PAROKIA MPYA YAZINDULIWA JIMBO KUU KATOLIKI DODOMA



KATIKA  safari  ya  kueneza   Injili  kwa  watu  wote  hapa  duniani, Jimbo  Kuu  Katoliki Dodoma  limepata  Parokia  mpya  ya  Pwaga  iliyozinduliwa  hivi  karibuni  na  Askofu  Mkuu  wa Jimbo  hilo Mhashamu   Beatus  Kinyaiya OFM-Capp.

Akizindua parokia  hiyo  mpya hivi karibuni, Askofu  Mkuu Kinyaiya OFM-Capp amesema  kuwa  safari  ya  injili  ni ngumu  na  kuwa  si  vyema  wanadamu   kuipuuzia   kwani  ni  safari  ya  toba huku Kanisa  likiwa ni  moyo  wa  muamini  popote  pale na  kuwa  pamoja  na  kuwa  parokia  hiyo  mpya  haina  jengo  kubwa lakini Kanisa  ni  watu  na ni  popote  pale bila kujali  ni  wapi  wanasalia, la msingi ni kuwa  na  imani  kwa  Mungu.

“Mama   Kanisa   anasisitiza  watu   kusali  kwa  moyo  na  nguvu  kubwa   bila  kujali  sala   inafanyika  wapi, mkristo  anatakiwa kusalia  mahali  popote   kwani  sala  ni  Baraka  na muamini  anapata  nafasi  ya  kuongea  na  Mungu  na  si  Kanisa. Parokia  ya  Pwaga  kwa  uchanga   wake  wa  majengo  isiwe   sababu  ya  kuibeza   bali  na   itiwe  nguvu  na  waamini  wake   kwa  kusali   kwa  nguvu   na  kuwa  suala  la  majengo  makubwa  na  mazuri  yatakuja  baadaye.” Amesema Askofu Kinyaiya.
Amesema   parokia   mpya  ya  Pwaga   imefunguliwa   kutokana   na  mahitaji  ya  waamini kutaka  huduma  za  kiroho  kufanyika  karibu  nao  na kuwa ombi hilo lilitolewa kwa  marehemu  Askofu  wa  pili  wa  Jimbo Kuu  Dodoma  Mhashamu  Joseph Isuja Shungu  miaka  30  iliyopita yaani mwaka  1987.
“Kristo  hapatikani  katika  majengo  mazuri  bali  anapatikana  katika  mioyo  yenu, saline kwa  nguvu   msitafute  pa  kusalia bali  pa  kusalia  pawe  popote  ili  mradi  mnasali  kwa  moyo  na  Kristo  atapatikana  hapo  hapo  mlipo, msifadhaike  mioyoni  mwenu. Majengo  mazuri  na  makubwa  yatakuja,  ruhusuni Roho  Mtakatifu  aingie  mioyoni  mwenu  atawaelekeza cha  kufanya  huku  mkijitoa  kama  mlivyojitoa  katika  ujenzi  wa  nyumba  hii  ya  mapadri.” Amesisitiza.
Amesema  kwa  sababu  parokia  hiyo  ya  Pwaga  inaanza  chini  yake,   ni  vyema  iwe  kioo  kwa  ajili  ya  kufundisha    watu   kumuongokea   Mungu  huku  akiwaonya  wana  kipaimara  26  aliowapa  sakramenti  siku  hiyo kulisikia  neno  hilo  na kulifuata.
Pamoja  na  kutangazwa  kwa  parokia  hiyo  mpya  Askofu  Mkuu  Beatus  Kinyaiya  OFM-Capp  amemtangaza  Padri Nestory  Ngunwa  kuwa  paroko  wa  parokia  hiyo mpya  na  kuwa  kwa  sasa  atakuwa   akikaa  parokiani  Lumuma  hadi  hapo  nyumba  mpya  ya  mapadri  hapo  Pwaga  itakapomalizika.
Paroko  wa Parokia  hiyo  mpya, padri  Ngunwa  amesema  kuwa  anamshukuru  Mungu  kwa  kumuona,  na kwa  kutumwa na Askofu katika  parokia  hiyo, ataifanya  kazi  ya  Bwana  kwa  moyo wote.
Parokia  hiyo  mpya  ya  Pwaga  ina  vigango  12  ambavyo  ni   Godegode, Mgoma, Kisisi, Tambukareli, Wisuzaje, Idibulilo, Lufu, Kidenge, Gomhungile, Munguwi, Idaho na Maswala .   

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU