MSINGI WA KANISA KATOLIKI NI EKARISTI TAKATIFU
KANISA
Katoliki kamwe haliwezi kuchoka katika kuadhimisha fumbo la Ekaristi Takatifu
ambalo liliachwa na Yesu mwenyewe miaka elfu mbili iliyopita hasa siku ya
Alhamisi kuu, kama kiini cha Kanisa na chimbuko lake linalomwezesha mwanadamu
kupata neema ya utakaso mara baada ya kufanya toba.
Sakramenti
ya Ekaristi takatifu ni utajiri wa Kanisa Katoliki katika maumbo ya mkate na
divai ambapo Yesu alitoa mwili wake na damu yake kwa ajili ya ukombozi wa
mwanadamu alipowaalika waamini kuula mwili wake na kuinywa damu yake ndio
sababu ya Kanisa Katoliki kuendelea kuheshimu sakramenti hiyo kama chimbuko la
Kanisa lenyewe
Wito huo
umetolewa na paroko msaidizi wa parokia ya Bikira Maria wa Calmeli Dr Stan
Rodrigues ambaye pia ni mtaalam katika masuala ya ndoa na familia katika
adhimisho la kutoa sakramenti ya Ekaristi takatifu kwa vijana 86 iliyofanyika
parokiani hapo Kihonda maghorofani jimboni Morogoro.
Dr.
Rodrigues amesema kuwa inasikitisha kuona baadhi ya waamini kushindwa kutambua
neema ipatikanayo katika mafumbo hayo, hali inayosababisha wengi wao kupokea
sakramenti hiyo katika hali ya dhambi na wengine kushindwa kabisa kushiriki
mafumbo hayo, akitolea mfano wanakwaya wa nyimbo za liturujia ambapo hali hiyo
imekuwa dosari ndani ya Kanisa katika sehemu mbalimbali.
“Ninyi
wanakwaya wataalamu sana kuimba na kucheza kanisani, inashangaza mmekuwa
watazamaji kwa sababu mnahamasisha waamini kwa nyimbo nzuri lakini wakati wa
komunio takatifu hamuendi kupokea, yale ambayo mnaimba lazima yaendane na
maisha yenu ya kiroho msipoteze maana ya mafumbo haya, na utajiri wa Kanisa
ambao Yesu ametuachia katika maumbo ya mkate na divai, utajiri huu una maana
kubwa tuzingatie na kupokea,” Amesema Dr Rodrigues.
Aidha
amesema kuwa wakati mwingine waamini wanadhani kwamba Sakramenti ya Ekaristi
takatifu imewekwa kwa walio watakatifu na matajiri tu, kumbe sakramenti hiyo
inamhitaji kila mmoja kuijongea akiwa katika hali ya utakataso ingawa Yesu
haonekani kwa macho isipokuwa katika maumbo ya mkate na divai.
Mbali na
hayo Dr Rodrigues amesema kuwa katika dunia hii kuna dini na madhehebu mengi
sana, na hakuna mwanzilishi wa dini zaidi ya Yesu mwenyewe, hasa Kanisa
Katoliki ambalo linaadhimisha kwa njia ya misa takatifu, hivyo ni wajibu wa
wakatoliki kutetea imani yao kwa kuzingatia maneno ya Yesu siku ya alhamisi kuu
akisema kuwa aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu ana uzima wa milele.
“Huo
utajiri wa uwepo wa Ekaristi takatifu ndani ya Kanisa una maana tusipoteze,
hakuna sakramenti kubwa kama Ekaristi takatifu japo zinachangamana, ujueni
utajiri wa Kanisa Katoliki, Ekaristi ni chemchem ambayo inatupa nguvu ya
kutembea katika uzima, hatuwezi kupoteza tunu hiyo. Mlango wa Kanisa Ekaristi
takatifu na sakramenti zozote zile zina uhusiano wa karibu ndio maana hata mtu
mgonjwa anahitaji kupewa mpako wa wagonjwa na padre,” Amesema Dr Rodrigues.
Hata hivyo
kiongozi huyo wa kiroho ametoa wito kwa vijana hao 86 walioimarishwa kwa
sakramenti ya Ekaristi takatifu kujenga imani kwa Yesu wa Ekaristi kiini cha
imani ya Kanisa, kwa kuzingatia kanuni, mafundisho na sheria za Kanisa ikiwa ni
pamoja na kuhudhuria misa za mara kwa mara katika dominika zote sanjari na
ibada ya Ekaristi takatifu ambayo hufanyika siku ya alhamisi ulimwenguni pote.
Comments
Post a Comment