matakatifu na vitabu vya liturujia”.
Muziki
unadai elimu ya teolojia: Jifunze
“115.
Jitihada kubwa ifanyike ili kuhamasisha elimu na mazoezi ya muziki katika
seminari, katika nyumba za unovisi za mashirika ya kiume na ya kike, katika
nyumba za wanafunzi, kama vile vyuo na shule za kikatoliki; ili kupata elimu
hii, walimu waandaliwe kwa bidii kubwa, kisha watumwe kufundisha muziki
mtakatifu. Ikiwa inafaa, uundaji wa Taasisi za Juu za muziki mtakatifu
uhimizwe.
Wanamuziki, wanakwaya, na juu ya
wote watoto, wapewe elimu halisi ya kiliturujia”
Biblia na
uimbaji
Hatuna haja ya kuvamia maneno ya mtaani au kuzidiwa na muziki wa
kidunia. Tunayo hazina kuu isiyokauka, ambayo kwayo tunapata maneno
yanayotutafakarisha vya kutosha. Watunzi na waimbaji, tumieni Biblia Takatifu.
Yako mengi ya kujifunza humo. Maneno ya mtaani tuwaachie wengine. Tunaagizwa
hivi:
“24.
Jambo muhimu kuliko yote katika adhimisho la Liturujia ni Maandiko Matakatifu,
maana katika hayo huchukuliwa masomo ya kusomwa na kufafanuliwa katika
mahubiri, na pia zaburi zinazoimbwa.
Sala,
maombi na nyimbo hupata uvuvio toka Maandiko, kama vile toka Maandiko matendo
na ishara hupata maana. Kwa hiyo, ili kufaulu kufanya marekebisho na maendeleo
na malinganisho ya Liturujia, ni lazima kuhimiza ule upendo mtamu na hai wa
Maandiko Matakatifu, ambao unashuhudiwa na mapokeo mastahiki ya Makanisa ya
Mashariki na ya Magharibi”.
Kwa
maoni 0657835343
Comments
Post a Comment