SERIKALI IANGALIE UPYA WALIOFUKUZWA KWA VYETI FEKI
SERIKALI imeombwa kuangalia
upya hatua yake ya kuwatoa katika ajira watumishi waliogundulika kuwa na vyeti
feki kwa kuwalipa japo kwa kuwafuta jasho.
Rai hiyo
ilitolewa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi TUCTA Yahya
Msigwa katika washa ya watalaam ya kupitia sera za Ukimwi na afya kazini.
Alisema
kuwatoa katika ajira bila kuwapa chochote kunawafanya watumishi hao kuwa
masikini ghafla ukizingatia kuwa katika maisha yao walitegemea mishahara.
Msigwa
alisema kuwa pamoja na TUCTA kutokuwa na tatizo na uamuzi huo wa
serikali,lakini watumishi hao wengine wana mikopo kwenye taasisi mbalimbali za
fedha ikiwa ni pamoja na benki.
“Kitendo cha
kuwaondoa ghafla watumishi hao nafikiri hata hizo taasisi zilizokuwa
zikiwakopesha zitaathirika kwa kuwa
mikopo hairejeshwi hivyo suala hilo liangaliwe,’’alisema.
Alisema
ingawa ni makosa kisheria kwa mtumishi kuwa na cheti feki lakini iangalie kwa
jicho la karibu kuwa watumishi hao wanawategemezi pia.
“Sisi kama
TUCTA hatuna ugomvi na serikali lakini ombi letu serikali iangalie jinsi ya
kuwasaidia watumishi hawa hata kuwalipa fedha kidogo kwani walikuwa watumishi
wazuri tu,” alisema .
Alisema
tatizo siyo wao bali ni mfumo uliokuwepo wakati wakiingia kwenye ajira zao
kipindi cha nyuma.
Aidha katibu
huyo aliwataka viongozi wanaohudumia matatizo ya wafanyakazi kutatua matatizo
hayo kwa kipindi kifupi.
Alisema
kumekuwa na matatizo mengi ya wafanyakazi ambayo huchukua muda mrefu kutatuliwa
jambo ambalo linawakatisha tama watumishi hao.
Akizungumzia
masuala ya Ukimwi katibu huyo alisema ni vyema watumishi wenye maambukizi ya
Ukimwi sehemu za kazi wakapewa haki zao kama watumishi wengine.
Comments
Post a Comment