Utambulisho wa watawa uwe umoja na Upendo- Ask. Ruzoka
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora
Mhashamu Paul Ruzoka amewataka watawa nchini kufanya kazi kwa ushirikiano
mkubwa wakizingatia karama za mashirika huku wakipendana na kusaidiana katika
maendeleo ya jumuiya zao za kitawa.
Askofu Ruzoka ameyasema hayo hivi
karibuni baada ya Adhimisho la Misa
Takatifu ya kumbariki Abate Pambo Martini OSB katika Abasia ya Roho Mtakatifu
Mvimwa, Jimbo Katoliki Sumbawanga.
Akimpongeza baada ya kuchaguliwa kwake
kuwa kiongozi wa Abasia ya Mvimwa, Askofu Ruzoka amemtaka Abate pambo kufanya
kazi kwa moyo mkuu ulio na uvumilivu kwani amepewa majukumu mazito ambayo
hakuyatarajia bali Mungu humchagua amtakae kwa ajili ya wengine ili aweze kuwa
kiongozi .
“Kila cheo kina uzuri wake, magumu yake
na uzito wake lakini Yesu Kristo alishatuelekeza kuonja magumu hayo. Itatokea
wakati mwingine mtu akufunge mikono na kukupeleka usikotaka, hivyo tambua sana
kuchaguliwa kwako kuwa Abate kwa niaba ya wanashirika, kunamkumbusha kila mtawa
katika Abasia ya Mvimwa kuwa na umoja na upendo ili mumjenge Kristo Yesu katika
abasia yenu ili jamii ya wakristo wapate manyunyu ya imani kutoka katika
jumuiya yenu” amesema Askofu Ruzoka
Akitoa shukrani kwa mwenyezi Mungu
mbele ya waamini na viongozi mbalimbali wa kiserikali, Abate Pambo amewashukuru watawa wenzake wa Abasia ya
Mvimwa kwa kumchagua kuwaongoza akiwa kama abate wao, na kuwaomba kumpa
ushirikiano wa dhati katika maendeleo ya kiroho na kijamii yatakayokuwa msaada
kwa watu mbalimbali pasipo ubaguzi wala kujali dini, kabila, rangi na tofauti za
kisiasa.
“Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa
kunipatia madaraka ya utumishi kwa wenzangu, pia namshukuru sana Baba Askofu
Damian Kyaruzi kwa maombezi yake na zaidi sana kwa kunipatia Baraka ya uabate
siku hii ya leo. Ni huyu baba ambae amenizaa katika upadri Julai 10, 2005 na leo miaka 12 baadae
amenibariki kuwa Abate akitanguliza
mafundisho ya dhati katika utume wangu, kwa kweli namshukuru sana”.
amesema Abate Pambo.
Ameongeza kuwa cheo ni dhamana hivyo
madaraka wanayokabidhiwa wanawiwa kuyatumia kwa hekima na busara. Amesema
madaraka ni kwa ajili ya watu na utumushi, na hakuna anayepewa madaraka kwa
ajili yake yeye mwenyewe.
“Na zaidi tuendelee kutoa ushirikiano kwa
serikali, vyama vya siasa, taasisi binafsi na mtu mmoja mmoja katika kuleta
maendeleo ya kiroho, kiimani na kijamii. Pia tunaiomba serikali izidi
kushirikiana na taasisi binafsi na mashirika ya dini katika kuboresha
miundombinu katika maeneo ya Mvimwa kama
vile umeme, barabara za kudumu na maji
ili kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii zilizopo maeneo hayo” amesema.
Abate Pambo Martini OSB Amekuwa ni
abate wa tatu wa Abasia ya Mvimwa ambaye amesimikwa na Askofu Damian Kyaruzi wa
Jimbo la Sumbawanga katika misa ambayo ilihudhuriwa na maaskofu kutoka majimbo
mbalimbali kama vile Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki
Njombe, Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Askofu Liberatus Sangu
wa Jimbo Katoliki Shinyanga, na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda.
Wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni
Abate Romei Mbota wa Abasia ya Agbam nchini Togo, Abate Oktavian Masingo wa
Abasia ya Hanga, Abate Plasidius Mtunguja wa Abasia ya Ndanda, na Abate mstaafu wa Abasia ya Hanga Thadei
Mhagama. Viongozi wa serikali waliohudhuria ni pamoja na mama Anna Makinda,
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Comments
Post a Comment