STENDI KUU WAANZISHA JUMUIYA, WAWA MFANO KWA WENGINE




WAKRISTO wanaofanya kazi katika maeneo ya stendi kubwa nchini wameshauriwa  kuanzisha umoja wa jumuiya ndogondogo katika maeneo yao ya kazi ili kushiriki masuala ya ibada na taratibu za Kanisa kwakuwa wengi wao hawashiriki kusali jumuiya katika makazi yao kwani muda mwingi wanautumia katika mazingira yao ya kazi.
Wito huu umetolewa na wanajumuiya ya “watakatifu wote” wafanyao kazi katika maeneo ya Stendi Kuu jimboni Sumbawanga hivi karibuni wakati wa maandamano ya matembezi ya msalaba wa Jubilei ya miaka 50 ya parokia ya Kanisa Kuu jimboni humo ambapo maandamano hayo ya kutembeza msalaba yaliuteka mji wa Sumbawanga  kuanzia maeneo ya stendi kubwa ya mabasi iliyopo Sokomatola na kuhitimishwa katika parokia ya Kanisa Kuu na kupokelewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi.
Akizungumza kwa niaba ya wanajumuiya ya Watakatifu Wote, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Ernesti Kasanka amesema kuwa tangu alfajiri hadi jioni wanashinda stendi, kwa maana hiyo wengi wao hawashiriki ibada za jumuiya majumbani na hivyo kusababisha kukosa huduma za kiroho pale inapotokea matatizo kwa wenzao au uhitaji wa sakramenti za Kanisa kwani wanakuwa na vipingamizi vya kutoshiriki ibada hivyo kuomba kuanzisha jumuiya katika maeneo yao ya kazi.
 “Kwa kiasi kikubwa sana tunaofanya kazi katika mazingira ya stendi hatushiriki ibada, tunaonekana ni kama wahuni, watu wa fujo na kwakuwa mazingira ya kazi zetu toka alfajiri mpaka jioni tunakuwa stendi hivyo tuliamua kuomba kuanzisha jumuiya kwa  kufuata taratibu na miongozo ya Kanisa na kuchagua viongozi tulikubaliwa na mpaka sasa kila siku za jumamosi saa kumi jioni tunakutana katika moja ya ofisi na kusali, na kwa mantiki hii tunashauri pia wakristo wakatoliki wenzetu wanaofanya kazi katika mazingira ya stendi kama sisi katika mikoa yote ya Tanzania waungane waanzishe jumuiya, na viongozi wa Kanisa watusaidie kwa hili maana itasaidia kuimarisha na kuongoa watu, kupunguza maovu na hata itasaidia kuondoa dhana potofu ya kuwa watu wanaofanya kazi  stendi ni wahuni, hawafai wasiomcha Mungu wala kuwa na hofu ya Mungu kitu ambacho si kweli, tunajua umuhimu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya kila mwanadamu, ingawa mazingira yetu ya kazi yanakua ni changamoto kushiriki jumuiya nyumbani,” amesema Ernest Kasanka.
Naye Filbert Lwela maarufu kwa jina la Sumbuko, mmoja wa wanajumuiya ya Watakatifu Wote amesema kuwa ni manufaa mengi ambayo wameyapata tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kwani vijana wengi wameweza kujitambua na kuanza kufunga ndoa hata kushiriki sakramenti za Kanisa lakini pia imesaidia kupunguza vurugu na tabia zisizofaa kwa baadhi ya vijana.
“Tumeiita jumuiya ya Watakatifu Wote kwakuwa ni mkusanyiko wa watu wengi na wanatoka katika vigango na parokia mbalimbali na imetusaidia kama mimi na wenzangu tumeshaandikisha ndoa na sasa tumejitambua, tabia ya ulevi asubuhi, wizi, udokozi, uhuni na kila aina ya tabia mbaya huonekana katika  maeneo ya stendi, lakini kwa sasa unashangaa kuona vijana wa stendi kuwa na hofu ya Mungu kiasi kikubwa, na baadhi yao waliasi dini sasa wanarudi na wengine kubadili dini na kuja katika Kanisa Katoliki kwani tunashirikiana katika shida na raha kama zilivyo jumuiya zingine,” amesema Sumbuko
Jumuiya ya watakatifu wote jimboni Sumbawanga imeanzishwa mwezi wa pili mwaka huu na imekuwa mfano pekee wa kusaidia kubadilisha imani na kuleta utulivu na jitoleo kwa Mungu ambapo jumuiya hii  itazinduliwa tarehe 29 Novemba  na inaongozwa na Mwenyekiti Ernest Gervansi Kasanka, Makamu Mwenyekiti ni Paskali Chakupewa, Katibu Mkuu Nuru Abdul, Katibu Msaidizi Ladislaus Wasoka na mweka hazina  Ernest Boazi (Shamba boy).




Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU