‘Makanisa yataiwezesha Tanzania ya viwanda’ Dkt. Kigwangala
KATIKA kuelekea uchumi wa
viwanda nchini makanisa yametajwa kuwa mdau muhimu katika kufanikisha adhma
hiyo, kwa jinsi yalivyoweka kipaumbele kwa utoaji huduma katika sekta za afya,
elimu, sayansi na teknolojia.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangala katika maadhimisho ya jubilei ya miaka
25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini (CSSC), yaliyofanyika jijini
Dar es salaam hivi karibuni na kuhudhuriwa na mamia ya wajumbe.
Dkt. Kigwangala ameeleza kuwa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii imekua
mdau muhimu katika kuratibu na kusimamia huduma za jamii hapa nchini, hususani
huduma za elimu na afya, na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa
uchumi nchini.
“Kama mnavyofahamu, nchi yetu iko kwenye mpango wa kuelekea kwenye
uchumi wa viwanda, lengo hili litafikiwa tu iwapo nchi yetu itakuwa na watu
wenye afya bora na elimu ya kutosha ambao wataweza kushiriki kikamilifu na
kutoa mchango wao katika kufanikisha adhma hii kwa kufanya kazi kwa bidii na
weledi” ameeleza.
Aidha Dkt. Kigwangala ameeleza kuwa nchi haiwezi kuendelea kama watu
wake wanasumbuliwa na maradhi, ujinga na umasikini, na hivyo kuipongeza CSSC
kwa kuwa mdau muhimu katika kupambana na maradhi, ujinga na umasikini.
Kwa upande wake Rais wa CSSC, Askofu Dkt. Alex Malasusa ameeleza kuwa
tume hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuleta amani kwa
watanzania wote, kwa kupeleka huduma muhimu kwa kila kiumbe bila kujali rangi,
kabila au dini.
“Kanisa kwa maana ya madhehebu yote yaliyo mwanachama wa CSSC
yataendelea kutoa huduma hii muhimu, huu ndiyo wito wetu. Tunapofanya kazi hizi
kwetu ni sehemu ya ibada, na kutokufanya ni kukiuka hali ya kutoa upendo wa
Mungu kwa wanaohitaji” ameeleza Askofu Malasusa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Peter Maduki ametaja mafanikio
yaliyofikiwa na tume hiyo kuwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa elimu, kupanua
na kuboresha utoaji huduma za afya huku ubia katika huduma za afya
unaimarishwa.
Mpaka sasa tume inazo taasisi za elimu zaidi ya 1000 zikijumuisha shule
na vituo vya kutolea elimu. Kwa upande wa afya tume ina vituo vya afya
vipatavyo 900, ikiwa ni pamoja na hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati
696.
Comments
Post a Comment