Serikali kurahisisha huduma za DNA
SERIKALI imedhamiria kununua mashine tatu
za vipimo vya vinasaba (DNA) ili zitumike katika maabara za Kanda na hivyo
kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangala wakati akijibu
swali la Mbunge wa Chumbuni Mhe. Ussy Pondeza kuhusu ucheleweshwaji wa matokeo
ya uchunguzi wa sampuli ikiwemo sampuli za makosa ya jinai.
Dkt Kigwangala amesema kuwa Serikali
ina mkakati wa kuongeza mashine hizo ili kuwezesha uchunguzi kufanyika kwa
wakati kwa vielelezo vya makosa ya jinai ikiwa ni pamoja na vitendo vya
udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
“ Sampuli za uhalali wa watoto kwa
wazazi zinafanyika kwa wepesi zaidi kuliko sampuli za makosa ya jinai kwani
sampuli hizo zinachukuliwa moja kwa moja toka kwa wahusika hivyo kurahisisha
uchunguzi wake endapo wahusika wa uchukuaji watachukua kwa umahiri na uhifadhi
utafanyika kwa namna stahili,” Amefafanua Dkt. Kigwangala.
Aidha, Dkt. Kigwangala amesema kuwa
sampuli za uchunguzi wa makosa ya jinai zinachukuliwa toka maeneo ya matukio
hivyo uchunguzi wake unaweza kuchukua muda zaidi kutegemeana na aina ya sampuli
na eneo zilipotoka.
Vilevile Dkt. Kigwangala ameongeza kuwa
Serikali ina mpango wa kuanzisha kituo cha kupima vinasaba (DNA) Mkoani Mbeya
kwa lengo la kupunguza ucheleweshaji wa matokeo ya uchunguzi.
Mbali na hayo akijibu swali la Mbunge wa
Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia kuhusu Serikali kuagiza tohara kuwa lazima kwa
wanaume nchini, Dkt. Kigwangala amesema kuwa si rahisi kwa Serikali kuagiza
tohara kuwa lazima japokuwa ina faida
kiafya kwa wananchi.
“Tohara inasaidia kupunguza maambukizi ya
Saratani ya shingo ya Uzazi kwa wanawake pamoja na maambukizi ya virusi vya
Ukimwi,” Ameongeza Dkt. Kigwangala.
Aidha, amesema kuwa elimu kuhusu tohara
imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo Serikali kwa kushirikiana na
wadau katika Mikoa ya kipaumbele imekuwa
ikitoa elimu kabla na baada ya huduma ya tohara katika vituo vya kutolea huduma
za afya.
Asante. Mtakuwa mmtuokoa vijana na kusingiziwa watto
ReplyDelete