‘Hakuna maendeleo bila Kanisa’ Mwinyi asema
RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya
pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa Kanisa ni chombo muhimu katika
maendeleo ya jamii ya Tanzania, hasa kwa kuchangia katika kuweka mazingira
chanya ya upatikanaji wa elimu na afya.
Alhaji Mwinyi ameeleza
hayo katika maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za
Jamii nchini (CSSC), yaliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni, ambapo
amesema kuwa Kanisa daima liko mstari wambele katika katika kutoa huduma bora
za elimu na afya nchini.
“Mara zote huwa
nawaambia jamaa zangu kule Temeke, nendeni katika hospitali za Kanisa. Wale
wenzetu wanafanya ile kazi kama sehemu ya ibada yao. Nawaambia wazi wakienda
huko watapata dawa na upendo” amesema Mwinyi.
Ameongeza kuwa kutokana
na ushirikiano huo baina ya makanisa nchini katika utoaji wa huduma, watanzania
wengi wamepata huduma bora, na kuwaomba maaskofu waendelee kuithamini CSSC ili
iendelee kustawi.
Ameweka wazi kuwa jamii
ya watanzania inahitaji zaidi uwepo wa CSSC hivyo ametoa wito kwa viongozi wa
tume hiyo kuendelea kupanua na kuboresha huduma za jamii.
Comments
Post a Comment