PAROKIA MPYA YAZINDULIWA DODOMA



ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Nzinje jimboni humo huku akiwataka wakristo kulitumia ipasavyo Kanisa la parokia hiyo kwa kuwatumia mapadri kubariki ndoa, kubatiza na kupata huduma nyingine za Kanisa.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika homilia yake kwenye adhimisho la kutabaruku Kanisa na kutangaza parokia mpya ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Nzinje.
Amesema kuwa wakristo hao wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kupata parokia, kumbe wanalo jukumu la kuhakikisha wanapata huduma za kiroho kanisani hapo pamoja na masakramenti mbalimbali.
Askofu Mkuu Kinyaiya amefafanua kwamba waamini hao hawana budi kuwa wamisionari wa kulitangaza neno la Mungu na kuwavuta wakatoliki wengine kufika kanisani hapo kusali.
“Ndugu zangu leo tunapotabaruku Kanisa hili, lazima tujue ni nyumba ya Mungu, hivyo basi litumike kwa kazi yake Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Askofu Mkuu Kinyaiya.
Askofu Mkuu Kinyaiya amewashukuru na kuwapongeza waamini wote wa parokia hiyo kwa majitoleo yao ambayo walitumia nguvu kwa ajili ya kusomba kokoto, mchanga na rasilimali fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.
“Nina kila sababu ya kuwashukuru kwa yote mliyoyafanya hasa kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili, na pia nashuhudia sasa mnajenga nyumba ya mapadri hongereni nyote,” amesema Askofu Mkuu Kinyaiya.
Ibada ya misa takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa parokia hiyo imehudhuriwa na idadi kubwa ya waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na mke wake mama Tunu Pinda na viongozi wa dini mbalimbali.

Wakati huohuo Askofu Mkuu Kinyaiya amefungisha jumla ya ndoa takatifu nne kwa waamini wa Kanisa hilo.

Amewasisitiza wanandoa hao kutunza viapo vyao vya ndoa na kuzilea familia zao watakazopewa na Mungu kwa upendo na maadili ya dini ya kikristo.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU