"VIJANA WAJIKABIDHI KWA BIKIRA MARIA"





VIJANA wanaopokea Sakramenti ya Ekaristi takatifu wameshauriwa kujiweka katika tunza ya Bikira Maria ambaye ni tabenakro ya kwanza ya Kanisa hasa wakati huu Kanisa Katoliki ulimwenguni kote linapokaribia kuingia katika mwezi wa rozali takatifu ili mama Maria aweze kuwaombea katika maisha yao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na paroko wa parokia ya Mwili na Damu padri John Greyson katika ibada ya kutoa sakramenti ya Ekaristi takatifu kwa vijana 64 iliyofanyika katika Kanisa la Mwili na Damu lililopo Kola jimboni Morogoro.
Padri Greyson amesema kuwa ibada ya rozali takatifu ni msingi wa Kanisa ambao unamwezesha muamini kuungana na Yesu Kristo katika sala mbalimbali za Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria mama wa ekaristi takatifu ili kupata neema ya utakataso.
Aidha padri Greyson ameyataja baadhi ya mambo yatakayowawezesha vijana hao kuungana na Yesu Kristo mojawapo ikiwa ni matendo ya huruma kwa kuwasaidia wahitaji, kujimega kama Yesu alivyojimega kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.
“Msiache kuwa na ibada kwa mama huyu mwenye huruma awaombee na kusisitiza hilo  nitampatia kila mmoja rozali tano muwasisitize wana familia muungane nao katika kusali rozali takatifu, nawakumbusha msiache kuungama mnapoanguka dhambini, mnapoteza mastahili ya kupokea sakramenti ya ekaristi takatifu, ili kupata mastahili hayo lazima kupata sakramenti ya kitubio, hayo ndio maisha ya Ekaristi zingatieni hayo,” amesema padri Greyson.
Wakati huohuo padri Greyson amewahimiza wazazi na walezi wa watoto hao kuwasaidia na kuchochea imani ya Kanisa Katoliki katika familia zao, kwa kuwakumbusha kuwa Kristo ndiye tumaini lao na Mungu ndiye msaada katika maisha yao yote, waendelee kuungana na Mungu kamwe wasimuache kwa kuishi nje ya mafundisho ya Kanisa.
“Ndugu zangu wazazi na walezi watoto hawa wamejifunza mambo mengi ya kiimani na mazuri, na mimi ninawaomba muwasisitize wazingatie imani ya Kanisa Katoliki kama dira ya maisha yao, wajifunze hayo yote kwa kuona mifano adilifu ya maisha yenu, kwa maombezi ya mama Bikira Maria mama wa ekaristi takatifu awape nguvu wasipoteze huo muunganiko kwa kusaidiwa na ninyi wazazi,”  amesema padri Greyson.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU