Watoa huduma za Mahusiano ya Dini mbalimbali Mtwara watiwa hamasa





WATU wanaotoa huduma za kijamii kupitia mwamvuli wa Mahusiano ya Dini mbalimbali nchini, wametakiwa kujiona wenye thamani ya pekee kwa kile kilichoelezwa kuwa huduma yao hiyo ina mchango mkubwa katika kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara, Mhashamu Titus Mdoe wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya Haki za Binadamu yaliyowashirikisha viongozi wa dini na wasaidizi  Kisheria mkoani humo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Masista Mtwara.
Alisema kila anayefanya kazi chini ya mwamvuli wa dini mbalimbali hana budi kutambua kuwa anashiriki utume kwa njia ya pekee ili kuwezesha waja wa Mwenyezi Mungu kufurahia mema aliyowajalia muumbaji wao.
“Hata kule Adeni baada ya dhambi ya kula tunda ndio ulipoingia uhasama na hapo tunaona namna Adam alivyomtupia lawama ya dhambi mama yaani Eva na vile vile huyu mwanamama anamtupia lawama nyoka, hivyo huu unakuwa mwanzo wa  mfarakano hata kwa ndugu mfano mzuri ikiwa ni kwa Kaini na Aberi. Hata hivyo Mungu wetu anatudhihirishia kuwa hakutuumba kwa ajili ya mfarakano na ndio maana alimtuma mwanawe Yesu Kristo atukomboe,” amesema.
Askofu Mdoe amefafanua kuwa uwepo wa Kamati za Mahusiano ya Dini mbalimbali katika ngazi mbalimbali nchini zikiwemo ya Kitaifa, Kimkoa, Kiwilaya na hata ngazi ya Kata ni udhihirisho tosha wa kuviishi kwa matendo amani na upatanisho.
Ameongeza kuwa kupitia mahusiano haya ya dini mbalimbali wanajamii wameweza kuungana pamoja kufanya shughuli zao za kujiinua kiuchumi, kufuatilia rasilimali za umma na kuwa na ubavu wa kuhoji pale wanapoona miradi iliyotekelezwa haiendani na thamani ya fedha iliyotolewa pamoja na kupata fursa ya kupata elimu juu ya haki za binadamu.
“Tunayo sababu ya kufurahia kazi nzuri inayofanywa na wasaidizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali ikiwemo hapa Mtwara kwani wamewezesha wanajamii kuelewa juu ya haki za binadamu zikiwemo zile za wanawake, watoto na makundi mengine ya kijamii,” amesisitiza.
Ameongeza “ Jamani hakika Tanzania tunapendwa na Mwenyezi Mungu kwani watu wote bila kujali tofauti zao za kidini wanaweza kukaa pamoja na kuzungumza mambo yanayohusu ustawi wao…Tazama yaliyotokea kwa nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Somalia, Kongo na kwingineko…tujivunie upendeleo huu ambao zaidi unapambwa pia na upatikanaji wa fuvu la mwanadamu wa kwanza lililopatikana kwenye ardhi yetu ya Tanzania eneo la Olduvai Gorge,”.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mradi wa Uendelezaji wa Utu wa Mwanadamu inayofanya kazi chini ya Idara ya Haki, Amani na Uadilifu katika Uumbaji ya Kurugenzi ya Human Dignity ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) yalifadhiliwa na Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway (NCA) huku wawezeshaji wakuu wakiwa ni Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC) cha jijini Dar es Salaam.
Chini ya Mradi huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia Kamati ya Mahusiano na Dini mbalimbali mkoani Mtwara inatekeleza shughuli za kuwainua watu kiuchumi kupitia Benki za Kijamii Vijijini (IR-VICOBA), Ufuatiliaji wa fedha za umma zinazotolewa kwa ajili ya shughuli mbalimali za Maendeleo (PETS) pamojana  Msaada wa Kisheria ambapo kimeanzishwa kituo cha Wasaidizi wa Kisheria katika eneo la Ziwani mkoani humo.
Mbali na Mtwara wilaya nyingine ambazo TEC inatekeleza miradi kama hiyo kwa ufadhili wa NCA ni Mbozi, Ludewa, Njombe, Temeke, Kasulu, Karatu na Babati.

 Na Dalphina Rubyema, Mtwara

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU