UKIMYA WA KANISA KATOLIKI UTAWAPOTEZA WAAMINI

θ Lijibu changamoto za sasa kupitia sayansi na teknolojia
n Na Thompson Mpanji,Mbeya
MKURUGENZI wa Radio Vatikani, Sean Patrick Lovett amelialika Kanisa Katoliki Tanzania kujenga utamaduni  wa mawasiliano  kwa kutumia vyombo vya habari mahalia  kuendana na Sayansi na Teknolojia ili kufikisha mafundisho na ujumbe wa Viongozi wakuu wa Kanisa kwa waamini.
Mkurugenzi huyo amesema hayo wakati wa semina  iliyowahusisha mapadri,Watawa wa kike na kiume, mafrateri, viongozi wa Parokia,Wakurugenzi na baadhi ya wafanyakazi wa Idara za Jimbo Katoliki la Mbeya  iliyofanyika Septemba mosi 2017 katika Ukumbi wa Parokia  ya Mbeya Mjini.
Sean amesema kuwa ni jukumu la Maaskofu, Maparoko,Wakuu wa Mashirika,Wakurugenzi wa Idara mbalimbali, Viongozi wa Parokia  na  Halmashauri za Walei  sanjari na vyama vya kitume kuvitumia vyombo vya habari vya Kanisa na waandishi wake   kufikisha ujumbe na mafundisho ya Kanisa.
Huku akitolea mfano wa Baba Mtakatifu Francisko  alivyokuwa wazi kuendana na ulimwengu wa kidijitali kwa kutumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe ikiwemo kuzungumza na  kila mtu duniani kwa muda mfupi kupitia Twitter, Instagram, Face book na vyombo vingine vya habari vivyo hivyo kwa  Viongozi wa Kanisa mahalia na waamini wanapaswa kuiga mfano huo.
“Tunajaribu kumuona Papa Francisko  alivyofungua mitandao ya kijamii ili kuendana na sayansi na Teknolojia …kuendana na wakati na mahitaji ya sasa, amekuwa akitumia na kujiwekea muda wa kuwasiliana na  kila mtu kupitia mitandao na vyombo vya habari na hivi ndivyo Kanisa la Tanzania na la kiulimwengu linapaswa kufanya”.
“Tuangalie  wengine hususani waamini wetu na kuwapa  mahitaji yao ya kiroho kwa haraka na ukarabu kupitia vyombo vya habari vya Kanisa.
Lazima tuwe wazi tusijifungie kwani ulimwengu umebadilika, kwa hiyo tukiwa hatuwi wazi kuwapatia mafundisho kupitia mitandao na vyombo vya habari,kufikisha ujumbe wa Kanisa  na maandiko zikiwemo Sheria na Taratibu za Kanisa  ….watakwenda kuangalia na kusikia  kwa wengine  na matokeo yake  tutawapoteza, hivyo mawasiliano na kutumia vyombo vyetu na waandishi wetu ni muhimu kwa sasa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo katika Kanisa,”amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Aidha amezungumzia umuhimu wa majimbo kuanzisha vyombo vya habari ikiwemo Radio, Televisheni, Magazeti na mitandao ya kijamii ikiwemo Tovuti za majimbo  na blogs ili  waamini waweze kuendelea kupata habari, mafundisho na ujumbe  wa Kanisa.
Hata hivyo  washiriki wa semina hiyo wamepongeza msimamo na muelekeo huo wa Kanisa Katoliki kwa mahitaji ya sasa badala ya kuwepo kwa ukimya  ambao watoto na  vijana  wanaweza kushindwa kulielewa vyema Kanisa lao na hatimaye kuweza kukengeuka  na kukimbilia katika madhehebu.
Katika semina hiyo  Askofu Evarist Chengula  wa Jimbo Katoliki Mbeya  alionesha kufurahishwa na mafundisho hayo huku Mkurugenzi huyo akimshukuru Askofu kwa kumwalika kutoa semina hiyo ambayo  ni muhimu kwa Kanisa Katoliki duniani kuendana na mahitaji ya sasa kwa afya ya Kanisa kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU