TUSIIACHIE JAMII ITULELEE WATOTO



Dunia kwa sasa inashuhudia maeneo mbalimbali yakikabiliwa na maovu, ambayo licha ya kwenda kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu, pia yanaviumiza viumbe vyake alivyoviumba.
Wakati wa uumbaji, Mwenyezi Mungu alikusudia dunia iwe sehemu nzuri na ya raha kwa kila kiumbe chake. Binadamu, wanyama, wadudu na mimea tofauti na makusudio ya muumba, vinaendelea kuteseka na mahangaiko ya kila kukicha.
Uharibifu wa mazingira, vita, ujambazi, utekaji nyara, ulawiti, ubakaji na maovu mengi yameendelea kuigubika dunia giza, tofauti na kusudio la muumba.
Yote haya kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mwanadamu. Kiumbe ambacho Mwenyezi Mungu alikiumba kwa mfano wake. Swali la kujiuliza kama binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu maovu yanatoka wapi?
Wazazi tumejisahau kwa kiasi kikubwa. Mtaa hauzai mtoto, magereza hayazai mtoto, bunduki hazizai mtoto, majangwa na ukame havizai mtoto, mtoto anazaliwa na mwanadamu tena mwenye mfano wa Mungu. La kujiuliza hapa ni je, imefika wakati tumeviachia vitu hivyo vituzalie na kutulelea watoto?
Kisingizio kikubwa kwa sasa kimekuwa “ubize”. Kweli, kulingana na hali ya maisha ambayo hairuhusu jinsia moja tu ndio itafute, wote baba na mama wanatafuta ili kuwajengea watoto maisha mema ya baadaye. Pamoja na utafutaji huo, bado hatutakiwi kujisahau katika utafutaji huku tukiwaachia watumishi wa ndani, walimu, majeshi, magereza, NGO’s na taasisi za kidini zitufundishie watoto wetu tabia.
Wazazi lazima tutambue kuwa jukumu la kuijenga kesho ya mtoto linaanza na sisi. Tusikwepe majukumu eti kwa kuwapeleka watoto mbali na sisi ili tupate nafasi ya kutimiza mahitaji yetu ya kimaisha hasa utafutaji wa pesa. Inasikitisha kukuta mzazi anampeleka mtoto mdogo ambaye hata kuongea vizuri hajaweza akasome shule ya bweni. Hapo unatarajia nini? Hiyo pesa unayotafuta itaziba matokeo ya mwanao kukengeuka kitabia?
Tukae nao, tusali nao, tuwasimulie hadithi, tuwape mifano ya mafanikio, mifano mizuri inayowajenga katika misingi ya upole, huruma, kusamehe, nidhamu, upendo na uvumilivu. Tusiwakwepe au kuwaweka mbali nasi. Tujitahidi sana kuziba mianya ya wao kukaa mbali nasi na hatimaye kupata nafasi ya kusomba tabia za ajabuajabu ambazo mwisho wa siku zinarudi kwetu.
Majambazi, wauaji, vibaka, wabakaji, walawiti, waharibifu wa mazingira, watekaji hawajatumwa na Mungu kuja kufanya hayo. Ni matokeo ya sisi wazazi kuwaweka mbali na hatimaye wakapata “walimu” mitaani au magheto hadi kufikia hapo. Humwoneshi upendo mwanao kila siku vipigo, matusi, kebehi,kashfa na kumdhalilisha, huchezi naye, unamtenga, humtimizii mahitaji yake, humpi mafunzo ya kiimani, humpi nafasi ya kufurahia uwepo wako duniani, hapo unatarajia nini?
Mwenyezi Mungu wabariki watoto wetu.

Bernard James

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU