SHAMBULIZI DHIDI YA TUNDU LISU LASIKITISHA WATANZANIA
Maaskofu waonya
Na Pascal Mwanache, Dar
MAASKOFU Katoliki
Tanzania wamelaani vitendo vya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani
vinavyoendelea nchini na kusema kuwa vitendo hivyo vinalifedhehesha Taifa kwa
kuwa ni dhambi, uhalifu na siyo utamaduni wa Tanzania.
Wamesema hayo katika
tamko walilolitoa Septemba 11, 2017 ambapo wametaka vitendo hivyo vikomeshwe
mara moja.
“Tunatamani kuona
wale wote walio nyuma ya matukio haya ya vurugu, mauaji, utekaji na utesaji
wanatafutwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” imeeleza sehemu
ya tamko hilo.
Akiongelea tamko
hilo la maaskofu, Makamu Mkuu Mstaafu wa
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania, Padri Dkt. Charles Kitima amesema
kuwa Maaskofu wametoa tamko hilo kwa kuwa ni haki na wajibu wao wa msingi kama taasisi
iliyo na wajibu ndani ya jamii ya kulea maadili ya watu na kulinda utu wa kila
binadamu.
Amesema kuwa Kanisa
kama taasisi lina jukumu la kuhakikisha malezi ya uadilifu kwa viongozi na kwa
umma yanazingatiwa na yanapewa kipaumbele, na kuongeza kuwa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 ndiyo inayowapa uhalali maaskofu kuelekeza
jamii juu ya kulinda utu, amani, haki na
wajibu msingi ambazo ni stahili ya kila mtu kwa sababu ya ubinadamu wa kila
mmoja.
Aidha Dkt. Kitima
amesema kuwa Taifa la Tanzania halikuzoea matukio ya namna hii, jambo
linaloashiria kupwaya kwa utawala wa sheria.
“Kudhuru ama
kupoteza maisha ya mtu yeyote si tendo linalokubalika mbele ya Jamii, Mungu na
mbele ya Katiba yetu ya Muungano. Ni kinyume na utawala wa sheria. Hili sasa ni
tatizo kubwa linalokiuka Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Matukio haya yamesikitisha
watu wote wenye kuheshimu utu wa binadamu hata kama hakubaliani na wengine.
Mungu hakubaliani na
uovu huu ndio maana maaskofu wanaonya wahusika na watekelezaji wa matendo haya
kuacha tabia hiyo kwani inapingana na mpango wa Mungu wa kumuumba binadamu ili
afurahie hadhi ya utu na uhai wake, zawadi pekee yenye kuonyesha sura na mfano
wa Mungu aliye hai.
Nchi lazima ilinde
uhai wa kila binadamu ndani ya Tanzania hata kama ni uhai wa mhalifu. Serikali
iendeshe shughuli zake ikizingatia na kuongozwa
na katiba ambayo inapaswa iheshimiwe kwani hakuna mtu wala kiongozi
yeyote aliye juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Amesema.
Utu
hauthaminiwi kwa sasa.
Pia Padri Kitima
ameongeza kuwa kwa sasa utu (human dignity) wa mtu hauthaminiwi ambapo binadamu
anaweza kupotezewa heshima na hata maisha yake, na kuonya kuwa wale wanaofanya
hivyo wasipopewa onyo Taifa litaelekea pabaya.
“Taifa linalopuuza
utu linajiangamiza. Utu tunaozungumza hapa ni wa kila mtu siyo wa mtu fulani
tu. Hata muhalifu ana haki zake za msingi. Ibara ya 14 inatambua haki ya uhai
wa kila mwanadamu, awe msafi au asiwe msafi, awe muhalifu au la, ana haki ya
kulindwa. Unapojiamulia kuua mtu kwa sababu yoyote ile inaleta uvunjifu wa
katiba.
Ni mahakama pekee
ndicho chombo kinachoweza kutoa hukumu dhidi ya mhalifu.Taifa letu linaelekea
kubaya kwa sababu utu haupewi tena kipaumbele, tunaweka kipaumbele vitu kuliko utu, tukumbuke kuwa
Mungu hapendi uovu wetu wa kupuuza utu wa ndugu zetu, tutawajibika mbele ya
Mungu,” Ameeleza.
Kadhalika
amekumbusha kuwa ni wakati mwafaka sasa, wale wanaoshughulika na masuala ya
umma warejee katika misingi ya Taifa ya mshikamano, umoja na amani kwa kila
mtu.
“Hatuwezi kuwa
tunang’oa mizizi ya matatizo yaliyopo kwa njia ovu; ni kweli Serikali
inapambana na rushwa na wizi wa rasilimali za umma, lakini yote hayo lazima
yafanyike kwa kuzingatia utu na utawala wa sheria. Hatuwezi kuondoa uovu kwa
kutumia uovu kwa sababu sisi sote tutawajibika mbele ya jamii na mbele ya Mungu
kwa kuulinda utu. Anayepuuza utu hata afanye kizuri namna gani, hakitakuwa na
baraka za Mungu.
Tunaondoa uovu kwa
kutumia sheria na njia nzuri iliyokubaliwa na watu wenye mamlaka ya nchi hii.
Vyombo vya dola vimepewa mamlaka ya
kuendesha nchi kwa utashi wa raia wa Tanzania hata kama wana uwezo wa kufanya
lolote watakalo bado kutotii utashi wa watanzania ni usaliti dhidi ya utashi wa
wananchi na katiba yetu ya watanzania.” Amesema.
Akielezea matukio ya
kuvamiwa kwa ofisi za wanasheria, kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu Lisu na kesi
mbalimbali zinazoendelea nchini, Dkt. Kitima amesema kuwa matamko mengi
yametoka kwa viongozi kadhaa dhidi ya Tundu Lisu, lakini yeye alikuwa
anasimamia taaluma yake kama mwanasheria anayemtetea mwanadamu pia ambaye anafuata misingi ya haki za binadamu.
“Baba wa Taifa
tarehe 25 oktoba 1961 alipokuwa akizindua Chuo Kikuu cha kwanza Tanzania (Dar
es Salaam University College) alisema tunaaanza na kitivo cha sheria ili
kujenga Taifa litakaloongozwa na sheria, na pia aliasa watanzania waheshimu
haki za watu wote,, yeye Nyerere amekuwa kielelezo cha uongozi bora na kuweza
kutatua matatizo makubwa na hata kung’oa ufisadi wa kila aina kwa kuongozwa na
utaratibu wa kisheria. Alikuwa na uwezo wa kujenga mwafaka na wenye hoja
tofauti na zake kwa njia ya masikilizano (consensus building) kwa kuongozwa na
sheria ndio maana tumekuta rasilimali nyingi na amani na heshima kwa viongozi
wetu.
Na hiyo ndio
ilifanya aseme hatuwezi kuwa Taifa huru bila Chuo Kikuu chetu wenyewe akitaka
tuongozwe na waelewa wa fani mbalimbali ili tuweze kujijengea Taifa huru letu
wenyewe tuheshimu wataalamu wetu hata kama ushauri wao ni mgumu kuupokea.,
taifa hili ni letu wote na kila mmoja anahitaji kusikilizwa. Kuwapuuza wenye
maoni tofauti si utanzania, tuwasilize
na kuwaelimisha kama hawaelewi na hata watuelimishe nasi pia,” Amekumbusha.
Amesema kuwa hata
mhalifu ana haki ya kutetewa mahakamani kwa sababu ya utu wake, lengo
likiwa ni kumsaidia atendewe kwa haki kisheria
na wala si kutetea uovu wake. Kila mtu ana haki ya kujitetea mahakamni kwa
kupewa hudumu za kitaalamu ikiwepo huduma ya utaalamu wa kisheria..
Amesema sisi sote ni
wadhambi na Kanisa lipo kwa ajili ya kuwabadilisha wadhambi waache uovu
waongoke na ndicho hicho kilichomfanya Yesu awe kati yetu wanadamu. Wanasheria
wanapowatetea wahalifu nia yao ni kuwasaidia pia wabadilike kwa kuheshimu
sheria zetu hasa Katiba.
“Lakini ikumbukwe
kuwa wapo baadhi ya wahalifu
wamesingiziwa. Sasa unapoona
wanasheria wananyimwa majukumu yao ya kitaaluma kuwatetea watu kama hawa
inakuwa siyo halali. Zaidi ya hayo Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inasema kila mmoja ana haki ya kusimamia maoni yake ikiwa ni pamoja
na maoni ya taaluma yake. Hawa watu wasinyimwe haki ya kuwatetea wahalifu mbele
ya mahakama ili haki itendeke kisheria, kwa sababu wahalifu bado utu wao una
thamani kuliko maslahi yetu yapitayo, uhai unadumu milele,” Ameeleza.
Kwa nini
matukio hayo yanalaaniwa?
Aidha amebainisha
kuwa maaskofu wanalaani matukio hayo na
kuwataka wote waliohusika kuacha mwenendo huo kwani hakuna jamii iliyoweza
kukomesha uhalifu ama uovu wowote kwa kuangamiza wengine. Ni jukumu la kueneza
utawala wa sheria na uheshimu wa haki za kila mtu ndipo tutajenga Taifa lenye
mafanikio kiuchumi na kisiasa.
Serikali ndiyo yenye
jukumu la kulinda utu wa kila mtu na mali zake. Viongozi wa dini zote wana haki
ya kuwahabarisha viongozi wa Serikali juu ya uadilifu, thamani ya utu, haki
msingi za kila mtu na juu ya tunu za taifa ambazo ni WATU, ARDHI, SIASA
SAFI, UONGOZI BORA.
“Tumejenga nchi hii
kwa sababu ya siasa safi, tulikwepa siasa chafu ndio maana Tanzania ilipata
uhuru bila vita vya mtutu, na hivi Tanzania ilikuwa kimbilio la ukombozi wa
Afrika. Tuliitwa USWISI ya Afrika. Tukipuuza utu wa mtu yeyote hata tujitetee
vipi hatutaaminika wala kupata maendeleo yeyote. Kila nchi ina historia yake.
Historia yetu ndio hiyo na wala haiwezi kuwa historia ya China wala ya
Marekani. Hata watanganyika/watanzania
wenye mawazo tofauti waliheshimiwa na kuondoka nchini walipoona hawako tayari
kwendana na tunu zetu.
Tanzania tumekuwa
Taifa lisilo na waasi bali Taifa lenye watu wenye mitazamo tofauti.
Tulipokubali mfumo wa Vyama vya siasa lengo letu lilikuwa kujifunza kuachiana
madaraka kwa njia ya uchaguzi wenye kuheshimu Katiba na sheria. Na hivi vyama
vya kisiasa vilivyosajiliwa vyote vina hadhi sawa.
Wanaopata fursa ya
kuongoza hupewa ushirikiano kwa mujibu wa sheria. Wapinzani wa kisiasa wa
Tanzania ni watu wema na wanastahili kutendewa kiutu na siyo kuonewa na
kunyanyaswa. Ni hatari kubwa kitaifa
kuwanyanyasa wapinzani. Kazi ya viongozi wa dini ni kuipa Serikali
taarifa ambayo ina ukweli kwa pande
zote, kisayansi na kiutu. Maaskofu wanategemea nia njema ya walengwa wa ujumbe
wao kuuheshimu na kuutendea kazi kadiri ya taratibu za kisheria,” Amehimiza.
Tanzania ni jamii
yenye kupenda amani na umoja na haya ni matunda ya kuulinda na kuuheshimu utu
wa kila mtu. Ujumbe wa Maaskofu unawakilisha kiu ya kila mtanzania kupinga
ukiukaji wa misingi ya utu.
Comments
Post a Comment