SHINYANGA WAPATA MAPADRI WAPYA
|
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu
Liberatus Sangu ametoa Daraja Takatifu ya Upadri kwa mashemasi wawili wa
Parokia ya Nyalikungu – Maswa, mapema
Agosti 22, 2017.
Misa hiyo ya upadrisho imefanyika katika viwanja vya Kanisa la
Bikira Maria Malkia wa Mashahidi wa Afrika mjini Maswa na kuhudhuriwa na
mapadri kutoka ndani na nje ya jimbo la Shinyanga, Viongozi wa serikali, Watawa
pamoja na waamini.
Wakati wa misa hiyo Askofu Sangu
amemshukuru Mungu kwa kulijalia Jimbo la Shinyanga kupata Makasisi wapya.
Mapadre hao wapya ni James Jidasanja na James Misana ambao walikuwa miongoni
mwa mashemasi watatu waliopewa daraja la ushemasi na askofu Sangu mnamo
Februari 2 mwaka huu 2017 katika kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo mjini
Shinyanga.
Akitoa neno mara baada ya misa kwa
niaba ya mapadri na waamini wa parokia ya Nyalikungu, Paroko wa Parokia ya
Nyalikungu Padri Simon Maneno ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha mapadri hao wapya katika urika
wa mapadri na kumshukuru Mungu kwa
zawadi ya Mapadri hao wapya ndani ya Jimbo.
Pia amemshukuru askofu wa jimbo la
Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu kwa kuongeza watenda kazi wengine
watakosaidia kazi ya kikuhani katika Jimbo la Shinyanga.
Akizungumza kwa niaba ya mwenzake mara
baada ya misa ya upadrisho padri mpya James Jidasanja amemshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kuwawezesha kufikia daraja hilo la upadri na pia wamewashukuru wazazi
wao na wote waliowasaidia kufikia wito huo huku wakimshukuru Askofu Sangu kwa kukubali kuwapa daraja
takatifu la upadri na kuwaweka kuwa miongoni mwa makasisi wa jimbo la
Shinyanga.
Akizungumza kwa niaba ya serikali
katika sherehe hizo za updrisho Mkuu wa
Wilaya ya Maswa Dkt. Seif Shekalaghe amepongeza juhudi zinazofanywa na Kanisa
Katoliki kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi
kwani kwa muda mrefu limekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali na hasa katika
nyanja za elimu na afya.
Ametoa mfano jinsi Kanisa lilivyoweza
kuanzisha taasisi nyingi za kielimu ikiwemo shule za sekondari pamoja na
kujenga Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza ambayo inahudumia
Watanzania wengi bila ubaguzi.
Mkuu huyo wa wilaya pia alilielezea
Kanisa Katoliki kuwa lina mchango mkubwa
katika kudumisha amani na utulivu wa nchi na alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuwa macho na watu
wanaotaka kuvuruga amani na kuhakikisha wanailinda amani iliyopo ikiwa ni
pamoja na kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama pale wanapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani ili
hatua ziweze kuchukuliwa mapema.
Comments
Post a Comment