KANISA LASAIDIA WALEMAVU ARUSHA



 ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu ameongoza Harambee kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa viungo mbalimbali vya mwili katika kituo cha Mtakatifu Yohane Paulo II kilichopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha ambapo zaidi ya shilingi milioni kumi na saba zimekusanywa.

Harambee hiyo imefanyika hivi karibuni katika kituo hicho ambacho kipo chini ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo mapadri, wachungaji kutoka madhehebu mengine pamoja na Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Arusha Amina Mollel  kupitia walemavu .

Akizungumza katika harambee hiyo, Askofu Mkuu Lebulu amesema kuwa kila mtu ana wajibu wa kuwasaidia walemavu na wasiojiweza kwa kutowabagua, bali wanapaswa kuonyeshwa upendo na mshikamano kwani nao ni binadamu kama wengine.

"Jimbo Kuu Katoliki Arusha tuliamua kuanzisha kituo hiki mwaka 1990 kuweza kusaidia jamii kwa wenye ulemavu na kushughulikia afya za watu mara baada ya kubaini kwamba wapo walemavu ambao hawapewi haki zao za msingi na badala yake wanafungiwa ndani wakidhani kwamba hawana umuhimu katika jamii, hivyo jambo hilo lilitugusa ndipo tukajidhatiti kuanzisha kituo hiki ambacho kimekuwa mkombozi wa wengi," amesema Askofu Lebulu.

Amesema kuwa Serikali, Asasi  za kidini, vyama vya kisiasa na jamii wanapaswa kuwaunga mkono huku wakiwa na moyo wa kusaidia wenye ulemavu kwa kujali afya zao bila kuonyesha dharau juu yao jambo ambalo litasaidia kuwafanya kuwa na amani ndani ya nafsi zao kwani wanapotengwa wanajisikia vibaya.

Naye Mbunge wa viti maalumu (CCM) Mkoa wa Arusha kupitia walemavu Amina Mollel ambaye ametoa milioni mbili na magunia tano ya mahindi, akielezea historia  ya maisha yake kwa simanzi kubwa amesema kuwa naye ni mlemavu wa mguu tangu akiwa mtoto mdogo wa miaka miwili  na kwamba kufikia hatua hiyo amekutana na changamoto nyingi ambazo zilimfanya aweze kutimiza ndoto zake.

"Mimi ni mlemavu, kabila langu ni mmasai na mama yangu ni kabila la mrangi, kipindi nikiwa mdogo mama yangu alitaka kutengwa kutokana na mila potofu, jamii iliniona siyo mtu halali lakini familia yangu iliniombea na kunisaidia mpaka hivi sasa kuwa Mbunge vitu maalumu kwakweli namshukuru sana Mungu amenitoa mbali, ni historia ndefu kwa hiyo niwatie moyo walemavu wenzangu msikate tama." Amesema Amina Mollel huku akijifuta machozi.

Aidha amesema kuwa jamii nyingi zimekuwa na mawazo potofu kwamba mlemavu si lolote na ni mkosi na wengine wamekuwa wakiwaua bila hatia kwa madai kuwa siyo riziki jambo ambalo ni dhambi kubwa mbele za Mungu kwani mlemavu ana haki sawa na binadamu mwingine, bali ni tatizo tu ambalo ni mpango wa Mungu.

Hata hivyo ametoa wito kwa uongozi wa kituo hicho kuunda kikundi cha walemavu ili waweze kupewa asilimia ya pesa inayotolewa na mfuko wa walemavu Halmashauri huku pia akiitaka jamii kuunda mtandao wa marafiki wa kituo hicho ambao watakuwa wakiwasaidia walemavu kwani taasisi nyingi tayari zinafanya hivyo.

Akisoma Risala, Mratibu wa kituo hicho cha walemavu, Mireile Kapilima amesema kuwa kwa sasa kituo kinahudumia walemavu zaidi ya 20,000 wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro, Simanjiro, Arumeru na Karatu huku lengo likiwa ni kutoa huduma za elimu kwa walemavu ili waweze kujikimu kimaisha wanapotoka hapo, kutoa elimu kwa jamii kutambua haki za mlemavu na kumjali.

“Kupitia kituo hiki kumekuwa na matokeo chanya kwa jamii kwani kwa kiasi fulani kumesaidia kupungua kwa unyanyapaa, kujitokeza wazazi kuwaleta kupata huduma za matibabu na wengine kuchangia gharama kidogo.”

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho ikiwa ni uendelezaji wake kwani kwa asilimia kubwa wanategemea wafadhili wa nje ambao wamekuwa wakipunguza bajeti siku hadi siku, hivyo kuiomba jamii kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia watoto hao kwani huduma ya chakula, malazi na matibabu inakuwa tatizo.




Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU