MAGUFULI SAFI, ILA ATUPE KATIBA MPYA-ASKOFU NIWEMUGIZI
ASKOFU Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge Ngara amesema anaridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli kwa nia yake ya kuleta maendeleo nchini, lakini anamuasa aangalie vipaumbele vya wananchi ikiwemo kuwa na Katiba Mpya.
Akizungumza
na Gazeti Kiongozi baada ya kumaliza Mkutano wa zaidi ya asasi 80 za Kiraia wa
kufufua mchakato wa katiba uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam,
Askofu Niwemugizi amesema kuwa, ni wazi Rais John Magufuli anapambana na
ufisadi kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi, anahamasisha wananchi kulipa
kodi kwa maendeleo ya nchi lakini atafanikiwa endapo atakuwa na Katiba ambayo
ndiyo dira ya nchi.
“Ile
tathmini ya mwaka mmoja wa utendaji kazi wa Rais Magufuli ni wazi ilionesha
kazi alizozifanya na mafanikio na wananchi tuliridhika tukaona kuwa kweli
tumepata Rais.
Kazi
ya kupambana na rushwa, maadili kwa viongozi wa umma na amengine mengi, lakini ili
aweze kuyaendeleza awe na katiba madhubuti. Aangalie maoni ya wananchi kupitia
ile iliyokuwa inaongozwa na Warioba aone wanataka kujiongozaje ili awe na Katiba
madhubuti.
Hata
kama kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano si Katiba Mpya lakini Katiba hiyohiyo
ndicho kipaumbele cha watanzania. Ikiwa Rais amewekwa madarakani na wananchi
ana wajibu wa kuangalia vipaumbele vyao. Awasikilize wananchi.
Ieleweke
kuwa, si uchochezi kuhamasisha ama kushawishi Serikali ianze mchakato wa Katiba
Mpya kwani ni kazi ya asasi za kiraia kuchochea maendeleo. Hatuwezi kupata
maendeleo kama hatuna dira ya Taifa. Hatuwezi kufanikiwa kama Taifa kama
tunaongozwa na Katiba yenye mapungufu,” amesema Askofu Niwemugizi.
Amesema
yeye kama kiongozi wa dini alishapinga Katiba pendekezwa kwani ilikuwa haikidhi
mahitaji wa wananchi na ilikiuka maadili ya nchi pamoja na imani yake kwani ilikuwa
haielezi wazi mipaka ya uongozi, uhai wa mwanadamu kwamba unaanzia tumboni.
Amesema
Katiba lazima iwe imebeba maoni ya wananchi ambayo yameainishwa kutokana na
namna wanavyotaka kujiongoza.
“Katiba
si mapendekezo ya Bunge ingawa wabunge ni wawakilishi wa wananchi, lakini
lazima wasikilize wananchi wanataka nini. Ninasisitiza haya kwani hatutaki
Katiba itakayochezewa.
Wabunge
hawana mamlaka ya kurekebisha Katiba kwa mahitaji yao bali lazima iwekwe
kikatiba kuwa, marekebisho ya Katiba ama kipengele katika Katiba kinaweza
kurekebishwa kwa mamlaka ya wananchi. Hatutaki Katiba inayochezewa.
Wananchi
ndiyo watoe maoni kuhusu kubadilisha Katiba si bunge. Vitu vya msingi lazima
wapewe ridhaa na wananchi,” amesisitiza.
Ameziasa
taasisi za kiraia kuacha kuogopa kuzungumza yale mahitaji muhimu ya wananchi
kwani ni wajibu wao. Wasiogope kuitwa wachochezi kwa kutaka maendeleo ya nchi.
Na Sarah Pelaji,
Dar es Salaam
Comments
Post a Comment