Walionusurika kifo mgodini Geita waapa kumrudia Mungu
·
Watoa siri uchimbaji dhahabu, walivyozama na kuokolewa
· Waanza kushuhudia Habari Njema kwa wengine
“TUMEMUONA
Mungu kwa namna ya ajabu sana ambayo hailezeki kwa ufasaha. Ametutendea makuu
tukiwa shimoni kwa muda wa siku tano. Tuna deni kubwa kwake maana tusipomjua na
kumwelekea ni sawa na kujitenga naye” ni kauli ya mmoja watu 15 walionusurika
baada ya kuzama katika mgodi wa RZU.
Wahanga hao 15 walifukiwa na kifusi
na kukaa shimoni kwa muda siku 4 na kuokolewa siku ya tano wakiwa salama na
hivyo kuibua shangwe kwa wakazi wa eneo hilo waliokusanyika kushuhudia jitihada
za uokoaji huo, huku wahanga hao wakimtaja Mungu kama mwokozi wao.
Mmoja wa Wahanga hao Anicet Masanja
amesema kuwa yeye binafsi alikuwa mbali na masuala ya Mungu lakini katika tukio
hilo amekiri kuwa ameuona wema wa Mungu kwao na kuahidi kujiwekea mazingira ya
kuwa karibu na Mungu wa kuhakikisha anasali kila mara.
"Mimi nilikua mbali na masuala
ya Mungu lakini ukweli usiofichika ni kwamba mkono wa Mungu kwetu umeonekana
bila kificho. Kweli Mungu ni mwaminifu na ana huruma na watu wake japo tunamfanyia
maasi kila mara, mimi mwenyewe nikimo, lakini hakuangalia hayo na hivyo kutuokoa"
amesema.
Ameongeza kuwa "Tusipomrudia Mungu,
hasa mimi binafsi, tutakuwa wajinga wakubwa na kwa upande wangu natamani na
ninaomba Mungu anisaidie nienende katika mwenendo mwema kisha nimfuate katika
roho na kweli”.
Mhanga mwingine wa tukio hilo
Dickson moris (25) amesema kuwa mara kadhaa alikuwa akisikia watu hasa wahubiri
wakitaja miujiza ya Mungu, huku yeye akiwa mwenye kubeza kauli hizo lakini
akasema muujiza wa ajabu umetokea kwake na wenzake hao 15.
"Sina ubishi tena na Mungu juu
ya uwepo wake na matendo makuu anayotenda na aliyotutendea sisi viumbe wake, hata
tusiompenda na kumfuata. Tuna deni kubwa kwake. Iwapo tutaendelea kuwa na
kiburi katika kumfuata, sijui nini kitatupata maana ametutoa kuzimu tunapaswa
kumtukuza kwa matendo yetu mema" ameeleza.
Aidha wahanga wengine wa tukio hilo
wamekiri wazi kuwa hata shughuli zao za uchimbaji hazitakiwi kabisa kumtaja
Mungu na mara kadhaa wakiona kuna mtu miongoni mwao anamtaja Mungu, humchukulia
mtu huyo kuwa anawazibia rziki kwa kuwa wao wanaamini kuwa dhahabu na Mungu
haviendani.
Kutokana na tukio hilo wahanga hao
wamekiri kuwa dhana ya kutomhusisha Mungu katika uchimbaji wa madini ni dhana
potofu, huku wakihoji kuwa kama dhahabu na Mungu haviendani kwa nini Mungu
amewaokoa wakiwa wanatafuta dhahabu, tena kutoka sehemu ambayo kwa hali ya
kawaida asingeweza kuokoka hata mmoja.
Wakati huo huo watu mbalimbali
wamevipongeza vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama liiwemo jeshi la Polisi
mkoani Geita, jeshi la uokoaji la zimamoto, makampuni binafsi ya uchimbaji
madini yaliyotoa vifaa vyao vya kuokolea pamoja na wananchi wa kawaida
walijitoa muhanga kufanikisha uokoaji huo.
Hata hivyo wananchi hao
wamesikitishwa na wachimbaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza tena katika sekta
muhimu ya madini huku wakiwa na zana duni na hivyo nao kuonekana kama
wachimbaji wadongo wasio na zana za kisasa.
Comments
Post a Comment